Dk Bashiru: Tukishindwa kusimamia haki mtutose

Moro/Dar. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema kama chama hicho kitashindwa kusimamia haki na kuwapatia maendeleo wananchi ni bora wakakitosa katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na hakitakuwa na haki ya kuongoza nchi.

Amesema CCM inapaswa kusimamia misingi ya haki na usawa kwa wananchi na kama ikishindwa kufanya hivyo ni wazi kwamba itatetereka na kukumbatia watu wanaotenda dhuluma.

Dk Bashiru alisema hayo jana akiwa wilayani Kilosa wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za wilaya na Mkoa wa Morogoro, pamoja na wananchi wa kata tisa za wilaya hiyo.

Kauli hiyo ya mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ameitoa ikiwa zimepita siku chache tangu baadhi ya wabunge wa upinzani kuitaka Serikali bungeni kuruhusu mikutano ya hadhara ili wajiandae na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika mkutano huo, Dk Bashiru alisema CCM ya sasa inawasikiliza wananchi na kuwatetea katika kila nyanja, hivyo kama itashindwa kusimamia hayo ipasavyo haitakuwa na haki ya kuongoza.

“Uchaguzi unakuja wa serikali za mitaa, ni bora tukapigwa katika chaguzi kama tutashindwa kusimamia misingi ya haki na usawa kwa wananchi wetu, lakini naimani wananchi wetu wana imani na chama katika kuwatetea,” alisema.

Alisema kazi ya CCM sio tu kupigiwa kura, bali ni pamoja na kusimamia masuala mbalimbali ya utawala bora, siasa na hata maendeleo kwa wananchi na kwamba ikishindwa kufanya hivyo hakutakuwa na sababu ya kuongoza nchi. Alisema katika chaguzi zinazokuja, ni lazima wachaguliwe viongozi wenye uwezo wa kusimamia haki na masilahi ya wananchi kuliko wale wanaotanguliza masilahi yao binafsi.

Dk Bashiru alisema kwa sasa kila mwenye mali ni lazima ijulikane alizipataje na iwapo ni kwa njia ya halali ataeleza hata kama ni mtu mwenye utajiri wa namna gani.

Alisema watu wote wenye utajiri usioeleweka namna walivyoupata hawatatoka salama.

“Nimesikia watu wakinong’ona kuwa nakuja kila mara Kilosa, hii Kilosa ndiyo inaongoza kwa migogoro ya ardhi, hivyo kupitia CCM ujumbe huu wa haki na usawa katika ardhi utafikia nchi nzima kupitia wilaya hii ya Kilosa na ndiyo naifanya kama mfano.”

Awali, katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka alisema wapo baadhi ya viongozi siyo waaminifu na hawana nia njema na chama hicho wakikitumia kama mwamvuli wa kufichia maovu yao na mkoa wake umejipanga kuwafichua.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoi alisema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na ile ya siasa tayari wameshawabaini baadhi ya viongozi wanaosababisha migogoro ya ardhi kwa kuiuza kinyume na taratibu.

Alisema wamepanga kuanza kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

Wapinzani wampa mtihani

Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa amemsikia Dk Bashiru na kumtaka kama ni mkweli na ana dhamira ya anachokisema aanze na Spika wa Bunge.

“Kutetea wananchi ni pamoja na kuwapa wanachokiamini (kuwa) kipo sahihi ikiwamo Katiba mpya waliyoitolea maoni kwa miaka miwili,” alisema Mrema.

Mrema aliungwa mkono na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT - Wazalendo, Ado Shaibu aliyesema anafuatilia ziara za Dk Bashiru aliyewahi kumfundisha, lakini akasema kwamba haamini kama yote anayoyazungumza anafanya hivyo kwa dhati na hakika.

Alisema Dk Bashiru anazungumzia masilahi ya wakulima na wafanyakazi ilhali viongozi wenzake ni watu wa vijembe na siasa zisizoeleweka na kwamba kukosa uwiano huko ni dalili kwamba anayoyasema ni hadaa.

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema hashangazwi na kauli hizo na kwamba ni aina ya siasa za CCM unapokaribia uchaguzi, lakini akadai kuwa wananchi wanaosemwa kuwa ni wanyonge wanaotaka kuwasaidia, hawapati misaada hiyo zaidi ya wale wa mjini.