Dk Biteko aeleza mikakati usambazaji gesi asilia mikoa minne

Muktasari:

  • Asema kazi zitakazotekelezwa ni kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, usanifu wa kihandisi, na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga na Kongani ya Viwanda ya Kwala mkoani Pwani.

Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.

Hayo yamo kwenye hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo Aprili 24, 2024.

Amesema kazi zitakazotekelezwa ni kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, usanifu wa kihandisi, na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga na Kongani ya Viwanda ya Kwala mkoani Pwani.

Zingine ni kukamilisha ujenzi wa vituo vya CNG (kituo mama katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vituo vidogo vya Kairuki na Muhimbili, mkoani Dar es Salaam.

Dk Biteko amesema Serikali imejipanga kununua vituo vitano vya CNG vinavyohamishika vitakavyotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam.

“Sekta binafsi itaendelea kushiriki katika ujenzi wa vituo vya CNG na karakana za kubadilisha mifumo ya matumizi ya nishati ya gesi asilia kwenye magari,” amesema.

Dk Biteko amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) litakamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa usambazaji wa gesi asilia chini ya ufadhili wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Amesema nyumba 980 zitaunganishwa katika mikoa ya Lindi na Pwani; na kuanza awamu ya pili ya mradi huo kwa kuendelea kusambaza gesi asilia maeneo ya Mkuranga, mkoani Pwani.

“Katika mwaka 2023/24 Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuendeleza sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini katika maeneo ya utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta na gesi,” amesema.

Katika utekelezaji, Dk Biteko amesema “ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia (CNG) katika magari uliendelea kwa kushirikisha pia sekta binafsi.”

Amesema TPDC na Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA) ziliendelea na taratibu za kumpata mshauri mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa michoro ya kihandisi na tathmini ya athari ya mazingira na jamii ili kuwezesha GPSA kujenga vituo vya CNG katika bohari za Dar es Salaam na Dodoma.

Amesema hiyo ni hatua ya kuwezesha vyombo vya moto vinavyomilikiwa na Serikali kutumia CNG.

Dk Biteko amesema sekta binafsi iliendelea kutumia fursa ya matumizi ya CNG katika vyombo vya moto kwa kujenga vituo Dar es Salaam na Pwani, pamoja na karakana nane za kubadilisha mifumo ya matumizi ya CNG kwenye magari, ambayo ni nyenzo muhimu ya kuchochea matumizi ya gesi katika magari.

“Hatua hizi zimeendelea kuimarisha matumizi ya gesi asilia asilia katika magari,” amesema