Dk Buriani ataka uchunguzi kuwalinda nyuki

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian

Muktasari:

  •  Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Buriani amezitaka taasisi za utafiti wa wadudu, kuchunguza matumizi ya salfa wakati wa kunyunyuzia  mikorosho  kama haina athari kwenye ufugaji nyuki.


  

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Buriani amezitaka taasisi za utafiti wa wadudu, kuchunguza matumizi ya salfa wakati wa kunyunyuzia  mikorosho  kama haina athari kwenye ufugaji nyuki.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuona kama kuna athari ili hatua stahiki zichukuliwe.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Tabora na  Uyui, amesema makundi ya nyuki yasije yakapotea kutokana na matumizi ya viuatilifu ikiwemo salfa ambavyo vinaweza kusababisha vifo kwa nyuki wakati wanakwenda kwenye maua kutafuta chavua.

Amesema asali ni nembo na kielelezo kikubwa cha Mkoa wa Tabora kwa hiyo shughuli yoyote ya kuathiri makundi ya nyuki si vyema ikafanyika.

Amesema kuwa  nyuki wanazo faida nyingi ikiwemo uchavushaji mimea ya mazao mbalimbali na uzalishaji wa asali na mazao ya nyuki.

"Vitendo vya kuhatarisha maisha yao vinahatarisha pia maisha ya wakazi wa Tabora kwa kupoteza utajiri wa asili wa asali na kudhoofisha uzalishaji wa mazao mashambani," amesema.

Amebainisha kuwa  kimsingi hapingi ulimaji wa zao la korosho katika Mkoa wa Tabora, bali kinachotakiwa kuangaliwa kwa upana faida na hasara zitakazopatikana kutokana na matumizi ya viuatilifu kwenye korosho dhidi ya uzalishaji wa asali.

Ameongeza kuwa ni vyema watafiti wa wadudu na wale wa kilimo wakashirikiana ili kuja na msimamo wa aina moja katika suala la kilimo cha korosho Mkoani Tabora.

Mmoja wa wafanyabiashara mkoani Tabora, Hamad Salum amesema yeye analima korosho lakini hatumii salfa kwani inahatarisha usalama wa nyuki.

"Situmii Salfa kwa vile nafahamu na wakulima wa korosho wasitumie kabisa ili kutowadhuru nyuki," amesema Salum.