Dk Chana ataka Watanzania kulinda mila, utamaduni

Muktasari:
- Wakati tamasha la pili la kitaifa la Utamaduni likifanyika mkoani hapa, Watanzania wamekumbushwa kuenzi utamaduni wa kiafrika na kuacha kuiga ule unaotoka nje.
Njombe. Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dk Pindi Chana amezindua tamasha la pili la kitaifa la utamaduni linalofanyika mkoani hapa huku akiwataka Watanzania kulinda mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania ambao una maadili mazuri.
Pia amewataka watanzania kuacha kufuata utamaduni wa kigeni ambao unasababisha mmonyoko wa maadili.
Akizungumza katika ufunguzi wa tamasha hilo, Dk Chana amesema utamaduni unaotoka nje ya nchi unawatoa watanzania kwenye reli hivyo wakati imefika wa kukumbushana kuulinda na kuundeleza utamaduni uliopo nchini.
"Kauli mbiu ya tamasha hili ni utamaduni ni msingi wa maadili tuulinde na tuuendeleze kauli mbiu hii imekuja wakati muafaka kwani inatukumbusha kurudi kwenye misingi ya utamaduni wetu halisi badala ya kukumbatia tamaduni za kigeni ambazo nyingine hazikubaliki na tamaduni zetu," amesema Dk Chana.
Amesema endapo utamaduni wa Tanzania usipolindwa Watanzania watatoka kwenye reli na kuanza kuiga utamaduni ambao haufai kwenye jamii.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema tamasha hilo la utamaduni litafanyika kwa siku tatu ambapo shughuli mbalimbali za sanaa zitafanyika.
"Kutakuwa na mashindano ya vyakula vya asili, ngoma za asili na maonyesho ya shughuli za sanaa na mdahalo mahususi kwa ajili ya kujadili namna ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili" alisema Yakubu.
Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka alisema tamasha hilo limetoa fursa kwa wananchi mkoani Njombe kufanya biashara mbalimbali ambazo zitawaingizia kipato na kukuza uchumi wao.