Dk Hoseah: Tutapigania uwakili wa Fatma Karume

Wednesday April 07 2021
hoseapic

Mgombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah

By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah amesema endapo atachaguliwa kuwa bosi wa chama hicho atapigania na kumtetea Fatma Karume arejeshewe uwakili wake.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 7, 2021 Dk Hoseah amesema, “sitosema sana kwa sababu jambo likiwa mahakamani hupaswi kulizungumzia lakini TLS tupo nyuma ya Fatma Karume kutetea haki yake ya  msingi anapopeleka shauri lake kwenye mahakama ya rufaa.”

Wengine watakaowania urais wa TLS mbali na msomi huyo katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 15 na 16, 2021 ni wakili maarufu Tanzania, Albert Msando;  Flaviana Charles, Shehzad Wall na rais wa zamani wa chama hicho, Francis Stolla.

Fatma Karume asimamishwa uwakili, mwenyewe asema ataendelea kupambana

Septemba 23, 2020 kamati  ya maadili ya mawakili nchini ilimuondoa Fatma ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya Sita ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Aman Abeid Karume, katika orodha ya mawakili wa kujitegemea baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya taaluma.

Fatma anadaiwa kukiuka maadili kwa kutoa maneno mabaya dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakati akiwasilisha hoja zake katika kesi iliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Advertisement

Katika maelezo yake Dk Hoseah amesema katika uongozi wake wa mwaka mmoja atahakikisha tuhuma zozote zinazowakabili mawakili zinashughulikiwa ndani  ya TLS, zitakwenda ngazi ya  juu endapo chama hicho kitashindwa.

 “Tutahakikisha yeyote anayetuhumiwa kwa maadili tutaanza kumshughulikia ndani ili wenyewe tujirekebishe huu ndiyo msisitizo wangu na sheria haizuii.” Amesema Dk Hosseah ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa mwanzo mzuri wa uongozi wake huku akiwabeza wanaomuita mzee “kuna wenzangu wazee sana walioitumikia na kuhudumu urais wa  TLS kuliko hata mimi, sasa wanaposema nimezeeka nastahili kustaafu nawashangaa hivi mimi nimezeeka?”

“Nimestaafu lakini bado sijachoka. Sasa nawashangaa ooh nimezeeka, nimezeeka vipi? Hata kutoa mawazo yangu nimezeeka, tutabishana sana kwa hili lakini nipo tayari kuwatumikia.”

Usikose kusoma mahojiano ya kina ya Dk Hoseah kwenye gazeti la Mwananchi la Alhamisi Aprili 8, 2021Advertisement