Fatma Karume asimamishwa uwakili, mwenyewe asema ataendelea kupambana

Friday September 20 2019
pic fatma

Dar es Salaam. Fatma Karume amesimamishwa uwakili na Mahakama Kuu kwa madai ya kuishambulia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na atafikishwa kamati ya maadili ya mawakili kujadiliwa.

Karume amesimamishwa leo Ijumaa Septemba 20, 2019 huku sababu ikitajwa kuwa ni alichokizungumza katika kesi iliyofunguliwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi aliyeteuliwa na  Rais John Magufuli Februari Mosi, 2018.

Shaibu amesema mawakili wa Serikali walilalamikia maneno yaliyoandikwa na Fatma wakati wanafungua kesi hiyo Mahakama Kuu.

“Maneno yenyewe aliyoyatumia ni commitment yake ya kwamba ‘hata kama kesi hii itashindwa ataendelea kupambana nayo, Rais akiondoka madarakani mwaka 2020 au kama ataondoka 2025 au kama mahakama itabadilika ataendelea kupambana’.”

“Na kwamba upande wa mwanasheria mkuu wanamtetea Rais Magufuli kwa hiyo wanasema ni kama amewa-attack, amemu-attack Mwanasheria Mkuu, hivyo wakasema inabidi apelekwe kwenye kamati ya maadili ya mawakili na wakati suala lake likijadiliwa atakuwa amesimamishwa uwakili,” amesema Shaibu.

Shaibu amesema uamuzi huo umetangazwa leo huku madai katika kesi ya msingi yakitupiliwa mbali kwa hoja kwamba Rais hawezi kusimamishwa mahakamani.

Advertisement

Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo dhidi yake, Fatma amesema anakusudia kufungua kesi Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) kupinga kusimamishwa kwake uwakili bila kupewa nafasi ya kujieleza.

Amesema hashangai kusimamishwa au kuvuliwa uwakili kwa sababu yapo mambo mengi yaliyotokea nchini, “Mimi sishangai kuvuliwa au kusimamishwa uwakili, pengine Mungu hataki niendelee kuwa huko, pengine anataka niingie kwenye siasa au nifanye kitu kingine tofauti. Nitakaa na kutafakari.”

Amesema hatua hiyo haitabadilisha maisha yake bali itabadilisha uwezo wake wa kusimamia kesi za kikatiba, akibainisha kuwa bado ni wakili  Zanzibar,  ana ofisi na ataendelea kusimamia kesi za kikatiba.

Advertisement