Dk Kigwangalla adaiwa kumpiga mfanyakazi wake

Mbunge wa Nzega Vijijini Dk Hamisi Kigwangala

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefungua majalada matatu tofauti na kuanza uchunguzi kuhusu taarifa tatu tofauti zinazomhusu Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk Hamisi Kigwangalla.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema jalada la kwanza ni la uchunguzi kuhusu Kigwangalla kudaiwa kumshambulia kwa makofi na mateke mmoja wa wafanyakazi wake, Jumanne Misango katika tukio lililotokea Mei 22, mwaka huu.

Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea eneo la jineri ya kuchambua pamba iliyoko Nyambiti, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza inayomilikiwa na Dk Kigwangalla ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii.

“Jalada la pili la uchunguzi limefunguliwa dhidi ya Jumanne Omari kwa kutoa taarifa za uongo polisi kuwa alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi mguuni na Dk Kigwangalla, madai ambayo uchunguzi wa polisi na ripoti ya daktari, ikiwemo picha za X-Ray umebaini kuwa ni uongo,’’ alisema Kamanda Mutafungwa.

Alitaja jalada la tatu la uchunguzi kuwa ni la madai ya tukio la wizi wa mali mbalimbali, ikiwemo nyaya na mashine, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh28.5 milioni uliotokea katika jineri inayomilikiwa na Dk Kigwangalla.

“Mei 22, 2023, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za wizi katika kiwanda cha kuchambua pamba kinachomilikiwa na mbunge Kigwangalla, askari walipofika walimkuta mbunge huyo ni miongoni mwa waliochukuliwa maelezo kwa ajili ya uchunguzi wa wizi huo wa mali yenye thamani ya zaidi Sh28.5 milioni.

“Baada ya kuchukua maelezo na kuondoka eneo la tukio, Polisi wilayani Kwimba ilipokea taarifa nyingine kuwa mmoja wa wafanyakazi wa jineri hiyo, Jumanne Omari ambaye ni mlinzi na mtunza stoo alishambuliwa, kujeruhiwa na mbunge Kigwangalla,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Alisema askari polisi walikwenda haraka eneo la tukio, lakini wakiwa njiani walikutana na Kigwangalla na kumweka chini ya ulinzi katika kituo cha polisi Hungumalwa, lakini walipofika kiwandani wakamkuta Jumanne aliyedaiwa kujeruhiwa akiwa mzima na hana jeraha lolote mguuni.

Alisema licha ya kukosekana kwa viashiria vya shambulio la risasi, hata waliokuwepo eneo la tukio walikana kuona tukio la shambulio wala mlio wa risasi.

‘’Kilichobainika ni kwamba wawili hao, yaani mbunge Kigwangalla na mfanyakazi wake walikuwa na mzozo unaohusishwa na tukio la wizi; lakini madai ya shambulio la risasi halikuwepo si tu kwa uchunguzi wa polisi na ushuhuda wa waliokuwepo, bali pia kwa taarifa ya daktari aliyemchunguza Jumanne Omari baada ya kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu,’’ alisema Kamanda Mutafungwa.

Alisema katika maelezo yake, Omari alidai kushambuliwa kwa makofi na kukanyagwa mguuni, hali iliyoilazimu polisi kumpa fomu ya matibabu, huku viatu na soksi zake alizovaa vikichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusu madai ya kupigwa risasi.

“Kutokana na madai ya Omari kushambuliwa kwa makofi na mateke, Polisi tunachunguza suala hilo kwa sababu ni kosa kisheria mtu kumshambulia mwingine. Tukikamilisha uchunguzi wa matukio yote matatu tutawasilisha majalada yote Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali kwa uamuzi na hatua zaidi za kisheria,’’ alisema Kamanda Mutafungwa.

Juhudi za kuwapata Kigwangalla na Omari kuzungumzia matukio haya zilishindikana baada ya simu ya kiganjani ya waziri huyo wa zamani kuonekana inaongea muda mrefu, huko namba ya Omari anayedaiwa kuishi wilayani Kwimba haikupatikana mara moja.