Dk Kihamia: Filamu ya Royal Tour kuipaisha Tanzania

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk Athumani Kihamia

Muktasari:

Imeelezwa kuwa Filamu ya royal tour itakayozinduliwa Aprili 28, 2022 mkoani Arusha na Rais Samia Suluhu Hassan itapaisha mapato ya nchi siyo kwa kupitia utalii pekee bali katika nyanja zote ikiwemo sekta ya madini, kilimo, biashara na michezo.

Arusha. Imeelezwa kuwa Filamu ya royal tour itakayozinduliwa Aprili 28, 2022 mkoani Arusha na Rais Samia Suluhu Hassan itapaisha mapato ya nchi siyo kwa kupitia utalii pekee bali katika nyanja zote ikiwemo sekta ya madini, kilimo, biashara na michezo.

Hayo yamebainishwa leo na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk Athumani Kihamia wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa filamu hiyo mkoani hapo.

Dk Kihamia amesema kupitia filamu hiyo mapato ya nchi yataongozeka kutokana na watu wa  mataifa mengi duniani kuifuatilia kwa karibu  Tanzania na kujionea vivutio adimu vilivyopo na hatimaye kugundua fursa zilizopo nchini na kuwekeza  kisha kupanua wigo wa ajira.

"Hali hiyo itafanya hata wanamichezo wetu watajulikama zaidi na kupata fursa ya kwenda nje ya nchi kama wanamichezo wa kimataifa," amesema

Amefafanua kuwa kwa sasa wananchi wengi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wamefurika mkoani hapo kujionea filamu hiyo ya kihistoria iliyochezwa na Rais Samia ambaye ni mbunifu na mwenye upeo wa diplomasia ya kiuchumi.

"Wananchi wa mkoa wa Arusha wamefurahia sana uamuzi wa Rais kuchagua kuzindua filamu hiyo ya kihistoria katika mkoa huu wenye utajiri mkubwa wa madini na utalii," amesema na kuongeza

"Wafanyabiashara wanaojihusisha na shughuli za kuelekeza watalii, mahoteli, na biashara mbalimbali zikiwemo mbogamboga na matunda yanayosafirishwa nje ya nchi, wafugaji na hata wavuvi wameonekana wenye shauku ya kuona matunda hayo ya utalii yanaotangazwa kwa weledi mkubwa chini ya uongozi wa Rais Samia," amesema

Dk Kihamia amesema wao kama serikali ya mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na wadau na wananchi wamejipanga kuhakikisha kwamba juhudi hizo za Rais na serikali yake zinaleta athari chanya kwa wananchi na wadau wa utalii.

"Tunataka juhudi hizi za Rais zinaleta matokeo chanya kwa wananchi na wadau wote wa utalii kwa ujumla ukizingatia kwamba asilimka 80 ya mapato ya utalii wote nchini yanapatikana Arusha.

"Wananchi wanaombwa kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo endelevu kwa haraka huku tukiwaombea viongozi wetu wakuu chini ya Rais Samia kuzidi kutatua changamoto mbalimbali kwa mujibu wa malengo na madhumuni ambayo serikali awamu ya sita inalenga kuyafikia," amesema

Aidha amesema kuwa Mkoa wa Arusha licha ya kunufaika na utalii, umepiga hatua kubwa katika nyanja za elimu, afya, miundombinu ya barabara,maji na ujasiriamali.

"Tutazielekeza Halmashauri zetu kuchungulia kwa kina fursa hizi za utalii ili kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani kwa lengo la kuongeza uwezo wa kutoa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Arusha," amesema