Dk Mollel agoma kuzindua muongozo wa afya ya lishe

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel

Muktasari:

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amegoma kuzindua muongozo wa afya ya lishe kijijini, akisema ulitakiwa uzinduliwe kijijini na sio mjini.

Dodoma. Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amegoma kuzindua muongozo wa afya ya lishe kijijini, akisema ulitakiwa uzinduliwe kijijini na sio mjini.

Muongozo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Afya ya Lishe nchini (TFNC) ulikuwa uzinduliwe leo Alhamisi juni 20, 2022 jijini Dodoma

Dk Molel ambaye amemuwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema uzinduzi huo ulitakiwa  ufanyike kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na ukosefu wa afya ya lishe vijijini na sio kwenye hoteli ya kifahari.

"Nimekataa kuzindua kwasababu ilitakiwa ufanyike kijijini na kuna filamu ambayo inawahusu watu wa vijijini kwahiyo tulitegemea kwamba wenzetu wangepeleka hili suala kijijini hasa kwenye kijiji ambacho kimeathirika zaidi na lishe" ameongeza

Dk Mollel amesema kuwa kukataa kuzindua mungozo huo ni ujumbe kwa taasisi zote ambazo zinatoa misaada kuwa ni wakati wa kwenda mitaani (Field) kwani Rais Samia Suluhu Hassan  amekuwa anahangaika kuboresha mahusiano na wadau ili kuleta fedha nchini na lengo lake ni fedha hizo ziwafikie wananchi.

"Rais Samia anapoboresha uhusiano wetu na mataifa mengine anajua fika kuwa mwisho wa siku tunaingiza fedha nyingi ambazo lengo lake ni ziende kwa wananchi wanyonge na yeye ameonyesha mfano kwenye fedha za Uviko" ameongeza

“Tunataka mfano aliouonyesha kwenye Sh1.3 trilioni, wa kuepeleka fedha kwa wananchi, tunataka kila taasisi yetu ya afya, kila mtaalamu na kila NGO's  washauri vizuri wanapokwenda kukutana na wadau washauri vizuri,” amesema Dk Mollel

Amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya pamoja na wataalamu wa afya ya lishe wakae na TFNC na waje na mawazo ya kuweka kwenye mpangilio unaofaa.