Dk Mollel: Serikali inatafuta fedha Bima ya Afya kwa Wote

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George.

Muktasari:

  • Japo haikutajwa siku, Serikali imesema inakusudia kurejesha Muswada wa bima ya Afya Wote Bungeni kwa mara nyingine, ikisisitiza tatizo lipo kwa wadau ambao wana mawazo kinzani.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Serikali inakusudia kurejesha bungeni Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote.

Japo hakutaja ni Bunge lipi muswada huo utarejeshwa, amesisitiza Serikali haina tatizo bali wadau ndiyo wanaoleta ukinzani wa mawazo kwenye mfumo huo.

Ikumbukwe Februari mwaka huu, licha ya kuwekwa katika ratiba ya mkutano wa Bunge la 10 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa kwa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC) uliondolewa katika vikao vya  kwa kile kilichobainika ni kutokuwepo kwa chanzo endelevu cha fedha kutekeleza mpango huo.

Leo Septemba 25, 2023 akizungumzia mafanikio ya sekta ya afya chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na mambo mengine,  Dk Mollel amesema kuhusu Bima ya Afya kwa Wote  Serikali inafikiria chanzo cha upatikanaji wa fedha.

"Hatuwezi kufanya mfumo wa afya kwa wote utembee bila kuwa na bima ya afya kwa wote, tunajipanga kwa ajili ya kupeleka Muswada tena bungeni, lakini nisiseme muswada utakwenda lini kwasababu Bunge ndilo linaamua," amesema.

Akizungumzia maboresho yaliyofanyika sekta ya afya, Dk Mollel amesema tayari Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa 727 ambazo zitasambazwa kila wilaya.

"Pia  miondombinu ya kutoa huduma za dharura' imeboreshwa ambapo majengo 128 yamejengwa katika hospitali ngazi ya taifa, maalumu, kanda na mkoa na  vimewekwa vifaa hadi kufikia Machi 2023 na vyumba 73 vya kuangalizia wagonjwa mahututi vimejengwa ngazi ya Taifa hadi wilaya,"amesema.

Mafanikio mengine aliyoitaja Dk Mollel ya Rais Samia kwenye sekta ya afya ni upatikanaji wa dawa ambapo Sh442 bilioni zilitengwa.

Amesema kwa mwaka 2022/2023 Serikali ilitoa zaidi ya asilimia 90 ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa (Sh190 bilioni).

Kwa upande wa vituo vya afya, Dk Mollel amesema kuanzia Julai mwaka jana hadi Machi 2023 mwaka huu vituo vimeongezeka kufikia 11,040 ikilinganishwa na vituo 8,549 mwaka 2021

"Kati ya hivyo hospitali ni 430 vituo vya afya vilikuwa 1,030, zahanati 7,458, kiliniki zilikuwa 906 na maabara binafsi 1,216," amesema.