Danadana bima ya afya kwa wote zimetosha
Kwa zaidi ya miaka 10 sasa kumekuwa na danadana ya kukamilika kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.Juzi kwa mara nyingine muswada wake umekwama kuwasilishwa bungeni kama ilivyoahidiwa na Serikali.
Tangazo la kutowasilishwa bungeni kwa muswada huo lilitolewa na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, huku akiahidi kuwa utawasilishwa wakati mwingine, pale kamati ya Bunge itakapokamilisha majadiliano na Serikali, kuhusu eneo la bajeti na vyanzo vya fedha vitakavyowezesha utaratibu huo kuwa endelevu.
Muswada huo uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza Septemba 23 mwaka jana ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa kwa siku mbili kabla ya kupitishwa katika kikao cha Bunge kilichoisha jana, kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kusainiwa kuwa sheria.
Kwa mara ya kwanza, muswada huo ulikwama kusomwa kwa mara ya pili katika Bunge la Novemba mwaka jana.
Tunachukua fursa hii kwanza kuipongeza Serikali kwa wazo na uamuzi wa kutunga sheria itakayomhakikishia kila Mtanzania huduma bora ya afya bila kujali uwezo wake kiuchumi kupitia Bima ya Afya kwa Wote.
Pamoja na pongezi, tunaamini muda sasa umefika kwa Serikali kumaliza hili tatizo la danadana kwenye hatua hii muhimu ya muswada utakaowezesha Taifa letu kuwa na sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Tunasema ni danadana kwa sababu hatua zote muhimu, kuanzia maoni ya wadau na ushauri wa kitaalamu tayari zimekamilika; kilichosalia ni Serikali kuyaunganisha pamoja ili kuwezesha sheria hiyo siyo tu kutekelezeka, bali pia kujenga misingi itakayodhibiti hila yoyote katika utekelezaji wake.
Kama ambavyo wadau wa sekta ya afya na sheria wanavyopendekeza, msingi wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unapaswa kujenga katika sheria, badala ya kanuni zinazotungwa na waziri ili kuepuka athari kama zilizojitokeza kwenye tozo.
Kuhusu bajeti na vyanzo vya mapato kugharamia Bima ya Afya kwa Wote, ni vema Serikali ikaiga na kutumia mbinu inayotumika sasa ya kutafuta fedha za kugharamia usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA kwa kuweka tozo ndogo kwenye bidhaa za anasa kama peremende, sigara, vinywaji vikali na laini.
Kama jina lilivyo; Bima ya Afya kwa Wote inatakiwa kujumuisha kila mtu bila kujali uwezo wake kiuchumi.
Ni wajibu wa Serikali ambayo ndiyo imepewa dhamana ya kukusanya kodi kuhakikisha uwezo mdogo kiuchumi, hauwakwamishi Watanzania kupata huduma bora za afya kupitia mfumo huo ambao tayari unatumika sehemu mbalimbali duniani.
Kwa mfano, tukiweka utaratibu wa tozo hata ya Sh50 kwenye bidhaa za anasa, ni dhahiri tutakusanya mamilioni ya fedha za kulipia gharama ya Bima ya Afya kwa Wote kwa watu wasio na uwezi kiuchumi.
Tufanye hivyo kupata tiba ya vikwazo vinavyoshuhudiwa hivi sasa katika utekelezaji wa Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) ambayo licha ya mtu kutakiwa kulipa Sh30, 000 pekee kwa ajili ya huduma kwa watu sita, bado wapo watu wasiomudu kulipia.
Uhakika wa bajeti na fedha za kugharamia Bima ya Afya kwa Wote utawahakikishia Watanzania huduma bora za afya kuanzia kwenye vituo vya umma na binafsi bila vikwazo, kwa sababu watoa huduma watalipwa kwa wakati tofauti na hali ilivyo sasa ambapo malipo yanaweza kuchukua miezi kadhaa.
Huduma bora ya afya siyo tu ni haki kwa kila Mtanzania, bali pia ni miongoni mwa mahitaji ya kila binadamu. Serikali ihakikishe kila mwananchi ana afya bora.