Dk Mpango anavyorejesha mjadala wa kifo cha Magufuli, ukimya wa Kinana
Makamu wa Rais, Philip Mpango
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Phillip Mpango, alirejea nchini Jumamosi, Desemba 9, 2023. Hakuonekana kwenye uso wa jamii kwa zaidi ya mwezi mmoja. Jumapili, Desemba 10, 2023, Dk Mpango, alihudhuria ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege, Dodoma.
Kisha, jioni (Desemba 10), Mpango alikuwepo Ikulu, Chamwino, Dodoma, kwenye hafla ya kupokea michango ya maafa ya maporomoko ya matope, yaliyotokea huko Hanang mkoani Manyara.
Kuonekana kwake kulimfanya Dk Mpango awe “mtu wa siku”. Maneno yalikuwa mengi kuhusu kutoonekana kwake. Wapo waliosema alikuwa taabani, wengine wakamtangulizia mauti.
“Wapo walisema mzee amekata moto. Wengine wakachukua picha yangu, wakaweka na mishumaa,” alisema Mpango kanisani. Maneno kama hayo, aliyarejea Ikulu, aliposimama ili kumkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Ujumbe wa Dk Mpango kwa Watanzania ni kutumia vizuri mitandao ya kijamii. Alionya kuwa mwaka 2021 alipozushiwa kifo, dada yake aliyemlea, ambaye alikuwa na umri wa miaka 80, alianguka.
Ni sahihi kuwa uzushi ulikuwa mwingi kuzunguka kutoonekana kwa Dk Mpango. Baada ya kila kilichozushwa, hatimaye alijitokeza akiwa na afya njema. Akasema alikuwa nje ya nchi kwa shughuli maalumu.
Chanzo cha uzushi
Rais wa 28 wa Marekani, Woodrow Wilson, alipata kuandika: “Serikali inapaswa yote kuwa nje na sio ndani. Inatakiwa kusiwe na mahali popote, chochote kinaweza kufanyika ambacho yeyote hajui.”
Maneno ya Wilson yanajenga ukumbusho kuwa Serikali inatakiwa kuendeshwa kwa uwazi. Wananchi hawapaswi kuwekwa katika mazingira ambayo mambo yanafanyika pasipo wao kufahamu.
Kutoka nukuu ya Wilson, kuielewa mantiki na mwongozo wake, sasa tujadili chanzo cha uzushi kuhusu Dk Mpango. Kwanza, hatubishani kuwa kweli hakuonekana kwa zaidi ya mwezi mmoja. Pili, sio uongo, watu walizusha kumhusu yeye.
Aliyesababisha uzushi huo ni nani? Dk Mpango ni Makamu wa Rais. Kiongozi namba mbili kwenye nchi. Haonekani kwenye uso wa jamii. Serikali haitoi taarifa yoyote huku familia nayo imenyamaza. Mhusika naye hatokezi kuongea chochote kumhusu wala uzushi.
Anatokea mtu anaandika tanzia. Nchi inaingia kwenye taharuki. Hofu inatanda. Sauti zinaongezeka kuhoji alipo Dk Mpango. Ukiwaza vizuri, unapata jibu kuwa chanzo cha kila uzushi kuhusu Dk Mpango ni Serikali yenyewe.
Kama Serikali na taasisi ingekuwa inaendeshwa kwa mwongozo wa Wilson, uzushi usingepewa nafasi. Serikali ilipaswa kutoa taarifa kwa umma kuhusu safari ya Dk Mpango. Kisha, wangetokea wazushi, wangepuuzwa.
Haina maana walioandika tanzia za utunzi kuhusu Dk Mpango hawana makosa. Wamekosea sana. Hata hivyo, Serikali inapapaswa kubeba lawama kwa kutengeneza mazingira yenye kuruhusu uzushi kupenyezwa.
Uzushi hupata nguvu pale mambo yanapokuwa yamejificha. Uzushi hutiliwa shaka haraka na kuwa dhaifu, endapo watu watakuwa wanaujua ukweli. Hivyo, taharuki kuhusu mahali alipokuwa Dk Mpango ina mbeleko ya walioamua kutosema ukweli tangu awali na kukaa kimya.
Dk Mpango ni mfanyakazi wa Watanzania. Wanamlipa mshahara, analindwa na kuhudumiwa na vyombo ambavyo vinakasimu mamlaka za wananchi.
Je, kumficha mwajiri taarifa kuhusu alipo mfanyakazi wake hilo siyo kosa?
Hadi sasa wananchi hawajaambiwa Dk Mpango alikuwa wapi. Alikwenda kufanya nini na matokeo ya alipokwenda ni yapi? Mwongozo wa Wilson, kuiondoa Serikali ndani na kuiweka hadharani ndiyo msingi wa uwazi na uwajibikaji.
Muhimu kwa Serikali ni kuwa inapotoka na kutoa taarifa zake mapema, inajijengea mamlaka ya habari zake. Inapochelewa kisha watu wengine wakasambaza uzushi, Serikali inapokanusha, inakosa mamlaka. Inaonekana inafanya propaganda.
Suala la Dk Mpango, kila kauli ya kiongozi wa Serikali ilionekana ni propaganda mpaka mwenyewe alipojitokeza. Ni udhaifu mkubwa kwa Serikali kukosa mamlaka kwenye taarifa zenye kuhusu viongozi wake au masuala yake yenyewe.
Katiba ya Tanzania, ibara ya 18, inaeleza haki ya watu kuomba na kupewa taarifa. Wananchi wanahoji alipo kiongozi wao, hawapewi taarifa yenye kunyooka. Kumbe sasa, suala la Dk Mpango siyo tu ukaidi wa mamlaka kwa wananchi, bali kuna namna Katiba inapuuzwa.
Mawasiliano ni karma
Thich Nhat Hanh, alifariki dunia Januari 22, 2022. Wavietnam na Wabudha wa Magharibi, humwita “Baba wa Tafakuri” – “Father of Mindfulness”. Moja ya zawadi za Nhat Hanh ni kitabu chake “The Art of Communicating” – “Sanaa ya Kuwasiliana.”
Sura ya nane ya kitabu hicho, Nhat Hanh aliandika kuwa mawasiliano huunda mwendelezo wa mtu. Jinsi mtu anavyowasiliana na wengine, huumba saini yake. Alikwenda mbele na kueleza kwamba mawasiliano ni “karma”, yaani jinsi unavyowasiliana, itakurudia kwa wema au ubaya.
Machi mpaka Juni 2017, kulikuwa na maswali mengi juu ya aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana. Alikuwa kimya, hakuonekana ofisi za chama akitekeleza wajibu wake, wala haikuelezwa alipokuwa.
Maswali yakaibuka juu ya mahali alipokuwa. Wakatokea watu wakavumisha kuwa Kinana alijiuzulu na kujiweka kando na majukumu ya chama. Aliyekuwa Mwenyekiti CCM, Dk John Magufuli, alijitokeza na kusema Kinana alikuwa nje kwa matibabu.
Kauli ya Magufuli haikumaliza minong’ono kuhusu Kinana. Iliendelea mpaka Mei 2018, Magufuli alipotokeza na kueleza kuridhia Kinana kujiuzulu ukatibu mkuu. Akasema, Kinana aliomba zaidi ya mara mbili kuachia ngazi. Swali, baada ya kauli ya Magufuli, nani hatimaye alionekana mkweli?
Waliosema Kinana alijiuzulu na kujiweka kando na majukumu ya chama au Magufuli aliyekanusha na kusema alikuwa kwenye matibabu nje ya nchi?
Mwishoni mwa Februari hadi Machi 2021, taarifa zilianza kutolewa mitandaoni kuwa Rais Magufuli alikuwa na hali mbaya kiafya. Ikadaiwa kuwa alifikishwa hadi Kenya. Wapo waliodai alipelekwa India.
Kipindi hicho taarifa zinavumishwa, Taifa likageuka jukwaa la propaganda. Maudhui ni afya ya Magufuli. Waliomnenea ugonjwa wakanena. Waliopaza sauti kuwa alikuwa na siha njema, walisema. Wengine walihitimisha kuwa Magufuli alishaaga dunia.
Wakati mitandao ikipaza sauti kwa taarifa mbili (kifo na kuugua). Kulikuwa na jitihada nyingi za kukanusha uvumi huo. Kuna wakati zikawa zinasambazwa picha mnato na video za Magufuli za zamani ili kuonyesha alikuwa vizuri akichapa kazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Magufuli alikuwa Ikulu akichapa kazi. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, aliuambia umma kuwa yeye alikuwa akizungumza mara kwa mara na Magufuli, akashuhudia kuwa alikuwa mzima na salama.
Machi 14, 2021, Rais Samia, wakati huo akiwa Makamu wa Rais, alifanya ziara Tanga na akiwa Pangani, alisema, kusumbuliwa na mafua na homa ni kitu cha kawaida.
Ni kusema, baada ya mengi, Samia kwa mbali alikiri Magufuli kuumwa. Hata hivyo, namna ilivyoelezwa ni taarifa kuwa hakuwa kwenye hali ya hatari.
Machi 17, 2021, saa 5 usiku, Rais Samia alilihutubia Taifa, kulitaarufu kifo cha Magufuli. Kwamba kilitokea siku hiyo, Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.
Lilipokuja suala la Dk Mpango, Majaliwa alitaka watu wapuuze uzushi wa mitandaoni. Hapo hapo, kuna watu walikumbusha: “Hata Magufuli ilikuwa hivihivi. Majaliwa alikanusha hivihivi.” Nhat Hanh alisema, mawasiliano ni karma.