Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DPP alivyokutana na mfupa mgumu kesi ya nyara za Serikali za Sh323 milioni

Muktasari:

  • Jaji Stephen Magoiga alisema ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa na utata mkubwa kuhusu tarehe za kukamatwa kwa vielelezo na washtakiwa, jambo lililovunja mnyororo wa ushahidi na kuacha mashaka.



Morogoro. Jitihada za Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) za kutaka Mahakama iwatie hatiani washtakiwa wawili kwa kosa la kupatikana na meno ya tembo yenye thamani ya Sh323 milioni zimekwaa kisiki mara mbili kortini.

Hii ni baada ya Mahakama ya Wilaya ya Morogoro kuwaachia huru wasitakiwa wawili, Yahaya Juma na Masima Mlugu, katika kesi ya jinai namba 23754 ya mwaka 2025. DPP alikata rufaa, lakini Mahakama Kuu imeitupa rufaa hiyo.

Uamuzi wa kuitupa rufaa hiyo ya DPP ulitolewa Julai 17, 2026 na Jaji Stephen Magoiga wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Morogoro, aliyesema rufaa hiyo haikuwa na mashiko na hivyo ameubariki uamuzi wa kuwaachia huru.

Awali, wawili hao walishtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi la kupatikana na meno ya tembo yenye thamani ya Sh323 milioni, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kibali, kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa Agosti 18, 2024, katika eneo la SUA-Mashamba, Kata ya Mafiga, Manispaa ya Morogoro, walipatikana na meno matatu ya tembo na vipande 18 vya meno ya tembo vyenye thamani hiyo.

Ilidaiwa na upande huo wa Jamhuri kuwa Agosti 17, 2024, polisi kwa kushirikiana na maofisa wa wanyamapori, wakifanyia kazi taarifa (tip) waliyopewa na mtoa taarifa wao, waliwakamata washtakiwa hao wakiwa na nyara hizo za Serikali.

Shahidi namba 2 wa Jamhuri alieleza alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Fadhila Chacha, na alikuwa ofisa mkamataji akishirikiana na maofisa wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa).

Kwa mujibu wa shahidi huyo, alidai maofisa wa Tanapa walithibitisha eneo walikokuwapo washtakiwa, na walikwenda kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah na kufanikiwa kuwakamata washtakiwa katika barabara ya Iringa, eneo la SUA-Mashamba.

Upekuzi ulifanyika na kushuhudiwa na shahidi huru, ambaye ni shahidi namba 3, Seleman Butwa, ambapo vipande 18 vya meno ya tembo na meno matatu ya tembo vikiwa vimehifadhiwa katika mifuko ya sandarusi (sulphate bags) vilipatikana.


Utetezi wao ulivyokuwa

Mshtakiwa wa kwanza, Yahaya Juma, alijitetea kuwa alikamatwa akiwa katika nyumba ya kulala wageni ya Ngurasi Lodge iliyopo Mtaa wa Maelewano, karibu na Kituo cha Mabasi cha Mafiga, tofauti kabisa na eneo lililotajwa na Jamhuri.

Pia alikanusha kuhusika na vielelezo P2 na P3, ambavyo ni meno ya tembo.

Katika usikilizwaji huo, mshtakiwa huyo alipinga uhalali wa meno hayo kwa kuwasilisha video ya YouTube iliyorekodiwa na kurushwa na chombo cha habari kuhusu kukamatwa kwa pembe hizo, akidai video hiyo inaonesha hazikuwa na alama, ilhali vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani vina alama.

Mshtakiwa namba 2, Masima Mlugu, kwa upande wake, alidai kuwa alikuwa eneo la Kasanga akisubiri usafiri wa kwenda Mikumi ndipo akakamatwa na polisi.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ya Wilaya ya Morogoro iliwaachia huru baada ya DPP kushindwa kuthibitisha kosa bila kuacha mashaka.


Rufaa ya DPP ilivyokuwa

DPP hakuridhishwa na uamuzi huo na kukata rufaa, akiegemea sababu moja kwamba mahakama ya awali ilikosea kisheria na kiuhalisia kwa kuamua kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi bila kuacha mashaka yoyote.

Hata hivyo, kulingana na mwenendo wa rufaa hiyo, licha ya majaribio mara mbili ya kuwakabidhi wito wa mahakama na kutangazwa katika gazeti la Mwananchi mara tatu, wajibu rufaa, ambao ni waliokuwa washtakiwa, hawakupatikana.

Ruhusa ya kutangazwa kwa wito huo gazetini ilitolewa Mei 4, 2026 na Juni mosi, 2026, ambapo Juni 29, 2026, mahakama ililikubali ombi la DPP lililotolewa na Wakili wa Serikali, Paulina Massawe, la rufaa hiyo kusikilizwa bila wajibu rufaa kuwapo.

Wakili huyo, akiegemea shauri la Woolmington v DPP, alijenga hoja kuwa upande wa mashtaka, wakati wote, ulikuwa na jukumu la kuthibitisha hatia bila kuacha shaka yoyote na kwamba mahakama ya awali ilikosea kwa kuhitimisha vinginevyo.

Alieleza kuwa kupatikana na nyara hizo za Serikali kulithibitishwa na ushahidi wa mdomo wa shahidi namba 2 na 5 wa Jamhuri, ambao uliungwa mkono na shahidi huru (independent witness) namba 3, aliyeitwa kushuhudia upekuzi.

Wakili huyo alisema mnyororo wa kushughulikia vielelezo (chain of custody) haukukatika na kwamba utambuzi na uthamanishaji wa nyara hizo za Serikali ulithibitishwa na mtaalamu, shahidi namba 4, Joseph Bunango.

Pia alijenga hoja kuwa Jamhuri ilithibitisha kutokuwapo kwa kibali cha kuwa na nyara hizo. Aidha, alieleza kuwa ushahidi wa kutokuwapo eneo la tukio (alibi) hauaminiki, ulijikanganya na haukutolewa notisi kama sheria inavyotaka.


Hukumu ya Jaji

Jaji Magoiga katika hukumu yake alisema kuwa, kwa kuwa mahakama yake ndiyo ya kwanza ya rufaa, ina wajibu wa kuchambua na kupima ushahidi wa pande zote mbili uliotolewa katika mahakama ya chini na kufikia uamuzi wake huru.

 “Katika hoja kuu ya rufaa, mrufani (DPP) anaishutumu mahakama ya awali kwa kuamua kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote inayofaa,” alisema Jaji Magoiga katika hukumu yake, na kuongeza:

“Wakili wa Serikali aliyemwakilisha DPP kortini anaamini kuwa ushahidi uliowasilishwa ulikuwa wa kutosha kusababisha wajibu rufaa kutiwa hatiani.

“Nakubaliana na hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka kulingana na kesi za awali kwamba, katika kesi za jinai, jukumu la kuthibitisha hatia ni la upande wa mashtaka pekee. Pia nakubaliana na msimamo kwamba uthibitisho huo lazima uwe wa kiwango kisichoacha shaka yoyote ya msingi na si vinginevyo.

“Sitaki kuonekana nikipuuza hoja za rufaa zilizowasilishwa na upande wa mashtaka kwani, kwa kiasi fulani, wana hoja yenye mashiko. Hata hivyo, baada ya kutathmini ushahidi, nimebaini kuwepo kwa utata ambao hauwezi kupuuzwa.”

Jaji alisema shahidi namba 6 aliibua suala lenye utata ambalo ni la msingi kwa kesi hiyo, kisha akanukuu maneno aliyoyatamka wakati wa usikilizwaji wa kesi, kama yalivyoandikwa katika kumbukumbu za mahakama.

Ushahidi huo unasomeka: “Mnamo tarehe 18.07.2024 nilikuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro. Nilipokea jalada kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusu kosa la kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.”

Ushahidi huo unaendelea: “Nililetewa jalada pamoja na vielelezo tarehe 18.07.2024, na washtakiwa waliletwa Agosti 2024.”alisema wakati akijibu maswali ya dodoso na kuongeza: “Ni vielelezo vilivyokamatwa tarehe 18.07.2024.”

Jaji alisema ili kuelewa kikamilifu utata huo, ni vyema kufahamu kuwa mashahidi namba 2, 3 na 5 wa Jamhuri walieleza kuwa kukamatwa kulifanyika Agosti 17, 2024 na kwamba utwaaji wa mali (vielelezo vya meno ya tembo) ulifanyika siku hiyo hiyo.

Hata hivyo, alisema Wakili wa Serikali alidai huo ulikuwa utata mdogo tu.

Jaji Magoiga alichambua shauri la Dickson Shapwata na mwenzake dhidi ya DPP, ambalo Wakili wa Serikali aliliegemea akisema utata huo ni mdogo, lakini akaeleza kuwa shauri hilo linatofautiana na utata wa shauri lililokuwa mbele yake.

“Katika rufaa hii, utata uliokuwepo ulikuwa tofauti kabisa, kuna hitilafu ya muda inayoathiri uhalali wa mnyororo wa utunzaji wa pembe za ndovu.

“Tuseme kwamba pembe hizo kwa hakika zilipatikana tarehe 18.07.2024, kunakuwa na kipindi cha takriban mwezi mmoja ambacho hakijafafanuliwa hadi tarehe 17 Agosti, 2024,” alisema Jaji, na kuongeza:

“Kuna utata kuhusu iwapo pembe hizo zilipatikana huku watuhumiwa wakiwapo au la. Maneno ya shahidi namba 6 yalisema pembe hizo za ndovu zilinaswa tarehe 18.07.2024, na watuhumiwa walifikishwa kwake Agosti 2024.

 “Hii inakinzana kabisa na yale yaliyoelezwa na mashahidi namba 1, 3 na 5 wa upande wa mashtaka kwani, kwa mujibu wa maelezo yao, wajibu rufaa walikamatwa wakati mmoja na pembe hizo zikachukuliwa kutoka kwao.

“Sasa, ni lipi la kweli na lipi si la kweli, kwa kuwa ukweli hauwezi kuwa wa namna zote mbili kwa wakati mmoja?” alihoji Jaji Magoiga katika hukumu yake.

Jaji alisema utata huo haukurekebishwa kamwe na mawakili wa upande wa mashtaka wakati wa hatua ya kuwauliza tena maswali mashahidi wao, na rekodi inaonesha mawakili hao hawakuuliza tena maswali ya kurekebisha utata huo.

Kwa mujibu wa Jaji, dosari hizo zinakwenda hadi kwenye mzizi wa kesi, hasa ikizingatiwa kuwa shahidi huyo namba 6 ndiye aliyekuwa mpelelezi mkuu, na kwamba dosari hizo zinatosha kuitupa rufaa hiyo iliyowasilishwa na DPP.