Dk Mpango ashangaa ujenzi hospitali kusimamiwa na mhandisi wa kilimo

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Hospitali hiyo ambayo inajengwa Kata ya Mwanga imeshagharimu Sh2 bilioni zikiwa ni sehemu ya Sh7.4 bilioni zinazotarajiwa kutumika ujenzi utakapokamilika.

Mwanga. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ameeleza kutoridhishwa na ubora wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro na kuagiza Waziri wa nchi, ofisi ya Rais (Tamisemi), kutuma timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo, jana Machi 21, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Mwanga, katika stendi ya mabasi wilayani humo, mara baada ya kutoka  kutembelea na kukagua ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo pia ameonyesha kushangazwa na ujenzi kusimamiwa na mhandisi wa kilimo.

"Nimetoka kuangalia ujenzi wa hospitali, msema kweli mpenzi wa Mungu, sijafurahi kwa sababu tungeweza kufanya zaidi, Mkurugenzi urekebishe, kwanza hata hiyo barabara yenyewe ya kwenda hospitali haifanani na barabara ya kwenda hospitali ya wilaya.

"Tarura (Wakala wa Barabara wa Mijini na Vijijini) ipo, Mkuu wa Mkoa waambie waangalie hicho kipande cha kwenda hapo hospitali, kwa sababu hata ikiisha utapelekaje mgonjwa hospitali kwa namna hiyo?” alihoji.

Ameendelea kusisitiza kuwa hajafurahishwa na ubora wa ujenzi wa hospitali hiyo.

“Leo ndiyo nimesikia kwa mara ya kwanza mhandisi kilimo ndiye anasimamia majengo, hapana. Mkurugenzi umeshindwa hata kumwambia Mkuu wa Mkoa au wakurugenzi wenzio ukaazima hata mhandisi wa majengo wakakusaidia wakawa wanakuja kukagua? Milango ya ovyo," amesema.

Amesema tayari amemwagiza Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) kupeleka timu kwa ajili ya uchunguzi na kurekebisha,  ili hospitali hiyo iweze kukamilika na kuanza kazi na kwamba kwa watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua. 

"Kwa hiyo nimemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, ataleta timu hapa. Mama Samia (Rais) anatafuta hizi hela kwa jasho na damu, haiwezekani tumuangushe namna hii, kwa hiyo tutaleta timu hapa na hiyo timu ije mara moja, watafute ubora wa majengo na fedha iliyopotea na wanaohusika wachukuliwe hatua," amesema.  

Dk Mpango pia amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kusimamia ujenzi wa chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) katika Wilaya ya Mwanga ili kuhakikisha kinakamilika na vijana wanaingia kupata mafunzo.

"Nimeambiwa pia Veta ujenzi wake unasuasua, kwa hiyo mkalirekebishe, mkuu wa mkoa mkalisimamie hili, yale ambayo yanahitajika serikali kuu tuleteeni ili vijana hawa wa Mwanga waanze kusoma kwenye veta ya hapa," amesema Dk Mpango.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Zahara Msangi tayari Serikali imeshatoa Sh2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya na yameshajengwa majengo tisa.

"Serikali imeshatoa Sh2 bilioni na mpaka ikamilike hospitali hii inatarajiwa kutumia Sh7.4 bilioni, majengo tisa yamejengwa likowemo jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo dawa, jengo la mama na mtoto, wodi ya wagonjwa mchanganyiko, Mochwari (chumba cha kuhifadhia maiti), jengo la kufulia na kuchomea taka," amesema.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo amesema miongoni mwa miradi ya kimkakati katika wilaya hiyo ni hospitali ya wilaya, chuo cha Veta pamoja na stendi ya mabasi na kwamba miradi hiyo iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

Amesema pamoja na miradi mingi na mikubwa inayotekelezwa na Serikali, bado zipo changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa vyanzo vya mapato na kuomba mradi wa ujenzi wa stendi ambao tayari umefanyiwa upembuzi yakinifu, upewe fedha ili ujenzi uanze.

"Changamoto nyingine ni magugu katika ziwa Jipe, ziwa lile limefunikwa na magugu maji na Wilaya ya Mwanga hatufaidi kuvua samaki kwa sababu ya magugu hayo, naibu waziri alishakuja akaona, tunaomba mradi ule wa kuondoa magugu hayo uharakishwe ili wananchi waweze kuvua samaki na kuchochea ukuaji wa mapato," amesema.