Dk Mpango asisitiza maadili, nidhamu viongozi wa mikoa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka viongozi wa juu katika ngazi za mikoa kuhakikisha wanatafuta njia bora ya kuwashirikisha wengine ili msingi wa uongozi na utendaji uwe chachu zaidi kuleta maendeleo kwa wananchi.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango amewataka viongozi wa juu ngazi za mikoa kuzingatia maadili na nidhamu katika maeneo ya kazi ili kuwa picha nzuri na ya mfano kwa wengine.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 22, 2023 wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.

Amewataka viongozi wa mikoa kuongeza jitihada kuiwezesha sekta binafsi ili iweze kukua, kushamiri na kuzalisha ajira kwa kuweka vivutio na mazingira mazuri ya uwekezaji, akisisitiza sekta binafsi inapaswa kuwa mshirika muhimu katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa.

“Maudhui ya mada zitakazowasilishwa katika mafunzo haya yanalenga kuondoa matukio mbalimbali yanayotokana na mapungufu katika uongozi ikiwemo kutokuzingatia mipaka ya kiutendaji kati ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wenu.

“Hususan katika matumizi ya fedha pamoja na kushindwa kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali hususan katika zama hizi za utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano,” amesema Dk Mpango.

Makamu huyo wa Rais pia amewataka viongozi hao kuzingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira hususani kutunza vyanzo vya maji, kufuatilia fursa mbalimbali zitokanazo na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na biashara ya kaboni na uchumi wa buluu.

Amewaagiza kuhakikisha kunakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepuka migogoro mbalimbali ndani ya jamii na kuzingatia changamoto zozote zinazojitokeza katika jamii zinashughulikiwa mapema na kwa ukamilifu.

“Dhima ya mafunzo haya ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020, ambayo inaelekeza umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika hali iliyo shirikishi na yenye ubora,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Angellah Kairuki amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea viongozi hao uwezo wa kuongoza na kusimamia wananchi, fedha na rasilimali zingine muhimu za taifa.

“Mafunzo haya yatawawezesha viongozi kuwa na maamuzi ya kimkakati pamoja na kuwa na uwezo katika masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa majukumu yenu,” amesema.

Kairuki amesema katika siku sita za mafunzo jumla ya mada 20 zinatarajiwa kuwasilishwa kwa viongozi hao ambazo zitajikita katika masuala ya uongozi, usimamizi rasilimali, miongozo na taratibu mbalimbali za utendaji kazi serikalini, usimamizi miradi na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukuza uchumi.