Dk Mpango ataka watumishi fedha kujihadhari na corona

Dk Mpango ataka watumishi fedha kujihadhari na corona

Muktasari:

  • Ni wito wa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, kwa watumishi wa wizara yake

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango, amewataka watumishi wa wizara hiyo kuchukua tahadhari zote kuhusu ugonjwa wa corona, licha ya kukiri kuwa Tanzania haina maambukizi ya virusi hivyo kwa sasa.

Dk Mpango alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mkutano huo ulifanyika jana katika ukumbi wa Kambarage uliopo jijini Dodoma.

Waziri Mpango alisema ugonjwa huo haupo nchini, lakini umeendelea kuitikisa dunia na kuyumbisha uchumi wa nchi nyingi.

“Tumshukuru Mungu ugonjwa huu umetupisha mbali hapa nchini kwetu, lakini niwasihi watumishi tuendelee kuchukua tahadhari zote kama tunavyoelekezwa na wataalamu wetu wa Wizara ya afya,” alisema.

Awafunda wafanyakazi

Aidha, Dk Mpango aliwagiza viongozi wa baraza hilo kufikisha ujumbe kwa wanaowaongoza, watende kazi kwa kufuata miongozo na kutotoa siri za Serikali.

Alisema watashughulika na watendaji watakaobainika kuvujisha siri za Serikali.

Katika hatua nyingine Dk Mpango aliwaagiza watumishi katika wizara hiyo kutobweteka kutokana na Tanzania kuingia katika uchumi wa kati.

Alisema wanapaswa kutambua kuwa bado wana safari ndefu ya kuipeleka nchi katika mafanikio zaidi.

‘‘ Hakuna maana kwa wizara kuwa na msururu wa wafanyakazi ambao hawatimizi wajibu wao bali kila mmoja ajione kuwa na thamani mahali pake na watenge muda wa kusikiliza matatizo ya walio chini yao,’’ alisema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, alitaja lengo la mkutano huo ni kuchagua viongozi na kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi.

James alisema maboresho ya mazingira ya watumishi yataendana na kuboresha mazingira ya kazi ili kufanya watu wawe na afya njema na kuendelea kuchapa kazi inavyotakiwa.

Akitoa neno la shukrani, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mary Maganga aliahidi kuwa maagizo ya Waziri yatazingatiwa na kwamba watayashusha kwa watendaji wa ngazi ya chini ili utekelezaji uanze mara moja.