Dk Mwigulu afunguka kuhusu deni la Taifa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba

Muktasari:

  • Kwa sasa mjadala mzito ni deni la Taifa, ambapo Dk Mwigulu amelieleza Bunge kuwa fedha hizo zilizokopwa zimetumika kujenga miradi mikubwa hasa uboreshaji wa miundombinu.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka wanaohoji kuhusiana na deni la Taifa kutofanya tathimini kama wamebambikwa bali wafanye hivyo huku wakiangalia miradi iliyofanyika kutokana na mikopo hiyo.

Dk Mwigulu aliyasema hayo bungeni jana wakati akihitimisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema wanayo orodha ya ndefu ya miradi ambayo imefanyika kwa kutumia fedha hizo za mikopo nchini.

“Niwaombe Watanzania hasa sisi ambao ni viongozi tusianzie mbali sana tuanzie wakati deni la Taifa likiwa kiwango cha Sh10 trilioni.

Halafu tuanze kuangalia katika mwaka 1995 deni lilikuwaje halafu tuangalie pia na miradi ambayo ililetwa na fedha zilizokopwa,” amesema.

Amewataka kuangalia pia ni kipi kilitakiwa kifanyike wakati deni linalotajwa lilikuwa dogo.

Dk Mwigulu amesema wakati huo hakukuwa na mikoa ambayo iliunganishwa na barabara za lami jambo ambalo liliwafanya watu kusafiri kwa muda mrefu.

“Analysis (tathimini) iliyofanyika je tuchukue makusanyo ya fedha tujenge barabara zetu? Tufungue uchumi na tukishafungua uchumi utuletee fedha.

…Je tuendelee na hali kama hii halafu na deni letu liwe dogo au tuchukue fedha tutengeneze miundombinu tufungue nchi yetu halafu miundombinu hiyo ituletee fedha tulipe deni,” amehoji.

Dk Mwigulu amesema uamuzi huo ulipofanyika hivi sasa karibu kila eneo lina umeme wakati awali eneo kubwa lilikuwa giza na hali ilikuwa hivyo hivyo katika sekta nyingine ikiwemo ya afya.

Amesema ipo orodha ya karibu miradi 1,000 ambayo imejengwa kwa kutumia fedha hizo  ambayo isingeweza kufanyika katika kipindi hicho kama Serikali isingekopa.

“Tusifanye tathimini kama tumebambikwa tufanye tathimini ya deni huku tukifanya tathimini ya miradi ambayo imefanywa kutokana na deni hilo,” amesema.

Amesema kuna wengine wenye siasa nyepesi wanasema Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imeingia madarakani miezi sita iliyopita imeshakopa fedha nyingi.

Amewataka kumuogopa Mungu kwa sababu mkopo wa kwanza iliyokopa ni Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF).

Hata hivyo, amesema kwa mazungumzo yanayoendelea kuhusu mkopo huo utakuwa wa masharti nafuu kuliko mikopo yote ambayo imeshakopwa na Serikali.

Amesema Serikali haijawahi kukopa kwa ajili ya kulipa mishahara ama kuweka mafuta kwenye magari ya umma bali ni kwa ajili ya kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Amesema Serikali iko katika mwelekeo sahihi licha ya wengine kusema kuwa wamechukua katika akiba iliyowekwa.

Amesema mwaka 2015 akiba (reserve) zilikuwa dola za Marekani bilioni 4.3 wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, lakini wakati inaondoka madarakani akiba ilikuwa Dola za Marekani bilioni 5.03.

Amesema kutoka Machi, mwaka huu wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia ilipandisha kutoka dola za Marekani bilioni 5.03 hadi bilioni 6.4, fedha ambazo zinazotosha kwa uagizaji wa miezi sita.

“Hatupaswi kuangalia mambo ya fedha, tunatakiwa kujua zimetumikaje. Sio kila siku watu wanaangalia namba tu wengine wanawatisha wananchi wetu tuangalie tulipowekeza,” ameongeza Dk Mwigulu.

Hata hivyo, amesema kuwa anakubaliana na mapendekezo ya Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kuwa ya kufanya tahimini ya deni hilo.

Mapema wiki hii Nape akichangia mapendekezo ya mpango huo alipendekeza ukaguzi wa kina ufanyike kwenye akaunti ya deni la Taifa ili kufahamu fedha zilizokopwa zimetumika kwenye miradi ipi.

Amesema Serikali inapaswa kueleza wananchi kuhusu fedha zilizokopwa zilipelekwa wapi, thamani yake na uhalisia wa miradi inayotekelezwa kutokana na fedha hizo.

“Mwenyekiti iwekwe wazi kwenye akaunti ya deni la Taifa, tujue kilikopwa nini, kimeenda wapi, thamani yake nini, uhalisia wa miradi inayotekelezwa na thamani tuliyoambiwa. Iwekwe mezani ili tuige mfano mzuri uliofanywa na Rais Samia (Suluhu Hassan) wa kuweka mezani Sh1.3 trilioni na kila mmoja anajua,” alisema Nape.