Dk Mwigulu aibua upya kauli tata za viongozi

Dk Mwigulu aibua upya kauli tata za viongozi

Muktasari:

  • Kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ya kuwataka Watanzania wasioridhishwa na ongezeko la tozo za miamala ya simu na kodi za mafuta kwenda nchini Burundi kutafuta unafuu, imeibua mjadala mzito miongoni mwa wananchi, huku pia ikikumbusha kauli tata zilizowahi kutolewa na viongozi wa Serikali.

Dar es Salaam. Kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ya kuwataka Watanzania wasioridhishwa na ongezeko la tozo za miamala ya simu na kodi za mafuta kwenda nchini Burundi kutafuta unafuu, imeibua mjadala mzito miongoni mwa wananchi, huku pia ikikumbusha kauli tata zilizowahi kutolewa na viongozi wa Serikali.

Dk Mwigulu alitoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV Julai 20, mwaka huu, ambapo alisema kwa sasa sheria ya tozo ya miamala imeshapitishwa hivyo hawezi kuibadilisha.

“Yaani hata hivi nafafanua tu ili kutoa uelewa, lakini hata mimi niliyeweka mapendekezo siwezi kufuta uamuzi wa Bunge, hiyo ni sheria. Kwa hiyo yule anayedhani anaweza kuhamia Burundi kuliko nafuu na aende ahamie huko Burundi, lakini hii ni sheria inakwenda kutekelezwa,” alisema Waziri Mwigulu.

Kauli hiyo imezua mjadala mitandaoni, baadhi ya watu wakidai kuwa ni ya kukejeli Watanzania wanaoumizwa na makato mapya ya miamala ya simu.

Huku akiweka msisitizo, Dk Mwigulu aliendelea kusema: “Uchumi wa Tanzania wala hauathiriki kwa jambo hilo. Hiki naongea daktari wa uchumi hupaswi kunitilia shaka, hauathiriki na tunakokwenda tutakuwa imara zaidi kwa sababu tunakwenda kufungua bidhaa zitoke katika ziada ziende kwenye upungufu, wala sina mashaka na jambo hilo.”

Licha ya kauli hiyo ya Dk Mwigulu, Rais Samia Suluhu Hassan amemwagiza Waziri Mkuu kukaa na mawaziri wa Fedha na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ndugulile kufanyia kazi malalamiko ya wananchi kuhusu tozo hizo. Tayari kikao hicho kimefanyika na kamati imeundwa kufanya tathmini.

Hata hivyo, kauli ya Dk Mwigulu imeamsha hisia na kumbukumbu ya kauli tata zilizowahi kutolewa na viongozi wa Serikali zilizopita.

Kauli nyingine ambazo zimenasa kwenye vichwa vya Watanzania ni iliyowahi kutolewa na Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba alipokuwa akitetea ununuzi wa ndege ya Rais (Benjamin Mkapa wakati huo), ambapo alisema Watanzania tuko tayari kula nyasi ilimradi ndege ya Rais inunuliwe.

Pia, miongoni mwa kauli hizo ipo aliyowahi kutolewa na Hayati Rais John Magufuli wakati akiwa Waziri kabla ya baadaye kuwa Rais.

Januari 2012 akiwa Waziri wa Ujenzi, Hayati Magufuli aliwataka wananchi wa Kigamboni waliokuwa wakilalamikia ongezeko la bei ya kupanda kivuko kutoka Sh100 hadi Sh200 wapige mbizi.

Viwango vipya vya nauli vilipandishwa tangu Desemba 29, 2011 kwa asilimia 100 na vilianza kutumika Januari Mosi, 2012.

Baada ya malalamiko hayo, Magufuli alifanya ziara eneo la Kivukoni, Dar es Salaam na kusisitiza nauli hizo lazima zilipwe na mtu asiyetaka ni vyema akapiga mbizi kwa kuogelea kutoka Kigamboni hadi ng’ambo ya pili au apite Kongowe kuingia katikati ya jiji.


Tetemeko la Kagera

Alipokuwa Rais, Hayati Magufuli pia alitoa kauli tata zikiwemo za wakati wa tetemeko la Kagera mwaka 2017, ambapo aliwaeleza wananchi walioathiriwa na tetemeko hilo kuwa Serikali haikulileta na hivyo, haitawapa msaada wa chakula.

“Pasitokee mtu wa kuwadanganya kuwaambia kuwa kuna vitu vitaletwa bure, pasitokee mtu wa kuwadanganya kwamba Serikali itagawa chakula. Huwezi ukagawa chakula ardhi ya kijani hivi.

“Kwa hiyo Mkuu wa Wilaya nataka nikueleze hapa, sitaleta chakula, ukishindwa wewe leta tu kwamba useme nimeshindwa kuongoza wilaya hii. Hakuna chakula cha Serikali, mvua zinanyesha watu tufanye kazi,” alisema Hayati Magufuli.

Mbali na chakula, Magufuli pia alisema Serikali haitawajengea nyumba wale waliobomokewa nyumba zao kutokana na janga hilo.

“Haiwezekani Serikali ikajenga nyumba zote za wananchi katika mkoa wa Kagera, haipo Serikali ya namna hiyo duniani.”

Alitoa mfano wa Italia akisema lilipotokea tetemeko kwao nao hawakujengewa nyumba.

“Najua wanasiasa wengine watakuja hapa watasema Serikali iwajengee nyumba, waambieni wanasiasa hao wawajengee wenyewe. Mimi ninawaeleza ukweli mlinichagua niseme ukweli.

“Jukumu la Serikali ni kurudisha miundombinu ya Serikali siyo kujenga nyumba ya wananchi, kwa sababu tetemeko hili limeiumiza Serikali na imewaumiza wananchi. Kwa hiyo kila mmoja abebe msalaba wake.

“Wapo wengine nyumba zao zilibomoka kidogo wakaambiwa Serikali itakuja kujenga majengo yao, wakazibomoa zote, mwafaa!”


Dk Mwakyembe na ‘degree nne’

Kauli nyingine iliyochukuliwa kuwa ya kejeli ni iliyotolewa na waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Novemba 2019 alipokuwa akieleza kuhusu wimbo wa Romwa uliotolewa na msanii Roma Mkatoliki.

“Sanaa ni pamoja na kuonya na kukemea, lakini mwenyewe unayeonya na kukemea, uwe na maarifa na weledi na elimu ya kukemea. Siyo tu umetoka na darasa lako la pili kule unanionya mimi nina degree (shahada) nne, nitaona kama unafanya mzaha tu.

“Wewe utanionya nini kwa mfano wewe darasa la saba, mimi hapa daktari wa falsafa, mwalimu wa vyuo vikuu mbalimbali, utanionya nini? Sana sana unaweza kunionya ni kuhusu mfuko wako wa suruali kama una hela au hauna, huwezi kunionya chochote,” alisema Dk Mwakyembe.

Hivi karibuni Waziri Mkuu wa zamani, Cleopa Msuya amesema kati ya mambo anayoyakumbuka katika utumishi wake Serikalini ni pale alipowaambia Watanzania kuwa kila mtu atabeba msalaba wake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam, Msuya, aliyekuwa Waziri Mkuu kati ya mwaka 1980 hadi 1983 na baadaye mwaka 1994 hadi 1995 alisema kauli hiyo iliyeyuka yenyewe.

“Moja ya kauli ambayo nilikuwa quoted out of context (nje ya muktadha) na ikajirekebisha yenyewe, ilikuwa ni wakati wa bajeti. Tukawa tunajadili hapo Karimjee (Dar es Salaam). Sasa wabunge wengi wakawa wanasema ooh mimi nimeoa mke, mwingine nimeoa wake wawili, sasa itakuwaje?” amesema Msuya alipoulizwa swali kuhusu kauli zake tata.

“Ikafika mahali mimi nikasema, kila mtu atabeba msalaba wake, kwa sababu haiwezekani mtu ukaamua kuoa wake wawili, sasa Serikali inataka kujenga shule watoto wasome halafu wewe unakuja unasema umeoa wake wawili? Kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe,” amesisitiza.

Mbali na kauli hizo, pia zipo nyingine zilizowahi kutolewa na baadhi ya viongozi, ikiwemo ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alipomtukana dereva wa bajaji akimtaka kutuliza makalio. Japo Kasesela alijitokeza hadharani kuomba radhi, lakini kauli hiyo iliibua utata miongoni mwa wananchi. Siku chache baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya na Kasesela hakuwemo.