Dk Mwigulu awaagiza makandarasi kurejea kwenye miradi ya barabara
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Sokoine, wilayani Serengeti, mkoani Mara, leo Jumatano Julai 1, 2026.
Muktasari:
- Ndani ya Mkoa wa Mara miradi ya barabara iliyosimama utekelezaji wake kutokana na ukosefu wa fedha ni pamoja na Tarime- Mugumu, Sanzate - Mugumu, Musoma - Busekekela na Mika -Kirongwe
Serengeti. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza Wizara ya Ujenzi kuwaelekeza makandarasi waliositisha utekelezaji wa miradi ya barabara kutokana na ukosefu wa fedha kurejea mara moja kwenye maeneo yao ya kazi ili miradi hiyo ianze kutekelezwa.
Dk Mwigulu ametoa agizo hilo leo Julai Mosi, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Serengeti, mkoani Mara, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Amesema uamuzi wa Serikali wa kusitisha kwa muda utoaji wa fedha kwa baadhi ya miradi ya barabara ulilenga kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo wa kufua umeme wa Julius Nyerere na ujenzi wa Daraja la Magufuli.
“Hatukufanya hivyo kwa sababu tulipuuzia umuhimu wa barabara hizi, bali tulifanya uamuzi wa busara ili kukamilisha miradi ya kimkakati ambayo ilikuwa muhimu kwa maendeleo ya Taifa. Mradi wa Julius Nyerere ulikuwa unakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo vikwazo kutoka nje ya nchi,” amesema.
Amesema Serikali ililazimika kuweka kipaumbele katika kuongeza uzalishaji wa umeme baada ya kufanikisha kusambaza umeme katika maeneo mengi nchini, hali iliyosababisha mahitaji kuongezeka kuliko uwezo wa uzalishaji.
“Baada ya kufikisha umeme katika karibu vijiji vyote nchini, mahitaji yaliongezeka sana wakati uzalishaji ulikuwa mdogo. Hali hiyo ilisababisha mgao wa umeme ulioathiri shughuli za uchumi na uzalishaji, hivyo ilikuwa lazima kukamilisha mradi wa Julius Nyerere,” amesema.
Dk Mwigulu amesema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, Serikali ilikuwa ikitumia zaidi ya Sh300 bilioni kila mwezi, hali iliyosababisha miradi mingine, ikiwemo ya barabara katika Mkoa wa Mara, kuchelewa kupata fedha.
Amesema sasa Serikali imeweka utaratibu mpya wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kasi, ambapo mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya miradi ya barabara yataelekezwa moja kwa moja katika Mfuko wa Barabara badala ya kupelekwa kwanza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Amefafanua barabara zitakazoanza kutekelezwa ni pamoja na Tarime – Mugumu, Sanzate – Mugumu na nyingine zilizokuwa zimesimama, huku utekelezaji ukitarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2026/27.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Mara haukuwa pekee ulioathiriwa na uamuzi huo, bali miradi ya barabara katika mikoa mingine pia ilisimama kutokana na kipaumbele kilichotolewa kwa miradi ya kimkakati.
Katika mkutano huo, Dk Mwigulu pia amezitaka mamlaka mbalimbali kuacha tabia ya kuwanyang'anya wafanyabiashara wadogo vitendea kazi vyao kwa madai ya kukiuka taratibu.
Amesema badala ya kuwachukulia hatua zinazoharibu shughuli zao za kiuchumi, wanaobainika kukiuka sheria wanapaswa kutozwa faini kwa mujibu wa sheria.
“Tabia ya kuwanyang'anya wafanyabiashara pikipiki, baiskeli, mikokoteni au vifaa vya wamachinga na mama lishe ikome. Hakuna sababu ya kuharibu mtaji wa mtu wakati hicho ndicho chanzo chake cha kipato. Viongozi wanapaswa kutumia busara,” amesema.
Kuhusu watumishi wa umma wasiozingatia maadili ya kazi, Mwigulu amesema Serikali haitawavumilia, akieleza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Tayari nimeagiza kuwa mtumishi atakayebainika kwenda kinyume na maadili hatapelekwa kituo kingine cha kazi, bali atachukuliwa hatua katika kituo chake, ikiwemo kufukuzwa kazi pale inapobidi,” amesema.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mpango wa kupima vijiji vyote 78 vya Wilaya ya Serengeti ili kupunguza migogoro ya ardhi.
Amesema zoezi hilo litatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano na litasaidia kumaliza migogoro ya mipaka kati ya vijiji, kata na taasisi mbalimbali.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho, amesema kukamilika kwa miradi ya barabara wilayani Serengeti kutaimarisha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kuunganisha wilaya hiyo na maeneo mengine ya Mkoa wa Mara na nchi kwa ujumla.
Pia amewataka wananchi kuendelea kulinda amani, akisisitiza kuwa amani haina dini, kabila wala chama cha siasa, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda.
Awali, Dk Mwigulu alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kusema Serikali imejenga majengo 150 ya utawala katika halmashauri mbalimbali nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mara, Jeje Jeje, amesema ujenzi huo unagharimu zaidi ya Sh4.5 bilioni, umefikia asilimia 42 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Aprili 2028.