Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwinyi azindua bohari ya gesi Zanzibar

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi (wa kwanza kulia) akifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa bohari ya gesi Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja

Muktasari:

  • Asema itakuwa chachu ya utekelezaji wa mpango mkuu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024-2034.

Unguja. Wakati Zanzibar ikizindua bohari ya kwanza ya kupokea na kusambaza gesi, Rais Hussein Mwinyi amewataka wananchi kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni.

 Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 27, 2024 alipozundua bohari hiyo eneo la Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja chini ya Kampuni ya Oryx Gas Zanzibar Ltd.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza athari za mazingira na kujiepusha na athari za kiafya zinazotokana na hewa sumu.

“Niombe kampuni ya gesi kutafuta namna ya kuwezesha kupatikana gesi kwa bei nafuu, ili wananchi wamudu bei ya bidhaa hii kwa matumizi ya kupikia,” amesema.

Pia amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kuilinda miundombinu hiyo itakayowekwa kwa kutokufanya shughuli yoyote isiyokubalika ambayo itasababisha madhara ya bandari na vilivyomo.

Amesema kuanzishwa kwa hifadhi ya gesi Zanzibar itakuwa chachu ya utekelezaji wa mpango mkuu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024-2034 ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ukilenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema uwekezaji wa Kampuni ya Oryx Gas Zanzibar Ltd ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano kwa kujenga matangi mawili yenye ujazo wa tani 1,388 sawa na kilo 1,388,000 za gesi.

“Hivyo basi, ningependa niwasihi kampuni nyingine za gesi kuharakisha ujenzi wa miundombinu katika eneo hili la Mangapwani tuzidi kupiga hatua katika kuimarisha sekta ya gesi nchini,” amesema.

Serikali imetenga eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha usalama wa ugavi wa bidhaa za mafuta na gesi kwa kupokea meli kubwa zenye bidhaa hizo ambazo zitakidhi mahitaji ya nchi kwa zaidi ya miezi mitatu bila ya matatizo yoyote.

Amesema kwa muda mrefu, shughuli za uingizaji wa gesi zimekuwa zikifanyika kupitia Bandari ya Malindi ambako kampuni nne za gesi za Oryx Gas Zanzibar Limited, Lake Gas Tanzania Limited, Taifa Gas Tanzania Limited na O – Gas, zinafanya shughuli hiyo.

Kutokana na ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi na kijamii, eneo hilo kwa sasa limeonekana halitoshi kuendelea kutumika kwa shughuli za gesi ikizingatiwa mazingira ya kiusalama kwa bidhaa husika.

Amesema Zanzibar ni nchi ya visiwa, kama zilivyo nyingine za aina hiyo,  shughuli za usafirishaji wa bidhaa kuingia na kutoka zinategemea zaidi usafiri wa baharini.

“Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na bandari za kupokea meli za aina mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema.

Mwenyekiti wa Kampuni za Vigor, Tawfic Turky amesema kazi hiyo haikuwa rahisi, lakini kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali imewasaidia kufikia hatua hiyo.

“Kwa sasa tumekamata soko la Zanzibar kwa asilimia 30, lakini tunataka kwenda mbali zaidi,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Mafuta (Zura), Omar Ali Yusuf amesema: “Meli zilikuwa zinashusha gesi inapakiwa kwenye meli nyingine inakwenda Tanzania Bara, kisha inarudishwa tena lakini sasa gesi inashushwa moja kwa moja Zanzibar,” amesema.