Dk Nchimbi atoa maelekezo mkoani kwa Chongolo

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo mara baada ya kuwasili Tunduma kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara.

Muktasari:

  • CCM imetoa maelekezo kwa viongozi wa Mkoa wa Songwe ikisisitiza haki kutendeka katika maeneo yenye migogoro ya ardhi na katika ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara.

Songwe. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa maelekezo matatu kwa Serikali ya Mkoa wa Songwe ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoani humo kuzingatia haki katika ukusanyaji wa kodi na sio kuwaonea watu.

Mengine ni kusimamia vizuri Sh100 bilioni zitakazotolewa na Serikali kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za maji katika mji wa Tunduma, na watumishi kutenda katika maeneo yenye migogoro ya ardhi.

Maelekezo hayo yametolewa leo Jumatatu, Aprili 15, 2024 na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Sekondari Tunduma mkoani humo, katika mwendelezo wa ziara yake akiambatana na wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho.

"Watu wasionewe walipe kodi kwa kiwango wanachostahili, sio kulipishwa zaidi, Rais Samia Suluhu Hassan aliposema haya watu walibeza kuwa ni maneno ya kisiasa nasisitiza, maelezo ya Rais ni ya mkuu wa nchi watu wasionewe watendewe haki," amesema Dk Nchimbi.

Jumatano ya Aprili 10, 2024 akiwa katika Baraza la Idd El – Fitri, Rais Samia alisema msimamo wa Serikali ni kutokubaliana na ukusanyaji wa kodi za dhuluma kwa wananchi huku akiwapongeza wafanyabiashara wanaotoa risiti za kielektroniki.

Hata hivyo, Rais Samia alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa hawatoi risiti wanapouza bidhaa za au wakitoa zina mapungufu.

Kuhusu suala ardhi, Dk Nchimbi amesema, "natoa maelekezo kwa Serikali ya Mkoa wa Songwe yale maeneo ambayo Serikali inatakiwa kusimamia haki za raia, naombeni sana watumishi wa halmashauri hakikisheni mnazingatia haki za wananchi.”

"Msiruhusu wananchi wadhulumiwe kwa namna yoyote wala kunyanyaswa naomba sana sana...," amesema Dk Nchimbi.

Katibu mkuu huyo, amewaambia watumishi wa Songwe fedha za mradi wa zikifika mkoani zitumike vizuri.

"Nitamhemea Waziri wa Maji, Jumaa Aweso shingoni kuhakikisha fedha za maji zinafika kwa wakati na zikifika zisimamiwe ili zifanye kazi vizuri," amesema Dk Nchimbi.

Awali, akimkaribisha katika mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo alimweleza Dk Nchimbi katika kipindi cha miaka mitatu Serikali imepeleka fedha nyingi mkoani humo kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za jamii, ikiwemo shule na hospitali.

"Ndugu Katibu Mkuu wa  CCM (Dk Nchimbi), ndani ya muda mfupi Serikali imeshusha Sh608 bilioni mkoani hapa kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za wananchi," amesema Chongolo aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Naye Katibu wa Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu amewataka wananchi wa mkoa huo  kujitokeza kwa wingi katika uandikishaji wa daftari la wapiga kura pindi mchakato huo utakapoanza ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu.