Siri uteuzi wa timu Nchimbi CCM

Dar es Salaam. Sasa ni rasmi kwamba timu atakayofanya nayo kazi kwenye sekretarieti, Katibu mpya wa Chama cha Mapinduzi, Dk Emmanuel Nchimbi imekamilika.

Hii ni baada ya mabadiliko yaliyofanywa jana na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), yakiwaondoa makada waliokuwa kwenye sekretarieti iliyokuwa chini ya Daniel Chongolo, aliyejiuzulu Novemba mwaka jana.

Kama ambavyo Nchimbi aliingia ikaelezwa na mkakati wa kujipanga na uchaguzi mkuu, vivyo hivyo, hata kwa timu yake hiyo iliyotangazwa jana imeelezwa hivyo na wasomi wa masuala ya siasa, kuwa inalenga uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mambo mengine yanayotajwa kuchagiza mabadiliko hayo kwa mujibu wa wanazuoni hao ni kukisafisha chama hicho, huku wengine wakisema hawatarajii mambo mapya katika safu hiyo mpya iliyopangwa.

Wasomi hao wamesisitiza kuwa hatua hiyo imelenga kuhakikisha sekretarieti chini ya Balozi Nchimbi inakuwa na safu inayoendana na yenye muunganiko utakaochagiza ufanisi katika utendaji wa chama hicho.

Mitazamo hiyo ya wasomi ilitolewa jana, muda mfupi baada ya NEC ya CCM iliyoketi jana Ikulu jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuwateua makada wanne kuziba nafasi nne za wajumbe wa sekretarieti zilizokuwa wazi tangu Machi 31, mwaka huu.

Nafasi iliyosalia kwenye wajumbe hao ni ya katibu mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), iliyobaki wazi jana baada ya Jokate Mwegelo aliyekuwa anaishikilia kuhamishiwa Umoja wa Vijana (UVCCM).

Jokate amepokea kijiti kutoka kwa Fakii Lulandala, aliyeteuliwa mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.


Timu yenyewe

Katika uteuzi huo walioingia ni Amos Makalla anayeshika nafasi ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, akirithi mikoba ya Paul Makonda aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Mwingine ni John Mongella anayekuwa Naibu Katibu Mkuu - Bara kurithi mikoba ya Anamringi Macha aliyepelekwa Shinyanga kuwa mkuu wa mkoa.

Safu hiyo inakamilishwa na Ally Hapi, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, akimrithi Gilbert Kalima aliyeteuliwa mkuu wa Wilaya ya Mkinga.

Uteuzi wa makada hao wanne, ulidokezwa kwa nyakati tofauti na gazeti hili kupitia vyanzo vyake ndani ya chama tangu Rais Samia alipofanya mabadiliko ya viongozi mbalimbali ambao wanatarajiwa kuapishwa leo, Ikulu ya Dar es Salaam.

Uteuzi huo umefanyika zikiwa zimepita siku 79 tangu NEC ilipkutana Januari 15 mwaka huu, kumteua Dk Nchimbi kuwa katibu mkuu kuchukua mikoba ya Chongolo, ambaye sasa ni mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Usafi wa chama

Kwa mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya siasa, Nassor Seif, mabadiliko ya viongozi wa sekretarieri, pamoja na mambo mengine umelenga kukiacha chama hicho “katika usafi uliotukuka.”

Alisema baadhi ya waliokuwepo kabla ya mabadiliko hayo, walihusishwa na tuhuma mbalimbali na wengi waliwalalamikia, pengine ndiyo sababu CCM imeamua kuwabadili.

“Ndani ya CCM kuna mikakati, viongozi waliokuwepo katika nafasi hizo baadhi yao walilalamikiwa na wananchi na vyama vya upinzani, kwa chama makini hakiwezi kuwaacha watu wa namna hiyo, ni vema kiwaondoe ili kujisafisha,” alisema Seif bila kuwataja.

Alisema hakutakuwa na athari hasi juu ya uamuzi huo, akisisitiza walioteuliwa ni wazoefu na wanakijua chama hicho vema.


Mkakati wa uchaguzi

Akichambua mabadiliko hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi alisema msingi wa mabadiliko hayo ni maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Kwa namna yoyote kilichofanyika ni kujiandaa na uchaguzi huu wa mwaka huu na ule wa mwakani, ndiyo maana wameamua kufanya mabadiliko,” alisema.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo alieleza kushangazwa na hatua ya mabadiliko katika nafasi ya mwenezi wa chama hicho, akisema aliyekuwepo (Makonda), alifaa zaidi.

“Kwa mtazamo wangu, ile nafasi (Makonda) aliiweza sana japokuwa kuna wakati alikuwa anazungumza vitu vinavyowapa wasiwasi, lakini aliwajengea imani sana wananchi, sasa kina Makala sijui kama wanayaweza mambo hayo,” alisema.

Alieleza mabadiliko hayo ni kama yanakwenda kuipoozesha CCM, kutoka kwenye siasa za amshaamsha zilizokuwa zikifanywa na mwenezi aliyepita.

“Japokuwa nguvu ya upinzani ni kama imefubaa, lakini huwezi jua pengine karibu na uchaguzi wakawa na amshaamsha zile za maneno makali, huenda chama kikajikuta kinapata shida,” alisema.


Ni walewale

Mabadiliko pia yanatajwa na Dk George Kahangwa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama hayana jipya na kuwa walioteuliwa ni walewale ambao wameonekana serikalini.

“Ni watu walewale wanabadilishwa, hatupati jambo jipya isipokuwa kubadilisha nafasi na inatupa picha Rais ndiye mwenyekiti wa chama, anatoa watu ndani ya Serikali na kuwapeleka kwenye chama na anatoa kwenye chama na kuwpeleka serikalini.”

Dk Kahangwa, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) alisema: “Yote yanayofanyika ni maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.”

Mhadhiri huyo alisema ni vigumu kuutenganisha uteuzi huo na Katibu Mkuu wa chama Dk Emmanuel Nchimbi “kwa sababu hadi Rais au mwenyekiti anateua kuna watu wanaomwandalia, sasa upande wa chama katibu mkuu ana nafasi kubwa kwenye hili, kuwa huyu anafaa hapa na huyu hapa.”

Alisema Dk Nchimbi amewahi kufanya kazi kwa karibu ndani ya chama na Makalla na Mongella, hivyo kuna uwezekano mkubwa safu hiyo ni maandalizi ya chaguzi hijazo.


Wasifu Makala

Makalla alizaliwa Septemba 16, mwaka 1971 na kupata elimu ya Sekondari katika shule ya Galanos mkoani Tanga. Mwanasiasa huyo ni msomi wa shahada ya uzamili katika biashara, aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.

Wasifu wake wa uongozi unaanzia ngazi ya UVCCM, aliwahi kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo na baadaye alishika nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM.

Nje ya CCM amewahi kuwa Mbunge wa Mvomero mwaka 2010 na mwaka 2013 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na baadaye Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji.

Kadhalika, Makalla amewahi kutumikia mikoa mbalimbali kwa nafasi ya mkuu wa mkoa, ukiwemo Kilimanjaro, Mbeya na Katavi katika Serikali ya awamu ya tano.

Chini ya uongozi wa Rais Samia, Makalla amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza alikohudumu hadi Machi 31, mwaka huu.


Mongella ni nani?

Jina la John Mongella si geni sana katika masikio ya Watanzania, lakini pengine asiwe na umaarufu katika nafasi za uongozi ndani ya CCM.

Utumishi wake katika nafasi za uteuzi, ulianza mwaka 2010 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa Wilaya ya Kigoma.

Alihudumu kwenye nafasi hiyo hadi mwaka 2012 alipohamishiwa Wilaya ya Arusha ambako nako hakuhudumu muda mrefu hadi pale alipopandishwa kuwa mkuu wa Mkoa.

Novemba mwaka 2014, Rais wa wakati huo, Kikwete alimteua Mongella kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, akipanda kutoka kuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Baadaye Machi mwaka 2016, Rais wa awamu ya tano, John Magufuli alimteua kuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, nafasi aliyohudumu hadi Mei mwaka 2021.

Kisha mwanasiasa huyo aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, wadhifa ambao alibadilishiwa siku ya kuapishwa kwake.

Katika uapisho wa nafasi hiyo, Rais Samia alitangaza kumhamisha Mongella kutoka Simiyu kwenda mkoani Arusha, kwa kile alichoeleza, kiongozi huyo ameshakuwa na uzoefu wa kuongoza majiji.

Alihudumu katika wadhifa huo hadi Machi 31, mwaka huu Rais Samia alipomteua Makonda kurithi nafasi hiyo, huku taarifa ikieleza Mongella angepangiwa kazi nyingine.


Huyu ndiye Hapi

Kwa upande wa Hapi, ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya sheria na shahada ya uzamili ya masuala ya biashara na utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aprili 16, mwaka 2016 hayati Magufuli alimteua kuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, baadaye mkuu wa mkoa wa Iringa na Mei 15, 2021 Rais Samia alimteua kuwa mkuu wa mkoa wa Tabora kisha mkoa wa Mara.

Julai 28, mwaka 2022 Rais Samia alitengua uteuzi wake na tangu wakati huo alionekana katika mitandao ya kijamii akijihusisha na shughuli za kilimo.


Safari ya Jokate

Jokate, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2018 aliteuliwa na Magufuli mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, baadaye Temeke na kisha Korogwe.

Safari yake ya chama ilianza Oktoba 2023 NEC ya CCM ilipomteua kuwa Katibu Mkuu wa UWT.

Hata hivyo, kuteuliwa kwake ndani ya UVCCM si mara ya kwanza, kwani aliwahi kuwa Katibu Hamasa na Chipukizi wa jumuiya hiyo.