Dk Ndugulile aitaka Serikali kudhibiti matumizi ya chumvi, sukari

Muktasari:

  • Dk Ndugulile ameitaka Serikali kubadilisha mfumo wa kuangalia zaidi magonjwa yanayoambukiza, kwa sababu wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukizwa ni wateja wa kudumu wa huduma za afya.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ameishauri Serikali kuweka mfumo wa udhibiti wa matumizi ya chumvi, sukari na mafuta kwenye vyakula vinavyozalishwa viwandani ili kuwaweka salama walaji wake.

Dk Ndugulile amebainisha hayo leo Februari 21, 2023 wakati wa mjadala wa Mwananchi Twitter Space uliokuwa na mada inayohusu “Jinsi ya kuepuka magonjwa yasababishwayo na matumizi chumvi ya mezani”.

Amesema mfumo wa Tanzania umejengwa kwa kuangalia magonjwa yanayoambukizwa na siyo magonjwa yasiyoambukiza. Ameitaka Serikali kubadilisha mfumo huo kwa sababu wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukizwa ni wateja wa kudumu wa huduma za afya.

“Wenzetu wa Ulaya na Marekani wameweza kudhibiti waandaaji wa vyakula kwa kuhakikisha wanazingatia udhibiti wa sukari, chumvi na mafuta kwenye vyakula wanavyozalisha. Suala hili ni muhimu nasi tukaanza kuliangalia,” amesema Dk Ndugulile.

Ameongeza kwamba kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uelewa wa madhara yanayosababishwa na matumizi ya juu ya bidhaa za chumvi.

“Wataalamu wa afya wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanafahamu madhara ya matumizi yaliyopitiliza ya chumvi, sukari na mafuta,” amesema Dk Ndugulile wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Twitter Space.

Dk Ndugulile Ameongeza kwamba: “Ni vizuri Wizara ya Afya ikakamilisha Sera ya Afya, tuna sera ya zamani ya mwaka 2007, ni vizuri wakaifanyia mapitio pamoja na kuangalia masuala ya lishe kuanzia ngazi ya uzalishaji hadi chakula.”

Kwa upande wake, Msemaji wa sekta ya afya, ACT Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa kuhudumia magonjwa yasiyoambukizwa hasa kupitia bima ya afya ambayo chama chake kinapendekeza ifungamanishwe na mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Huduma ya afya ya msingi iimarishe ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yana gharama kubwa, lazima tuwe na mfumo endelevu na bora utakaowezesha Taifa kuhudumia magonjwa hayo,” amesema Dk Sanga.