Dk Ndugulile: Muundo wa MSD chanzo cha matatizo

Muktasari:
- Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekiri muundo wa bohari hiyo hauakisi utendaji kazi hivyo jambo hilo wanalifanyia kazi kwani ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha dawa zinapatikana katika vituo vya afya huku ikiiomba Serikali kuangalia muundo wa bohari hiyo kwani ndio chanzo kikubwa cha matatizo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo Alhamisi Aprili 13,2023, katika Bohari ya Dawa, jijini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo amesema wataendelea kuupima utendaji kazi wa MSD kwa upatikanaji wa dawa.
“Mheshimiwa waziri sisi kama kamati tunatambua juhudi zako pamoja na watumishi wote. Utunzaji wa dawa, ununuzi wa dawa si sawa na bidhaa zingine kitu ambacho kina utaalamu wake ambao tunatambua jinsi ambavyo mnapambana,” amesema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Faustine Ndugulile ameitaka Serikali kuangalia muundo wa taasisi hiyo kwani umekuwa na shida.
“Nikuombe mheshimiwa waziri, Muundo wa MSD kwa sasa hivi ndio chanzo kikubwa cha matatizo kwa sababu muundo hauakisi majukumu ya taasisi, muundo umekaa kiutawala zaidi, hili naliona ni moja ya tatizo,”amesema Dk Ndugulile ambaye ni Mbunge wa Kigamboni.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekiri muundo wa bohari hiyo hauakisi utendaji kazi hivyo jambo hilo watalifanyia kazi kwani ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia, Waziri Ummy amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni matoeo ya dawa kutokuwa sawa hali ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu.
Awali, Mkurugenzi wa MSD, Tukae Mavere amesema wamefanikiwa kusambaza dawa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa watendaji.