Dk Ndumbaro: Watetezi si wapinzani wa Serikali

Muktasari:

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema Watetezi wa Haki za Binadamu sio wapinzani wa Serikali kwani wamekuwa wakiisaidia kutekeleza shughuli mbalimbali za kukuza na kulinda haki za binadamu na haki za watu.

Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema Watetezi wa Haki za Binadamu sio wapinzani wa Serikali kwani wamekuwa wakiisaidia kutekeleza shughuli mbalimbali za kukuza na kulinda haki za binadamu na haki za watu.

Kauli hiyo imetolewa siku moja kabla ya maadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Dk Ndumbaro ameyasema hayo leo Alhamisi, Mei 12, 2022 wakati wa kikao cha kupitisha mpango kazi wa asasi za kiraia kuhusu mapendekezo yaliyokubaliwa na Tanzania kwenye duru la tatu la mchakato wa tathmini wa haki za binadamu wa umoja wa mataifa (UPR) ulioandaliwa na THRDC.

“Ninyi siyo wapinzani wa Serikali, ninyi ni washirika wa Serikali na hili mmelithibitisha vizuri sana  kwenye mkutano wa 49 wa baraza la haki za binadamu kule Geneva ambapo mlisimama bega kwa bega na Serikali mkafanya mchakato na hatimaye kukubaliana kwa kauli moja na kupitisha maazimio 187 ambayo tutaanza kuyatekeleza.

“Lakini hamkuishia tu kuyaandaa mlienda kuhakikisha nchi zote zinapitisha maazimio hayo kwa kauli moja niwapongeze, mlipopitisha hamkukaa tu mliona lazima muweke mpango mkakati wa utekelezaji wake ili kuonyesha tumefanya nini na tumekwama wapi ila ifikapo duru ya nne tuwe tumefanikiwa kutekeleza yote 187,” amesema Dk Ndumbaro.

Amesema msimamo wa Serikali uliwasilishwa rasmi mbele ya Baraza la Haki za Binadamu Machi 23 mwaka huu, katika upigaji wa kura hakuna nchi iliyopinga msimamo wa Tanzania.

“Hivyo basi, msimamo wa nchi kutekeleza mapendekezo 187 uliidhinishwa rasmi na baraza na Tanzania limeingia katika duru ya nne ya mfumo huu ambapo tumepangiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendezo tutakayoyatekeleza ifikapo Julai, 2026,” amesema.

Ofisa Programu THRDC, Perpetua Senkoro amesema wanashkuru ushirikiano na mwitikio wa Serikali kuongeza mapendekezo na wiki hii wanapoadhimisha miaka 10, Serikali imekua ikiwaunga mkono kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha kuna ubora katika kutekeleza haki za binadamu nchini.