Dk Philip Mpango ni nani?

Dk Philip Mpango ni nani?

Muktasari:

  • Makamu wa Rais mteule, Philip Mpango ni mwanasiasa Mtanzania na mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye alichaguliwa kuwa mbunge kwa uteuzi wa Rais wa tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli mwaka 2015 – 2020 kabla ya kwenda kugombea Jimbo la Buhigwe lililopo mkoani Kigoma mwaka 2020.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais mteule, Philip amezaliwa katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Julai 14, 1957. Alisoma shule ya msingi Kipalapala na Muyama, alijiunga seminari ya Ujiji na baadaye seminari ya Utaga Tabora.

Alijiunga kidato cha tano na sita katika sekondari ya Ihungo, Bukoba na alihitimu mwaka 1977  na kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa Uhombora na baadaye JKT Songea.

Dk Mpango ambaye ni Waziri wa Fedha na Mipango, amesema hayo leo Jumanne Machi 30, 2021 baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza jina lake katika kikao cha kwanza cha Bunge la 12.

Amesema baada ya kuhitimu JKT, alifanya kazi kabla ya masomo ya chuo kikuu katika Shirika la NPF na Elimu Supply yote yakiwa mashirika ya Serikali.

“Nilirudi chuo kikuu kuchukua shahada ya uchumi mwaka 1984 baada ya pale nilifanya kazi Wizara ya Kazi kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 1986; niliporejea chuo kikuu kwa ajili ya shahada ya pili katika uchumi nikamaliza mwaka 1988.

“Nikaajiriwa kama mkufunzi halafu baadaye assistant lecture mwaka uliofuata nilienda masomoni Sweden kwa ajili ya PHD nilirejea mwaka 1992 nikaendelea na utafiti wakati huohuo nikiendelea kufundisha,” amesema Dk Mpango.

Amesema mwaka 1996 alihitimu shahada ya uzamivu katika uchumi na aliendelea kufanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na utafiti mpaka mwaka 2002 alipoamua kwenda kufanya kazi benki ya dunia kama mchumi mwandamizi.

“Haukuwa uamuzi mwepesi sana, niliamua kwenda kule ili nijifunze taasisi hizi kubwa zinazosukuma sera, kuna nini kule ndani nilifanya kazi pale na niliaminiwa kusimamia baadhi ya miradi ya matumizi ya Serikali,” amesema.

Amesema kazi hiyo ilimkutanisha na Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alimteua kama msaidizi wake wa masuala ya kiuchumi.

“Baada ya utumishi wa miaka mitano pale benki ya dunia Dar es Salaam, (JK) aliniteua kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha  nilitumikia mpaka mwaka 2010 (kuanzia 2007), baada ya hapo alinihamisha na kunipeleka kuwa mkuu wa Tume ya Mipango nchini hususan kazi kubwa ya kuandaa mpango wa kwanza wa maendeleo ya miaka mitano,” amesema.

Dk Mpango amesema alitumikia kazi ile kwa zaidi ya miaka mitano na kidogo na mpango wa pili wa miaka mitano uliandaliwa akiwa mkuu wa tume ya mipango kabla ya kuteuliwa na Rais wa tano wa Tanzania, Hayati Dk John Magufuli.

“Magufuli aliniteua nikiwa mkuu wa tume ya mipango akanipeleka kuwa kaimu kamishna mkuu wa mipango Tanzania, nilifanya kazi ile kwa mshangao kama leo kwa mwezi mmoja ilikuwa kazi ngumu sana sababu tulipewa kazi ya lazima tuongeze mipango na changamoto zake.

“Siku hiyo saa 2 usiku nikiwa ofisini, rafiki zangu wakaniambia Rais amekuteua kuwa mbunge na Waziri wa Fedha na Mipango, sauti yangu usiku ule ilikuwa Mungu wangu nisaidie niliona sasa mzigo umekuwa mkubwa zaidi,” amesema.

Tangu hapo Dk Mpango aliendelea kutumikia nafasi hiyo na kuwa miongoni mwa mawaziri watano ambao hawakuwahi kutumbuliwa na Magufuli na kuwa na bahati ya kuteuliwa tena kipindi cha pili na kuendelea kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Leo Machi 30, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan amewasilisha mapendekezo ya jina lake kuwa makamu wa Rais katika kikao maalumu cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na baadaye jina hilo kuwasilishwa bungeni na kupitishwa kwa kura 363 sawa na asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa.