Ahadi ya Dk Mpango kwa Watanzania

Ahadi ya Dk Mpango kwa Watanzania

Muktasari:

  • Unaweza kusema ni ahadi ya Dk Philip Mpango kwa Watanzania. Ni baada ya makamu wa rais huyo mteule kueleza mambo kadhaa atakayoyafanya baada ya kutangazwa na Spika Job Ndugai kuwa amependekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni ahadi ya Dk Philip Mpango kwa Watanzania. Ni baada ya makamu wa rais huyo mteule kueleza mambo kadhaa atakayoyafanya baada ya kutangazwa na Spika Job Ndugai kuwa amependekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.

Akizungumza bungeni leo Jumanne Machi 30, 2021, Dk Mpango ameeleza ndoto zake za kuibadilisha Tanzania kwa kusimamia rasilimali za nchi na kuahidi kuitoa nchi katika kipato cha chini mpaka kuwa nchi yenye kipato cha juu.

Mteule huyo amesema ni lazima kuwa na uwajibikaji kwa kufanya kazi kwa uwezo na akili zote kwa manufaa ya nchi.

“Jina langu limeletwa kwenu kwa pendekezo la Rais kwa ajili ya kazi hiyo ngumu ya kumsaidia yeye kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu. Nataka niseme kwamba alipofariki Dk John Magufuli nililia sana hadharani lakini pia hata binafsi huko nyumbani lakini baadaye machozi yangu yalikauka kwa sababu Tanzania lazima iendelee.”

“Jambo muhimu sana tunaloweza kumtendea haki ni kuisha ndoto yake  lazima tuibadilishe Tanzania, lazima tusimamie rasilimali za nchi yetu kwa nafasi ya bunge,” amesema.

Dk Mpango amesema endapo Bunge litamthibitisha katika nafasi ambayo ni mapendekezo, ahadi yake ni kumuenzi na lazima atende wajibu wake kwa Taifa.

“Ningependa sana tutoke kuwa nchi yenye kipato cha chini na kuwa nchi yenye kipato cha juu katika kipindi kifupi na anawezekana kwa pamoja tukiamua kama Watanzania,” amesema Dk Mpango.

Akimzungumzia Dk Mpango, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema tangu wakiwa wanafanya pamoja kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikuwa mchapakazi.

“Ni mchapakazi na anayesimamia taaluma ya wanafunzi, mlezi na hasa alipoleta wataalamu na wachumi nilimfahamu sana, Dk Mpango ni mcha Mungu na mchapa kazi katika maisha yake yote amekuwa akimtanguliza mwenyezi Mungu, anayejituma na mzalendo wa kweli,” amesema Profesa Ndalichako.