Dk Salim alivyong’ara katika anga za kimataifa

Muktasari:

  • Dk Salim Ahmed Salim, ambaye amefanya kazi ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 50, amefanya mambo mengi ambayo ni viongozi wachache wanaweza kuyafikia.

Dk Salim Ahmed Salim, ambaye amefanya kazi ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 50, amefanya mambo mengi ambayo ni viongozi wachache wanaweza kuyafikia.

Alihudumu katika Umoja wa Mataifa (OAU) katika nyakati zilizokuwa na changamoto nyingi kwa Afrika na dunia kwa ujumla. Kazi yake katika Umoja wa Mataifa iliambatana na misukosuko ya vita baridi na kilele chake.

Nyadhifa zake kimataifa zilianza akiwa na umri wa miaka 22 alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, baadaye India mwaka 1965 na China mwaka 1969.

Januari 1970, aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani alipohudumu kwa zaidi ya miaka 10.

Dk Salim pia ndiye katibu mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika aliyekaa muda mrefu zaidi ya OAU, akiwa na rekodi ya mihula mitatu mfululizo kuanzia 1989 hadi 2001. Akiwa huko alisimamia mabadiliko ya OAU kuwa Umoja wa Afrika (AU).

Kuanzia 2004 hadi 2008, Dk Salim alihudumu kama mjumbe maalumu wa AU kwa Darfur. Kuanzia 2007 hadi 2013, aliwahi kuwa mjumbe wa jopo la wenye hekima la AU, chombo kinachomshauri mwenyekiti wa Tume ya AU na Amani na Usalama wa umoja huo.

Kazi zake Umoja wa Mataifa

Miezi tisa baada ya kuondoka ubalozini China, Dk Salim aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Akiwa katika nafasi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja, Salim aliongoza vyombo mbalimbali vya Umoja wa Mataifa. Mwaka 1979 alikuwa rais wa kikao cha 34 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), kisha vikao maalumu vya dharura vya 6 na 7 vya UNGA (1980) na Kikao Maalumu cha 11 cha UNGA (1980).

Alishika pia nyadhifa katika kamati mbalimbali maalumu. Juni na Julai 1972 alikuwa mwenyekiti wa Ujumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa huko Niue (kisiwa katika Pasifiki ya Kusini), Mjumbe wa Kamati ya Kisiasa ya Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) huko Georgetown, Guyana, Agosti 1972 na mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Mkutano wa Kimataifa wa Wataalamu wa Kusaidia Waathiriwa wa Ukoloni na Ubaguzi wa Rangi Kusini mwa Afrika, wenye makao yake makuu mjini Oslo, Aprili 1973.

Mojawapo ya majukumu makubwa zaidi aliyofanya ni urais wa Baraza Kuu na mwenyekiti wa Kamati ya Kuondoa Ukoloni. Hiyo ilikuwa ni kamati maalumu ya Umoja wa Mataifa ya kuondoa ukoloni.

Alishika wadhifa huo kuanzia mwaka 1972 hadi 1980 na wakati huo kamati ilibeba jukumu kuu katika kuongoza makoloni mengi na maeneo yasiyo ya kujitawala kwa uhuru kamili na uhuru. Pia, mwaka 1975, alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iliyosimamia vikwazo dhidi ya Rhodesia Kusini (sasa Zimbabwe).

Mei 1977 Salim alichaguliwa kuwa makamu wa rais wa Kamati ya Kusaidia Watu wa Zimbabwe na Namibia na aliongoza kamati ya mkutano huo uliofanyika Maputo.

Pia alikuwa rais wa Mkutano wa Kimataifa wa Vikwazo dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini (1981), rais wa Mkutano wa Kimataifa wa Paris dhidi ya ubaguzi wa rangi (1984) na alihudumu katika Tume Huru ya Palme ya Masuala ya Usalama ya Kimataifa.

Kuwania ukatibu mkuu OAU

Mwaka 1981, Dk Salim alionyesha nia ya kugombea nafasi ya katibu mkuu. Hakufanikiwa, ingawa aliungwa mkono na nchi za Afrika, Asia na Kilatini.

Marekani na China, katika nafasi zao kama wanachama wa kudumu, walitumia mamlaka yao ya kura ya turufu dhidi ya wagombea ambao wao hawakuwataka.

Marekani ilimpendelea mgombea wa Austria, Kurt Waldheim, lakini China na Ufaransa zilimuunga mkono Dk Salim. Uingereza na Urusi hazikupiga kura.

Mchakato wa kupiga kura kumpata katibu mkuu unahitaji kuungwa mkono, au angalau kusiwe na upinzani miongoni mwa wanachama wote wa kudumu wa Baraza la Usalama na kura nyingi kutoka kwa Unga.

Mchakato huo wa muda mrefu wa uchaguzi ulirudiwa mara 16 katika kipindi cha wiki tano na Salim alimtaka rais wa Baraza la Usalama la wakati huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda, Balozi Olara Otunnu, kuwasiliana na Baraza la Usalama kuwaambia hataki jina lake lirudishwe kwenye upigaji kura uliofuata.

Ilidhihirika kuwa Marekani haikukata tamaa ya kumzuia Dk Salim kugombea, hivyo alijitoa kuruhusu wagombea wengine wa Afrika wanaotaka kugombea nafasi hiyo. Hatimaye, mwanadiplomasia wa Amerika ya Kusini kutoka Peru, Javier Perez de Cuellar alichaguliwa.

Nyadhifa Umoja wa Mataifa

Akiwa mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Kuondoa Ukoloni, alifanya ziara za kibalozi katika nchi za Uingereza, Tanzania, Zambia, Botswana, Msumbiji na Ethiopia.

Anabainisha kuwa tofauti kati ya nafasi hii na ile ya rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kwamba kamati hiyo ilitoa mapendekezo, wakati Baraza la Usalama lilikuwa na uwezo wa kufanya uamuzi.

Aprili na Mei 1976, Salim aliongoza kikosi cha wajumbe sita kutoka Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Kuondoa Ukoloni. Kikosi hicho kilisafiri hadi Lusaka, Zambia; Dar es Salaam, Tanzania; Addis Ababa, Ethiopia; Maputo, Msumbiji; Gaborone, Botswana na London, Uingereza kushauriana juu ya juhudi za kuondoa ukoloni katika nchi za Rhodesia na Namibia.

Mashauriano haya ambayo yaliwashirikisha wakuu wa nchi na maofisa wa Serikali, wawakilishi kutoka kwa watendaji wakuu wa OAU na kamati yake ya ukombozi, wanachama wa vuguvugu mbalimbali za ukombozi, yalikuwa hatua muhimu ya kuboresha ushirikiano kati ya Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa kuhusu ya kuondoa ukoloni katika Afrika.

Kipindi cha Salim kama mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vikwazo dhidi ya Rhodesia mwaka 1975 na kipindi chake cha mwaka 1976 kama rais wa Baraza la Usalama kilisaidia kufanikisha kupitishwa kwa Azimio 386 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono kupatikana kwa uhuru wa Msumbiji na nchi nyingine kadhaa, ikiwamo Namibia.

Kipindi ambacho Dk Salim alifanya kazi katika Umoja wa Mataifa, kiliinua hadhi ya Afrika na ile ya mataifa mengine yanayoendelea.

Mwaka 1980 alirejea nyumbani kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania hadi 1984 kilipotokea kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine, ndipo alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Salim aliongoza Kamati ya Ukombozi ya OAU mwaka 1983. Mwaka 1988 alimshinda Ide Oumarou, mwanadiplomasia wa Nigeria katika nafasi ya katibu mkuu wa OAU, wadhifa alioshikilia hadi Julai 2001.

Ni mambo gani alifanya akiwa OAU?
Tukutane toleo lijalo.