SIMULIZI YA DK SALIM: Alivyokataa siasa za ndani kuibeba OAU-4

Dk Salim Ahmed Salim ni kielelezo cha kizazi cha viongozi vijana wa baada ya uhuru waliokulia chini ya Sheikh Abeid Amani Karume na baadaye Mwalimu Julius Nyerere, ambao maono na fikra zao juu ya siasa na maendeleo zilichagizwa na hisia kubwa ya uzalendo.

Michango ya Dk Salim katika ngazi ya kitaifa na kimataifa ina uhusiano wa karibu. Alipotoka katika mapambano ya ukombozi, Dk Salim alijiendeleza kutoka mwanaharakati hadi mwanadiplomasia na kujenga msingi imara wa sifa ya Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Katika muda wote wa utumishi wake serikalini, aliinua hadhi ya Tanzania katika masuala ya kimataifa.

Ujasiri na nidhamu ambayo Dk Salim aliipata wakati wa utoto wake na alipokuwa kijana iliweka msingi wa mafanikio yake ya baadaye. Mapenzi yake ya umoja, amani, uaminifu na uadilifu yalizaa kiwango cha juu cha kujitolea binafsi na kitaaluma kuhudumia taifa.

Kwa kutambua kazi na mchango wa Dk Salim, nchi kadhaa za Afrika zilimtunuku tuzo za heshima.

Wakati Dk Salim anaondoka nchini kwenda kufanya kazi katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), alikuwa akijihusisha sana na shughuli za Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya chama na Katibu wa Mambo ya Nje na Katibu wa Tume ya Ulinzi na Usalama.

Mambo mawili yalikuwa yanamsumbua. Kwanza ni kuimarisha mamlaka ya juu kabisa ya chama ambapo aliamini viongozi walipaswa kuwa na ujuzi wa masuala ya mambo ya nje kwa sababu chama tawala ndicho kilikuwa mhusika mkuu katika kutunga na kutekeleza sera ya kigeni.

Jambo la pili lilikuwa ni hitaji la nchi kuimarisha msingi wake wa kiuchumi. Kutokana na uzoefu wake mkubwa katika mambo ya nje ya Tanzania, alikuwa na uwezo wa kubashiri kitakachotokea katika mkondo wa mambo ya nje ya Tanzania, kwani uchumi ulikuwa ukitegemea zaidi taasisi za fedha za kimataifa (Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani).

Kwa kutambua uzoefu, uadilifu na dhamira ya Salim, Watanzania wengi walijaribu kumshawishi agombee urais mwaka 1985 lakini hawakufanikiwa, licha ya kuamini ndiye aliyefaa kurithi mikoba ya Mwalimu Julius Nyerere.

Julai 1988, Salim alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa OAU--wadhifa ambao hatimaye aliushikilia kwa miaka 12 mfululizo.

Kwa mujibu wa Julius Edo Nyang'oro katika kitabu chake, 'JK: A Political Biography of Jakaya Mrisho Kikwete, President of the United Republic of Tanzania', mwaka 1995 Mwalimu Nyerere alimtaka tena Salim kugombea urais baada ya Ali Hassan Mwinyi kumaliza mihula miwili ya uongozi, lakini hatimaye uteuzi ukaenda kwa Benjamin Mkapa.


Kurejea Tanzania

Baada ya muda wake wa kuwa Katibu mkuu wa OAU kumalizika Septemba 2001, Salim alirejea Tanzania baada ya kuutumikia umoja huo kwa mihula mitatu mfululizo.

Wakati wa uongozi wake katika OAU, Dk Salim hakujihusisha kikamilifu na siasa za ndani nchini Tanzania, kwa sababu, kulingana na alivyokiri mwenyewe, "Huwezi kuwa katibu mkuu wa OAU na wakati huo huo ukijihusisha na siasa za nchi yako ... unakuwa mwanaharakati wa nchi zote za Afrika."

Aliporejea Tanzania, Salim, ambaye kwa sasa ni mwana-Afrika, hakuwa na nafasi yoyote ya kisiasa hadi Rais Mkapa alipomteua kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Baada ya hapo, Rais Jakaya Kikwete alimteua Salim kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa na kupendekeza jina lake kuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

Amekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki.

Mwaka 2011 Rais Kikwete alimteua Salim, pamoja na makamishna wengine 29, kuhudumu katika Tume ya Marekebisho ya Katiba ya nchi, kazi ambayo walikamilisha kwa mafanikio mwaka 2013 na pia amekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Salim alipochukua nafasi ya uongozi wa taasisi hiyo, aliendelea kutekeleza malengo yake, kama yalivyowekwa na Mwalimu Nyerere, hususan kwa kuandaa semina, warsha na makongamano katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, ikiwa ni pamoja na makongamano ya kimataifa ya mwaka 2002 na 2004 kuhusu Ukanda wa Maziwa Makuu yaliyofanyika jijini Kampala, Dar es Salaam na kwingineko.

Idadi ya nchi zinazounda eneo la Maziwa Makuu iliongezeka kutoka sita hadi 12 katika kipindi hicho.

Mwaka 2005 Salim aliombwa na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) wakati huo, Alpha Oumar Konare, kuwa mjumbe maalumu nchini Sudan.

Alipokuwa mpatanishi wa mgogoro wa Darfur nchini Sudan kuanzia mwaka 2005 hadi 2007, alifanya jitihada za kupatanisha pande zinazozozana akishirikiana na timu yake kuchukua hatua mbalimbali ili kufikia lengo hilo, ikiwamo kuandaa mkataba wa amani wa Darfur.

Somo jingine ambalo Salim ataendelea kukumbukwa nalo ni suala la wakati.

Anaamini kutokuwapo kwa mafanikio makubwa katika migogoro mingi ya Afrika, hasa mzozo wa Sudan kwa sababu wakati wa kusuluhishwa unakuwa haujawadia.

Utatuzi wa migogoro unakuwa rahisi wakati pande mbili zinazozozana zinapochagua kwa hiari kumaliza mzozo. Kwa hiyo, kitendo cha Tanzania kuingilia kati mgogoro huo wa Desemba 2014 kwa kiasi kikubwa ulikuwa wakati muafaka kwa sababu pande zinazohusika katika mzozo wa Sudan Kusini, Salva Kiir na Riek Machar, zilijitolea kushughulikia mambo yanayosababisha mzozo kati yao.

Dk Salim ameongoza na kuwa mjumbe wa tume kadhaa za Umoja wa Mataifa, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na AU.

Pia alikuwa mwenyekiti mwenza wa Kundi la Watu Mashuhuri na mjumbe wa Kundi la Wataalamu Mashuhuri lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufuatia Mkutano wa Dunia wa Durban dhidi ya Ubaguzi wa Rangi na Ubaguzi dhidi ya Wageni (Xenophobia).

Alikuwa katika Tume ya Ushauri wa Sera ya Shirika la Dunia la Haki Miliki. Kufuatia mwaliko kutoka kwa rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, alihudumu nafasi ya Ubalozi wa Maji Afrika tangu 2002, akiwa na jukumu la utetezi, uhamasishaji na uhamasishaji wa msaada.

Katika muda wote wa utumishi wake katika Serikali ya Tanzania, Dk Salim ameendelea kuwa muumini na mtetezi mkubwa wa maadili ya uongozi, uadilifu na kujitolea kuwatumikia wananchi.

Bila shaka, hii inaweza kuwa moja ya maelezo muhimu ya imani ya Mwalimu Nyerere kwa Dk Salim. Alikuwa miongoni mwa viongozi wachache makini na wenye kuchagua maneno ya kuzungumza mbele ya waandishi wa habari. Aliwahi kuulizwa kwa nini yupo kimya, jibu lake lilikuwa "Si lazima kila wakati mtu atoe maoni yake juu ya masuala. Hata kunyamaza ni njia ya kutoa maoni."

Salim anaendelea kudumisha umuhimu wa kuzingatia maadili ya uongozi na kwamba viongozi wa Tanzania wanapaswa kuwatumikia wananchi wao na si masilahi yao binafsi.


Mara tu baada ya uhuru wa Zanzibar mwaka 1963, Mapinduzi ya Januari 1964 na Muungano uliofuata kati ya Tanganyika na Zanzibar mwaka huo huo, Dk Salim aliteuliwa kuiwakilisha Serikali ya Tanzania katika nchi za Misri, India na China kabla ya kurejeshwa nyumbani kwa majukumu mbalimbali.

Hii ni tofauti na wanadiplomasia wengine wengi wa kizazi chake ambao walipata uzoefu katika utumishi wa Serikali kabla ya kupelekwa nje ya nchi.

Itaendelea kesho