Dk Serera: Ubora wa huduma kwa wateja ni kigezo kikuu cha ushindani wa kibiashara
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk Suleiman Serera akimkabidhi tuzo Meneja wa Masoko na Burudani wa Amell Ayoub Mbarazi kwenye ukumbi wa Mlimani city jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Hassan Serera, amebainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma, huku akisisitiza kuwa ubora wa huduma kwa wateja ndio kigezo kikuu cha ushindani wa kibiashara.
Dk Serera ameyasema hayo wakati akihudhuria hafla ya utoaji wa tuzo za Wiki ya Kimataifa ya Huduma kwa Wateja Tanzania, iliyoandaliwa na Taasisi ya CSW, tarehe 9 Oktoba 2025, jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa hatua hiyo inaonesha namna ambavyo nchi imejizatiti kuandaa wananchi wake kushiriki kikamilifu katika sekta ya huduma na biashara, huku akiongeza kuwa Watanzania wazawa ndio wanaoongoza katika utoaji wa huduma bora.
"Kama nchi tunajipima vizuri katika suala la utoaji wa huduma kwa sababu kipimo cha kwanza ni aina ya watu wanaohusika katika uwekezaji. Wanaotoa huduma nyingi sasa ni Watanzania wazawa, jambo linaloonesha tumepiga hatua kubwa katika kuwaandaa watu wetu," amesema Dk Serera.
Aidha, amesisitiza kuwa ili kuvutia wawekezaji kutoka nje, ni muhimu kuwa na wananchi walioboreshwa kitaaluma na kiutendaji katika sekta ya huduma, akionyesha kuridhishwa na hali hiyo kutokana na kuona Watanzania wengi wakiwa ndio wanaosimamia huduma na kuendesha shughuli kwa ufanisi mkubwa.
“Tumeona watu waliopokea tuzo na walioongozana nao ni Watanzania.
Hawa ndio wanaokutana na wateja wetu wa ndani, wanazungumza lugha ya ushawishi na kutoa huduma bora. Huu ndio ushindani tunaoutaka kuona katika taasisi na makampuni yetu,” ameongeza.
Dk Serera pia alionya kuwa taasisi au kampuni yoyote isiyotoa huduma bora inajiweka katika hatari ya kupoteza wateja, na kuongeza kuwa mteja akihudumiwa vibaya, ni rahisi asirudi tena. Hivyo, huduma bora ni msingi wa biashara endelevu.
Ameongeza kuwa katika mazingira ya ushindani wa kibiashara, biashara na uzalishaji sasa vinahitaji ubunifu na ubora wa huduma kama silaha kuu ya ushindani.
“Mtanzania kwa asili ni mkarimu, lakini sasa tunapaswa kuongeza ubora katika huduma zetu. Bidhaa bora bila huduma bora bado haijakamilika,” amesisitiza Dk Serera.
Pamoja na hayo, Dk Serera ameishukuru Taasisi ya CSW kwa kuandaa hafla ya tuzo, huku akiwapongeza washindi wa tuzo hizo. Aliwataka viongozi wa sekta zote, hususan za serikali, kuendelea kuboresha huduma zao ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora kila wakati.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa CSW Group, Annelise Nyangusi, ameeleza kuwa katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, huduma kwa wateja ni chachu muhimu ya kukuza biashara na kampuni. Aliweka wazi kuwa mchakato wa kutambua washindi wa tuzo unafanywa kwa uangalifu mkubwa kupitia kamati maalum inayochambua kwa kina vigezo mbalimbali ili kubaini kampuni zinazostahili kutunukiwa.
"CSW Tanzania tumeona umuhimu wa kutambua na kutunuku kampuni, mashirika, na wafanyabiashara wanaofanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wateja," amesema Nyangusi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Irene Gowele, alishukuru kwa kupokea tuzo hiyo, akielezea kwamba mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, katika kuwekeza katika sekta ya nishati.
“Tunajivunia kupata tuzo hii. Hii itatufanya tuendelee kuboresha zaidi huduma zetu kwa wateja, ili kuhakikisha wanahudumiwa kwa wakati na kwa ufanisi,” amesema Gowele, akiongeza kuwa maboresho ya huduma kwa wateja yakiwemo ununuzi wa vitendea kazi kama pikipiki, bajaji, na magari, yameongeza ufanisi wa shirika
Meneja wa Masoko na Burudani kutoka Amell ni Dar, Ayoub Mbarazi, alisema kuwa ushirikiano na kazi kwa bidii ndiyo siri ya mafanikio ya kampuni yao katika utoaji wa huduma bora kwa wateja, na alieleza furaha yao kwa kupata tuzo hiyo.
"Tumefurahi kupokea hii tuzo, na tunakiri kuwa ushirikiano na kujituma ndiyo imekuwa chachu ya mafanikio yetu. Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kushinda tuzo nyingi zaidi," amesema Mbarazi.
Steven Mkomwa, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Sekta ya Ujenzi na Miundombinu ya Tanzania (CCIT), amesema kuwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa kutambuliwa kwa mchango wao katika utoaji wa huduma bora kwa wateja, hasa katika sekta ya ujenzi na miundombinu.
Mkomwa ameongeza kuwa tuzo hiyo inawahamasisha zaidi katika kuboresha huduma na kuleta ubunifu zaidi katika sekta hiyo nchini.
Philemon Matoi, Mkurugenzi wa Masoko na Usambazaji wa LS General Supply Ltd, kampuni inayojulikana kwa usambazaji wa taulo za kike na wadhamini wakuu wa hafla hiyo, alielezea furaha yao kwa kuwa miongoni mwa washindi. Alisema kuwa tuzo hizo zinachochea uhusiano mzuri kati ya biashara na biashara na ni muhimu kwa ukuaji wa sekta nzima ya biashara nchini.
“Tunajivunia kuwa miongoni mwa washindi na tunasisitiza umuhimu wa kutunza na kuendeleza tuzo hizi kwa manufaa ya biashara na huduma kwa wateja,” amesema Matoi.