Dk Tizeba alia na wizara ya kilimo

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba.

Muktasari:

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa kuwezesha kilimo kufikia uchumi wa viwanda mjini Dodoma jana.

Dodoma. Licha ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kusheheni wasomi waliobobea, sekta hiyo imeshindwa kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa, imeelezwa.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa kuwezesha kilimo kufikia uchumi wa viwanda mjini Dodoma jana.

Dk Tizeba aliyemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema wizara hiyo ina vituo 27 vya utafiti wa kilimo, lakini wakulima wengi hawajafaidika.

“Ukitaka kujua mahali walipo wazamivu (PhD) wengi katika nchi hii, basi wako Wizara ya Kilimo. Tangu miaka ya 1970 kulikuwa na vituo vya utafiti wa kilimo, leo tuna vituo 27 nchi nzima. Pamoja na weledi walionao, wizara haija-perform (haijafanya) vizuri.

“Ungetegemea leo kilimo kingekuwa kinachangia pato la Taifa kwa asilimia 60, lakini kila siku maendeleo yanazidi kushuka. Bahati mbaya wasomi wanatuangusha. Mimi napenda kusema kweli,” alisema Dk Tizeba.

Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikipata hasara kwa kukosa mbinu za kilimo na biashara.

Makamu mwenyekiti wa Ansaf, Profesa Damian Gabagambi alisema ili kilimo kiwezeshe ukuwaji wa viwanda, kwanza inatakiwa nchi iwe na Amani na utulivu, ukuaji wa sekta ya uchumi na ongezeko la watu na upatikanaji wa nishati na maji.