Mazito yamkuta baba aliyembaka mwanaye wa miaka saba

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kifungu cha 131(30 cha Kanuni ya adhabu RE 2022, adhabu kwa kosa la mtu anayebaka msichana mwenye umri wa chini ya miaka 10 ni kifungo cha maisha jela.

Moshi. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya firauni, ni usemi unaoweza kutumika kuelezea tukio la baba mzazi huko Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, kumbaka mwanaye mwenye umri wa miaka saba anayesoma darasa la kwanza.

Lakini kama usemi wa Waswahili unavyosema, siku ya kufa nyani miti yote huteleza, ndicho kilichomkuta mzazi huyo baada ya kukata rufaa kupinga kifungo cha miaka 30 jela alichopewa mwaka 2023, lakini akaongezewa na kuwa kifungo cha maisha.

Mzazi huyo alishitakiwa chini ya kifungu 130(1)(e) na 131(1)(a) cha kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo 2022 ikisema ni kosa kwa mtu wa jinsia ya kiume kumbaka msichana au mwanamke bila ridhaa yake akiwa na umri wa chini ya miaka 18.

Ili kumlinda mtoto na unyanyapaa na kumsababishia mateso ya kiakili na kisaikolojia, jina la baba linahifadhiwa ili kukwepa jina hilo kutumika kumtambulisha mtoto kwenye jamii.

Hukumu ya kumuongezea kifungo hicho kutoka miaka 30 kwenda maisha, imetolewa Aprili 29, 2024 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi, Lilian Mongela, aliyesema adhabu ya kifungo cha miaka 30 haikuwa sahihi kisheria.

Ushahidi wa upande wa mashitaka uliowasilishwa Mahakama ya Wilaya ya Siha mwaka 2022, unaeleza kuwa kosa hilo lilitendeka Mei 14,2022 katika Kijiji cha Lomakaa,  baba huyo alimbaka mwanaye huyo aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Lomakaa.

Ilielezwa kuwa mara kadhaa kwenye kitanda cha wageni katika nyumba yao, baba huyo alimwigilia mwanaye huyo aliyeamua kumweleza mtoto mwenzake wanayesoma naye ambaye alimshauri akamweleze suala hilo dada mkuu wao.

Dada mkuu naye alimjulisha mwalimu mkuu ambaye naye alimshirikisha mwanaharakati wa kupinga ukatili wa kingono aliyewashauri kutoa taarifa kweye dawati la jinsia kituo cha Polisi Sanya Juu na baadae mtoto alipelekwa hospitali kuchunguzwa.

Huko, daktari aliyemfanyia uchunguzi alibaini sehemu zake za haja kubwa hazikuwa zimeingiliwa isipokuwa kwenye uke wake hakuwa na bikira na uke wake huo ulikuwa umeongezeka upana wa inchi moja akisema kiini ni kuingiliwa na kitu butu.

Vipimo vya maabara vilionyesha pia kuwa uke wake ulikuwa unatoa harufu na alikuwa na maambukizi (infection) na daktari alimwanzishia rasmi dawa kumtibu. Upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watano akiwamo daktari aliyemchunguza mtoto.


Mshitakiwa alivyojitetea kortini

Baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wake, Mahakama ilimuona mshitakiwa ana kesi ya kujibu, hivyo kutakiwa kujitetea . Na katika utetezi wake alisema mzazi mwenzake ambaye ni mama wa mwathirika (victim) walishatengana kitambo.

Baada ya kutengana, aliieleza Mahakama kuwa mzazi mwenzake huyo alitaka haki ya kuishi na mtoto na alimkatalia ombi lake hilo na hapo mwanamke huyo alimtisha kuwa atafanya jambo ambalo hatakaa asahau na shitaka hilo ametengenezewa.

Shahidi wake wa pili naye hakuwa mbali na kile alichokisema mrufani huyo kwamba, mama wa mtoto aliomba haki ya kuishi na mwanaye na kukataliwa na baada ya kukataliwa alitoa maneno kuwa angewafanyia kitu kibaya ambacho hakukieleza.

Alieleza kuwa Juni 14, 2022 alibaini mtoto alichelewa kutoka shule na alipofuatilia alibaini kuwa alikuwa amechukuliwa kutoka shuleni saa tano asubuhi na alipoenda shule ndipo alipobaini kuwa mtoto huyo alikuwa amebakwa usiku saa mbili.

Pamoja na utetezi huo, hakimu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Elibahati Petro aliukataa utetezi wake na kumtia hatiani kwa kosa hilo akisema upande wa mashitaka ulikuwa umethibitisha shitaka hilo na kumhukumu kifungo cha miaka 30.

Hata hivyo, hakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa Mahakama Kuu akiegemea hoja nne ikiwamo kuwa hakimu alikosea kumhukumu kwa kuegemea ushahidi wa shahidi wa 1 (mwathirika) na wa 2 ambao ni watoto, ulichukuliwa kinyume cha sheria.

Pia, alieleza hakimu alikosea kisheria kwa kumtia hatiani wakati kulikuwa hakuna uthibitisho wa umri wa mtoto, mashitaka dhidi yake hayakuthibitishwa na kuacha shaka na alimhukumu bila kuzingatia utetezi wa upande wa mashitaka.

Upande wa Jamhuri kupitia kwa Wakili wa Serikali, Henry Daud ulipinga hoja zote za mrufani na kusisitiza kuwa mashitaka dhidi ya mshitakiwa yalithibitishwa katika viwango vinavyokubalika kisheria, hivyo kutiwa kwake hatiani kulikuwa sahihi kisheria.

Wakili huyo alienda mbali na kuiomba Mahakama kubadili adhabu ya miaka 30 aliyopewa baada ya kutiwa hatiani na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela ambayo ndio adhabu sahihi kulingana na kifungu cha 131(1) cha Kanuni ya adhabu RE 2022.


Hukumu ya Jaji Mongela

Katika hukumu yake, Jaji Mongela alizungumzia hoja ya mrufani kuwa ushahidi wa mwathirika na mwanafunzi mwenzake kuwa hakimu hakuzingatia taratibu lakini Jaji akasema swali ni kama ushahidi wa mashahidi hao ulikuwa na mashiko kiasi gani.

Jaji alisema shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye ni mtoto mwenyewe alitoa ushahidi akisema mshitakiwa ni baba yake mzazi na alikuwa amemfanyia tabia mbaya na kuonyesha sehemu ya siri kuwa ndio humfanyia tabia mbaya.

Akinukuu ushahidi wa mtoto Jaji alisema mtoto alisema: “Baba ananifanyiaga tabia mbaya katika chumba cha kulala wageni.”

Jaji alisema inavyoonekana, ushahidi wa mtoto ulikuwa wa moja kwa moja wala haukuwa wa kutiliwa shaka. Alisimama katika kile anachokisema muda wote akitoa ushahidi wake hata wakati alipododoswa maswali na upande wa utetezi,” alisema Jaji.

“Kwa mazingira hayo, sioni sababu ya kutilia shaka ushahidi wake na naona dosari katika kuzingatia kifungu cha 127(2) cha sheria ya ushahidi haikufanya ushahidi wa mtoto usiaminike wala kutomtendea haki mshitakiwa,” alieleza Jaji katika hukumu yake.

Jaji alisema katika utetezi wake, mshitakiwa alidai kesi hiyo ilikuwa imetengenezwa na walimu wa mtoto kwa kushirikiana na mzazi mwenzake aliyetaka haki ya kuishi na mwanaye lakini Jaji akasema anaukataa utetezi huo kwa kuegemea hoja mbili.

Moja ni kwamba mrufani huyo hakueleza ni sababu gani ziliwafanya walimu wamtengenezee kesi hiyo dhidi ya mwanaye mwenyewe na pili mtoto alikuwa karibu zaidi na baba na rafiki wa mtoto kuliko mama, hivyo isingekuwa rahisi kumbambikia.

Jaji alisema pia hakuna ushahidi namna gani mama wa mtoto alikuwa akimtembelea mara kwa mara mtoto ili awe naye karibu kiasi kwamba aweze kutengenezea hadithi ya uongo dhidi ya baba yake aliyekuwa akimlea tangu alipotelekezwa na mama yake akiwa na umri wa miezi saba.

Kutokana na ushahidi huo, anaona kuwa Mahakama ya Wilaya ya Siha ilikuwa sahihi kumuona mrufani ana hatia ya kosa aliloshitakiwa nalo na akazungumzia ombi la Jamhuri kubadili kifungo na akakubaliana nalo na kukiongeza hadi kuwa cha maisha.

Jaji alisema kwa mujibu wa kifungu cha 131(30 cha kanuni ya adhabu RE 2022, adhabu kwa kosa la mtu anayebaka msichana mwenye umri wa chini ya miaka 10 ni kifungo cha maisha jela hivyo naye anabadili kifungo hicho na kuwa kifungo cha maisha jela.