Dk Tulia anavyoikabili mitihani iliyoachwa na Job Ndugai

Thursday May 19 2022
spika pic

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson

By Habel Chidawali

Mkutano wa saba wa Bunge la 12 unaendelea jijini Dodoma, huku wabunge wakishuhudia baadhi ya mambo yaliyowahi kutokea katika mabunge yaliyopita.

Mkutano huu unaacha mitihani mbalimbali anayokabiliana nayo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, kubwa likiwa na kuamua hatima ya wabunge 19 wa viti maalumu Chadema na mengine kadhaa yaliyoachwa na mtangulizi wake.

Mitihani hiyo inamkuta Dk Tulia ikiwa miezi minne tangu alipochukua kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Job Ndugai aliyejiuzulu mwanzoni mwa mwaka huu.

Wakati wa uongozi wa Ndugai yalitokea mambo kadhaa, ikiwemo upitishwaji wa sheria ambazo baadaye zililalamikiwa na wananchi, wabunge na hata spika mwenyewe.

Miongoni mwa sheria ambazo hata Ndugai alieleza kushangaa ni ya utaifishaji mifugo inayoingia kwenye hifadhi, akisema haifai na akahoji huenda ilipitishwa wakati wabunge wakiwa wamelala.

Jambo hilo liliwashangaza wengi na kuhoji umakini wake na Bunge wakati wa upitishwaji wa sheria mbalimbali. Dk Tulia anatakiwa ama kukwepa ili asiingie kwenye mtego kama huo, huku akicheza karata zake vizuri kusahihisha baadhi ya mambo.

Advertisement

Sheria nyingine zilizoleta sintofahamu ni zile za habari, utangazaji, takwimu, ugaidi, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha pamoja na ile ya vyama vya siasa.

Kwenye mitihani inayotajwa kuwa ni midogo, ipo hofu ya baadhi ya wabunge, kwani wakati wa Ndugai baadhi walipoteza matumaini kutokana na yaliyowakuta.

Baadhi waliokutana na mkono wa Ndugai alikuwa ni Nape Nnauye, aliyekemewa kutokana na kuwaita wabunge 19 wa viti maalumu ni Covid-19. Wengine ni

Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima na mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa ambao walihojiwa kwenye Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu kauli walizozitoa nje ya Bunge na baadaye kuadhibitiwa kukosa mikutano miwili ya Bunge.

Pamoja na adhabu hiyo, wabunge hao walitakiwa kuangaliwa kuhusu mienendo yao nje ya Bunge.

Gwajima alikuwa akituhumiwa kwa makosa ya kusema uongo na kushusha hadhi ya Bunge, huku Silaa akikabiliwa na tuhuma zilizotajwa kwamba ni kuchonganisha wananchi na Bunge.


Mtihani kwa Tulia

Dk Tulia anakutana na mtihani mkubwa unaomweka kwenye vipimo vya ulinganifu na watangulizi wake kuhusu wabunge 19 waliokuwa wanachama wa Chadema.

Sakata lenyewe lilianza na namna wabunge hao walivyoitwa bila kungazwa wazi na kuapishwa nje ya ukumbi wa Bunge, jambo liliobua mjadala mkali. Pamoja na utetezi uliotolewa na spika wakati huo, sasa ni jukumu la Spika Tulia kurekebisha mazingira hayo.

Dk Tulia amerithi sakata hilo kutoka kwa mtangulizi wake, Ndugai ambaye aliwahi kutangaza hawezi kuwafukuza, hivyo akaahidi kuwalinda.

Siku chache baada ya kuchaguliwa, Dk Tulia alipozungumza na waandishi wa habari alieleza kuwatambua wabunge hao hadi Chademakitakapopeleka barua ya kuonyesha wamepoteza uanachama wao.

Tayari Spika ambaye pia ni mbunge wa Mbeya amepokea barua ya Chadema huku akiwa tayari amepata taarifa kuwa wabunge hao wamefungua shauri mahakamani kupinga uamuzi wa kufukuzwa uanachama, hivyo naye anasubiri uamuzi wa mahakama.

Swali dogo linakuja kupitia majibu ya Dk Tulia, je, kama Bunge pia huongozwa na maamuzi yake ya nyuma, kwanini hakuona umuhimu wa kutumia uamuzi wa waliokua wabunge wa CUF ambao Bunge lilibariki kutumuliwa kwao bila kusubiri uamuzi wa mahakama.

Kwa mtihani huu itabidi Spika awe na kifua kipana kuhimili kejeli, vijembe na kuzodolewa ambavyo vitakuwa sehemu ya maisha ya kila siku katika shughuli za siasa.

Yeye amehitimisha suala hilo akisema yeye ndiye msemaji pekee wa jambo hilo. Kauli hii inaonyesha mtihani huo kwake kama umevuja akayaelewa maswali au mwalimu ametunga mtihani kwenye maeneo ambayo alikuwa ameyapitia vizuri.


Maoni ya wadau

Mbunge wa zamani wa Chilonwa, Joel Mwaka alisema Spika anatakiwa kufuata kanuni na taratibu zinazotakiwa, ili kuepuka kuingia katika mtego wa wanasiasa.

Mwaka alisema pia anatakiwa kufuata Katiba ya nchi ambayo ndiyo inamuongoza na mambo mengine yaliyobaki anatakiwa kutumia busara zaidi.

Mzee Juma Ramadhan alisema hekima ya Spika inatakiwa kutangulia mbele ya kanuni za Bunge, ili kujitofautisha na mtangulizi wake ambaye aliingia kwenye migogoro na wabunge, huku nje ya Bunge wananchi wakimuona anabeba wasiobebeka.

Wakili Elias Machibya akizungumzia sakata la wabunge 19 alisema suala la wabunge hao linaweza kuchukua muda mrefu kwa kuwa kuwahi au kuchelewa kwake kunategemea limefungulia kwa mtindo upi, kwa hati ya dharura kwa marejeo.

Advertisement