Dk Tulia awataka Watanzania kutangaza utalii wa ndani
Muktasari:
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson amewataka Watanzania kuwa mstari wa mbele kutangaza utalii wa ndani na sio kuwaachia wageni kuja kuutangaza mlima Kilimanjaro.
Moshi. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson amewataka Watanzania kuwa mstari wa mbele kutangaza utalii wa ndani na sio kuwaachia wageni kuja kuutangaza mlima Kilimanjaro.
Amesema zaidi ya asilimia 94 ya wanaopanda mlima Kilimanjaro ni watalii kutoka nje za nchi huku Watanzania wakiwa ni asilimia 5 pekee.
Dk Tulia ameyasema hayo Disemba 5, 2021 wakati akiwaaga wapanda mlima 150 walioanza safari ya kupandisha bendera Mlima Kilimanjaro kuelekea siku ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara Desemba 9 mwaka huu.
Miongoni mwa makundi yaliyopanda mlima Kilimanjaro ni waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari, Makamishna wa Tanapa,Tawa, TFS, wananchi pamoja na baadhi ya taasisi mbalimbali.
"Wenzetu wa nje wanaopanda mlima Kilimanjaro ni zaidi ya asilimia 94 na sisi ni kama asilimia 5 hivi, hivyo sisi kama Watanzania ni lazima tuone huu mlima upo kwetu na sisi ndio tunatakiwa kuwashawishi watu wengine, hatuwezi kuwasubiri, sisi ndio tusubiri kuwashawishi,"
"Niwaombe Watanzania tuwe mabalozi wa kulinda na kuthamini hifadhi zetu, lazima hizi hifadhi zihifadhiwe, tuendelee kufanya haya mambo muwa endelevu tusiwasubiri wenzetu,"
Pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kuendelea kuchanja chanjo ya Uviko-19 ili Mataifa mengine yaweze kuendelee kuwa na imani na Tanzania.
"Ili wenzetu wawe na imani na sisi kupanda mlima ni muhimu tukatumia fursa ambayo Rais wetu mama Samia ametupa Watanzania, chanjo zote zipo kila mahali, tuchanje ili tuweze kushirikiana vizuri na wenzetu,"
Naye Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini Shirika la Hifadhi la Tanzania (Tanapa), Jenerali George Waitara amesema idadi ya waliopanda mlima huo imevunja rekodi ikilinganishwa na miaka mingine.
"Mwaka huu waliopanda mlima ni 150 na wamevunja rekodi, hivi inaonyesha ni kwa namna gani Watanzania tulivyohamasika kusherekea uhuru wetu, idadi kubwa kipindi kilichopita ilikuwa 92, naomba mwakani muendelee kwa wengi zaidi na ikiwezekana tumia njia zote za kupandia mlima Kilimanjaro," amesema Waitara