EAC yajivunia kuogezeka kwa biashara kati ya Tanzania na Kenya

Muktasari:

Wakati Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki akitimiza siku 100 tangu ameshika wadhifa huo amesema yapo mafanikio ya kujivunia katika kipindi kifupi ambayo ni ongezeko la biashara kati ya Kenya na Tanzania kupitia mpaka wa Namanga na mchakato wa ajira.

Arusha. Wakati Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki akitimiza siku 100 tangu ameshika wadhifa huo amesema yapo mafanikio ya kujivunia katika kipindi kifupi ambayo ni ongezeko la biashara kati ya Kenya na Tanzania kupitia mpaka wa Namanga na mchakato wa ajira.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika kwanjia ya mtandao jana alisema marais katika sita wanachama wa EAC wamemhakikishia ushirikiano mzuri ili malengo ya jumuiya hiyo yawanufaishe wananchi wa kawaida.

“Baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu nilienda kwenye nchi zote wanachama kuonana na Marais ili nipate busara zao, nakumbuka walichoniambia ni kuhakikisha jumuiya inakua taasisi imara ya kuwahudumia wananchi ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake,”alisema Dk Mathuki

Alisema katika mpaka wa Namanga shughuli za usafirishaji mizigo kutoka nchi mbili za Kenya na Tanzania  zimeongezeka karibu mara sita ya zilikuwepo awali ikielezwa sababu ni utashi wa kisiasa uliochangiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na mwenzake wa Kenya,Rais Uhuru Kenyatta.

Dk Mathuki ambaye alitoa hotuba yake iliyofatiliwa na watu mbalimbali ndani na nje ya eneo la Afrika Mashariki kwanjia mtandao alisema ziara alizozifanya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye jirani ambazo pia ni wanachama wa EAC zinalenga kuimarisha ujirani mwema na diplomasia ya kibiashara.

“Napenda kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanza vizuri majukumu kutembelea nchi za EAC kwa lengo la kuleta nchi zetu pamoja na tunamwomba aendelee kufanya hivyo kwasababu itafanya nchi hizi kujenga utamaduni wa kuimarisha udugu na kutatua changamoto zilizopo,” alisema Dk Mathuki.

Alisema mwelekeo wa serikali ya Rais Samia unalenga kukaribisha uwekezaji kutoka nchi wanachama wa EAC ambao utakua na faida kubwa zikiwemo ajira kwa vijana ambayo ni ajenda muhimu pia kuvutia uwekezaji hatua itakayokuza uchumi wa nchi na kanda ya EAC kwa pamoja.


Kuhusu biashara zinazofanywa miongoni mwa nchi za EAC alisema zipo chini ya asilimia 15 huku lengo la Sekretariati anayoiongoza zifikie kiwango cha asilimia 40 hatua itakayoimarisha jumuiya na kukuza uchumi kwa ujumla.


Dk Mathuki alisema kwa zaidi ya miaka minne jumuiya hiyo pamoja na taasisi zake hawakua wameajiri wafanyakazi hatua iliyochangia kuwa na watumishi wachache na kuzorotesha utendaji kazi jambo ambalo limepatiwa ufumbuzi kwa kuanza mchakato wa ajira utakaoziba nafasi zilizo wazi.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Miundombinu,Mhandisi Steven Mlote alisema ujenzi wa miundombinu ya barabara inayounganisha nchi wanachama inaendelea kwa kasi hatua itakayofungua shughuli za biashara kustawi .