Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ewura kurahisisha utoaji vibali kwa wawekezaji nishati safi ya kupikia

urugenzi Mkuu Ewura, Dk James Mwainyekule

Muktasari:

  • Ili kuhakikisha kuwa agenda ya Serikali na Bara la Afrika ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inatimia ifikapo mwaka 2032, Mamlaka ya udhibiti wa  huduma za nishati na maji (Ewura) imesema kuwa itahamasisha uwekezaji wa nishati safi ya kupikia hapa nchini.

Dodoma. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Mwainyekule amesema mamlaka hiyo itaibeba ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini kwa kuhakikisha wawekezaji kwenye sekta hiyo wanapata leseni na vibali kwa wakati, ili kuharakisha upatikanaji wake mjini na vijijini.

Dk Mwainyekule ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Machi 10, 2024 jijini Dodoma alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusu mchango wa Ewura katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanafikiwa ifikapo mwaka 2032.

Amesema Ewura ina wajibu wa kutekeleza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wanawake barani Afrika kutumia nishati safi ya kupikia inafikiwa kwa kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya nishati safi ya kupikia.

“Hili litawezekana kwa kuhakikisha tunatoa vibali na leseni kwa wawekezaji kwa wakati, ili waweze kuwekeza, pia tunaangalia suala la upatikanaji wa hizi nishati katika maeneo mbalimbali, kwa hiyo tunawahamasisha wawekezaji waongeze usambazaji hususani maeneo ya vijijini, ili nishati hiyo ipatikane maeneo mengi na kwa gharama nafuu,” amesema Dk Mwainyekule.

Amesema Ewura inazingatia masuala ya bei kwa kuangalia mwenendo wake katika nishati safi za kupikia pamoja na kutoa leseni kwa wakati, ili mwekezaji awekeze kwa wakati na wananchi wafikiwe na nishati hiyo.

“Tunaamini kama vile ambavyo Serikali imefanikiwa kwenye kumtua mama ndoo kichwani, pia na huko mbele tunakokwenda nafikiri tutafanikiwa kumtua mama kuni kichwani, ili apate nishati safi ya kupikia na atumie muda mwingi kwenye shughuli za maendeleo badala ya kuhangaika kusenya kuni,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati na Teknolojia Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Advera Mwijage amesema wakala huo umefunga majiko yanayotumia nishati safi ya gesi asilia kwenye magereza yaliyopo kwenye mikoa ya Pwani na Lindi, yenye thamani ya Sh13.5 bilioni ambayo yatanufaisha wafungwa 1,400.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Mwainyekule (wa pili kushoto) akizungumza na baadhi ya wananchi pamoja na wafanyakazi wa mamlaka hiyo kwenye banda la maonyesho la mamlaka hiyo kwenye kongamano la wanawake Jijini Dodoma.

Amesema wameanzisha mradi wa kuzalisha mkaa mbadala ambao utakuwa unatokana na takataka, ili kulinda mazingira yasiharibiwe. Ameongeza kuwa nishati chafu ya kupikia inayotokana na kuni kwenye taasisi za Serikali ambapo magereza hutumia asilimia 93 ya kuni, huku Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) likitumia asilimia 84 ya kuni kama nishati ya kupikia.

Mmoja wa mama lishe kutoka mkoani Kilimanjaro, Romana Maswai amesema wamelipokea suala la kutumia nishati safi ya kupikia kwa mikono miwili, lakini bei ya gesi bado iko juu, hivyo ameiomba Serikali kuangalia upya bei ya nishati hiyo.

Amesema mtungi mdogo wa gesi wa kilo sita wananunua kwa Sh22,000 na kuomba bei ipunguzwe, ili waweze kumudu gharama ya nishati ya gesi.