Ewura yaonya vishoka mifumo ya umeme

Meneja wa mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na na Ewura kanda ya kaskazini, Mhandisi Loripi Long'idu akizungumza na wanafunzi wa chuo cha ufundi stadi (Veta) mjini Babati mkoani Manyara wa fani ya ufundi mchundo juu ya umuhimu wa kuwa na leseni ili kupunguza wimbi la wasio na leseni mitaani (vishoka). Picha na Joseph Lyimo.


Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) yatakata mafundi wa mifumo ya umeme majumbani, kuwa na leseni, kwani kufanya kazi bila kibali hicho ni kosa kisheria na kwamba ili kuipata, wanahitajika kupata mafunzo kupitia vyuo vya ufundi Veta.

Babati. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) yawatakata mafundi wa mifumo ya umeme majumbani, kuwa na leseni, kwani kufanya kazi bila kibali hicho ni kosa kisheria na kwamba ili kuipata, wanahitajika kupata mafunzo kupitia vyuo vya ufundi Veta.

Hayo yamebainishwa leo Juni 7, 2023 na Mhandisi Mwandamizi Umeme Ewura Kanda ya Kaskazini, Tegemeo Kamando wakati wa utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi wa fani ya ufundi mchundo chuo Veta, wakati akibainisha umuhimu wa kuwa na leseni na hivyo kupunguza wimbi la vishoka (wasio na leseni) mtaani.

Kamando amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi kwa mafundi wenzao na kuacha tabia ya kutegemea leseni ya mwingine ili kupitishia kazi zake.

“Ni kosa kisheria kufanya kazi za ufungaji wa mifumo ya umeme bila kuwa na leseni inayotolewa na Ewura…takwa la kisheria kifungu cha tano cha sheria ya umeme sura 131 kinaipa Ewura mamlaka ya kutoa leseni kwa huduma mbalimbali katika sekta ya umeme,” amesema na kuongeza;

“…kifungu cha nane (a) kipengele cha kwanza na cha pili (h) cha sheria ya umeme ya mwaka 2008 kinaipa Ewura mamlaka ya kutoa leseni kwa mafundi umeme wote wa Tanzania bara.”

Awali, Meneja Ewura kanda ya Kaskazini, Loripi Long'idu amesema Serikali kupitia mamlaka hiyo imeanza kutekeleza mpango wa kutoa mafunzo ya umuhimu wa mafundi mchundo kuwa na leseni ya umeme huku pia ikionya wananchi wanaoendelea kutumia mafundi umeme wasio na leseni zinazotolewa na Ewura.

"Lengo ni kuhakikisha kazi za umeme zinafanywa na watu ambao ni wataalam waliosoma maana hao ndiyo wanaweza kufanya kazi kwa kuzingatia viwango vya ubora wa kazi hali itayopelekea kupunguza maafa yanayoweza kutokea kutokana na majanga ya moto ambayo husababisha upotevu wa uhai na mali," amesema Long'idu.

Hivyo basi, bosi huyo wa Ewura kanda hiyo amesema: “Niwatake nyie vishoka mkijiona mnachangamoto fikeni vyuo vya veta, vina utaratibu wa kuwarasimisha. Kama wewe ni kishoka na kwamba kupitia njia ya saidia fundi, umeweza kujua taratibu za kufunga mifumo ya umeme, sasa ili kuwa rasmi fika veta ili kupata mafunzo ya muda mfupi.”

Long’idu ameeleza kuwa baada ya mafunzo hayo, mhitimu atapewa cheti ambacho kitamsadia kupata leseni kutoka Ewura na hivyo kufanya kazi ya fundi umeme bila kuwa na wasiwasi wowote kwani anatambuliwa rasmi.

Kwa upande mwingine meneja huyo ameionya jamii kutokiuka sheria kwa kutumia vishoka katika ufungaji wa mifumo ya nishati ya umeme kwani ni kati ya vyanzo vinavyosababisha majanga mbalimbali ya moto maeoneo ya makazi, sokoni, viwanda na kwingineko.

Mwanafunzi wa ufundi Mchundo Shufani Hemed amesema fani hiyo imekuwa ni fursa kwa vijana wengi ambao walikuwa mtaani na kuamua kujiunga na watapomaliza watahakikisha wanapata leseni ili waweze kujiamini wanapokuwa kazini na kupunguza wimbi la vishoka.