Ewura kuamua bei ya umeme

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Maharage Chande amesema siyo busara kushusha umeme baada ya mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), badala yake uwekezaji zaidi ufanyike ili wananchi wengi wapate huduma ya umeme.

Chande alibainisha hayo wakati kukiwa na matarajio ya watu wengi kuwa huenda umeme ukashuka bei baada ya kuanza kwa uzalishaji wa bwawa hilo.

Kauli hiyo aliitoa juzi jijini hapa, wakati wa mkutano kati ya Tanesco na wahariri wa vyombo vya habari, huku akisema suala la bei hata hivyo, limo ndani ya uwezo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Mkurugenzi huyo alieleza hayo wakati akijibu swali kuhusu mradi wa JNHPP ukikamilika kama bei ya umeme itashuka ili wananchi wapate umeme kwa bei ya chini.

 Chande alifafanua kwamba kuna bei na gharama, hayo ni mambo mawili tofauti. Alisema ukizalisha umeme kwa kutumia maji, gharama za uzalishaji zinakuwa chini, lakini kwa sekta ilipo, yeye hadhani kama ni busara kushusha bei kwa sababu watashindwa kuwekeza.

“Sasa wewe leo umepata mradi wa Mwalimu Nyerere, umepata gharama ya kuzalisha imeshuka, ndiyo unashusha na bei wakati hata miundombinu hujamaliza kujenga, ni sawasawa unafanya kazi, umeongezwa mshahara, unataka uzitumie hadi ziishe. Si unatakiwa ubane, ili uwekeze kwenye maendeleo zaidi.

Alisema hapa nchini, masuala ya bei yanashughulikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na kwamba hivi karibuni watakwenda kuzungumza nao kuhusu hilo.

“Mimi kwa busara, sidhani kama ni vizuri tukapunguza bei ya umeme ili pesa tutakayobaki nayo sisi iongezeke kupanua miundombinu,” alisisitiza mkurugenzi huyo.

Aliongeza: “Mwaka huu wa fedha kwa mfano, Tanesco kwa pesa zetu wenyewe, karibu Sh700 bilioni zitatumika kufanya extension (upanuzi)…wangine kule hawaunganishwi kwa sababu miundombinu haijafika na fedha za kuifikisha miundombinu hiyo hazipo.

“Sasa ukipata Mwalimu Nyerere, umepunguza gharama za kuzalisha, albaki (salio) yako kubwa, unasema nipunguze nizidi kurudi nyuma. Busara ya kawaida, ni ghafla albaki imepungua, uongeze kasi ya kupanua miundombinu ili wateja wengi wapate umeme.

“Kwa hiyo, ninasema tutofautishe bei na gharama, ni vitu viwili tofauti. Gharama zitashuka lakini ama ushushe bei au usishushe, ni uamuzi wa kimkakati. Kama unataka ubaki hapohapo usikue, shusha bei, unabaki hivi hivi, hamna umeme huku hamna umeme huku. Lakini ukitaka kukua usishushe bei, albaki iwe kubwa, utanuke zaidi”.


Matarajio ya JNHPP kushusha bei ya umeme

Julai 26, 2019, wakati akizindua mradi wa ujenzi wa bwawa hilo, Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alibainisha viwango vya gharama za umeme kulingana na vyanzo vinavyotumika kuuzalisha.

Alisema gharama za umeme unaozalishwa kwa maji ni Sh36 kwa uniti moja, jua ni Sh114.2, gesi ni Sh118, joto ardhi ni Sh114.2 na unaozalishwa kwa mafuta ni Sh547.

Wakati huo, Serikali ilieleza manufaa ya mradi ni pamoja na kushuka kwa bei ya umeme kwa wananchi kwa sababu Tanzania itakuwa ikizalisha umeme wa kutosha na ziada kuuzwa nje ya nchi.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude aliunga mkono hoja ya Chande, akieleza kwamba wakati wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma, Tanesco ilikuwa kwenye orodha hiyo, waliweza kuzuia isiuzwe, lakini hawakufanya uwekezaji wowote kwa kipindi kirefu.

Alisema bei ya umeme ya sasa nchini iko chini ya bei ya soko, kwa sababu ina ruzuku ndani yake, ilitakiwa iwe kubwa zaidi. Alisisitiza kwamba kukamilika kwa mradi wa umeme wa JNHPP hakuwezi kushusha bei ya umeme.

“Tanesco ina kazi tatu; ina kazi ya kuzalisha umeme, kusambaza na kuunganisha, zote ni kazi ambazo zinagharimu fedha nyingi, fedha hizo anazitoa kwenye tozo zake tu. Uwekezaji kule Stiglers ni mkubwa sana na ni mkopo, itabidi ulipwe, hiyo fedha inatoka wapi?” alihoji.

Alisema ili bei ya umeme ishuke, Serikali inatakiwa kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme kama vile upepo na jua.