Tanesco kusaini mkataba wa uzalishaji umeme

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande akizungumza katika moja ya tukio ya shirika hilo. Picha na Mtandao

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande amesema Jumatatu ijayo watasaini mkataba wa uzalishaji wa umeme megawati 50 kaskazini na kwamba tayari mkandarasi amepatikana.

Chande amebainisha hayo leo Mei 26, 2023 wakati wa majadiliano maalumu kati ya Tanesco na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Amesema vituo vya kuzalisha umeme vya kaskazini magharibi vinazalisha megawati 221, kiwango ambacho kinasaidia wakazi wa eneo hilo.

"Tuna mpango hadi ya mwaka 2035, mradi wa Julius Nyerere naona unaoanza kuzalisha umeme Juni mwaka huu utatufikisha mbali," amesema Chande.

Amesema katika idadi ya watu milioni 61, familia za watu milioni 12 zinatumia takribani megawati 2100 na kwamba umeme kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere likianza kuzalisha watakidhi mahitaji ya umeme.

"Kutokana na shughuli za kiuchumi kuongezeka, mahitaji ya pia umeme yameongezeka. Tunajitahidi kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji," amesema Chande.