PIC yaipongeza Serikali uwekezaji umeme kigoma
Muktasari:
- Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imetembelea mashine za uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta katika kituo cha cha Bangwe na kujionea ujenzi wa njia ya umeme mkubwa wa kilovolt 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma.
Kigoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imeipongeza Serikali kwa uwekezaji wa miradi ya umeme wa gridi ya Taifa mkoani Kigoma, kupitia Shirika la Umeme (Tanesco).
Pongezi hizo zimetolewa jana Machi 20 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Jerry Slaa kwa niaba ya kamati hiyo, wakati wa ziara ya kukagua mashine za uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta katika kituo cha cha Bangwe mkoani zitakazozalisha jumla ya megawati 8.75.
Slaa amesema Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika kupitia ujenzi wa miundombinu, ikiwemo ujenzi wa njia ya umeme mkubwa wa kilovolt 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma.
"Uzalishaji wa umeme kwa mafuta ni dola senti 25 kwa uniti, uzalishaji wa maji ni dola senti 5, umeme wa jua dola senti 4 na wa gesi ni dola senti 7 kwa uniti moja, hivyo tunaona kabisa uzalishaji wa mafuta unavyougharimu Serikali," amesema Slaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande amesema kuwa mradi umekamilika kwa asilimia 47 na juhudi zinafanyika kukamilisha kuhakikisha Mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani yanapata Umeme wa kutosha.
“Mradi huu utakapokamilika tutazalisha umeme wa kutosha kuwasha Kigoma na kuweza kufanya biashara ya kuuza umeme nchi za jirani," ameongeza Chande.