Vyura wa Kihansi kurudishwa nchini Julai

Chura wa Kihansi ambao kitaalamu hufahamika kama ‘Nectophrynoides asperginis’

Muktasari:

  • Tangu vyura 500 wapelekwe Marekani mpaka sasa, Tanesco imetumia zaidi ya Sh900 milioni kuwatunza huku asilimia kubwa ya gharama zikitolewa kwa ufadhili.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande amesema vyura wa Kihansi wanaohifadhiwa nchini Marekani wataanza kurejeshwa nchini Julai 2023.

Chande amebainisha hayo leo Ijumaa Mei 26, 2023 wakati akijibu swali la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Deodatus Balile aliyetaka kufahamu vyura hao wataendelea kuhifadhiwa hadi lini.

Chande amesema unapojenga miradi mikubwa lazima kuwa na mipango ya kuhifadhi ikolojia. Amesema mzunguko wa ikolojia ni miaka 20, na miaka hiyo ilitimia wakati wa kipindi cha Uviko-19, jambo ambalo lilikwamisha vyura hao kurejeshwa nchini.

"Wakati tunawapeleka vyura hao Marekani, nchi yetu ilikuwa haina maabara. Tulishindwa kuwarudisha mwaka 2021 kwa sababu ya Uviko-19. Lakini niwahakikishie kwamba Julai mwaka huu wanaanza kurudi nchini," amesema Chande.

Ameongeza kwamba uamuzi wa kuwahifadhi vyura hao ulikuwa wa faida na kwamba katika kipindi chote walichohifadhiwa, nchi imepata faida.

"Tulipeleka vyura 500, wamezaliana na kuongezeka zaidi. Na vyura hawa wako Kihansi tu, hawapatikani mahali pengine," amesema mkurugenzi huyo wa Tanesco.

Uamuzi wa kupeleka vyura hao Marekani ulifanywa na Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2000, waziri akiwa Abdallah Kigoda na Rais alikuwa Benjamin Mkapa (wote marehemu).

Tangu vyura 500 wapelekwe Marekani mpaka sasa, Tanesco imetumia zaidi ya Sh900 milioni kuwatunza huku asilimia kubwa ya gharama zikitolewa kwa ufadhili.

Tangu mwaka 2000 mpaka June 2019, gharama za matunzo ya vyura hao zililipwa na Benki ya Dunia (WB) na Global Environment Facility ili kutoa fursa ya mradi wa umeme kutekelezwa.

Mwishoni mwa mwaka 2020 Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli wakati huo Wizara ya Nishati ikiongozwa na Dk Medard Kalemani, ilihuisha mkataba wa kuendelea kutunzwa kwa vyura hao waliofikia 6,000.