Siri vyura wa Kihansi kutunzwa Marekani

Muktasari:

Tangu kuanzishwa kwa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Kihansi mwaka 2000, kiasi cha kwh bilioni 17.2 ambazo thamani yake ni Sh3.4 trilioni kilizalishwa huku gharama zilizotumika kwa miaka yote 22 kuwatunza vyura hao ikiwa ni Sh6.7 bilioni.

Dar es Salaam. Miongoni mwa habari zilizozua gumzo hivi karibuni ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutumia Sh611.92 milioni kutunza vyura wa Kihansi huko Marekani, gazeti hili limefanya uchambuzi, kukusanya maoni na taarifa muhimu zinazopaswa kufahamika na umma kuhusu viumbe hao wanaopatikana Tanzania pekee.

Mjadala wa vyura wa Kihansi ulianza baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kueleza vyura hao wanatunzwa kwa mamilioni hayo ya shilingi, baadhi ya watu walikwenda mbali zaidi na kutumia taarifa hiyo kwa maudhui ya utani (memes), lakini uhalisia na faida ni zaidi ya kile unachokifahamu.

Uamuzi wa kupeleka vyura hao Marekani ulifanywa na Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2000, waziri akiwa Abdallah Kigoda na Rais alikuwa Benjamin Mkapa (wote marehemu).

Tangu vyura 500 wapelekwa Marekani mpaka sasa, Tanesco imetumia zaidi ya Sh900 milioni kuwatunza huku asilimia kubwa ya gharama zikitolewa kwa ufadhili.

Tangu mwaka 2000 mpaka June 2019, gharama za matunzo ya vyura hao zililipwa na Benki ya Dunia (WB) na Global Environment Facility ili kutoa fursa ya mradi wa umeme kutekelezwa.

Mwishoni mwa mwaka 2020 Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli wakati huo Wizara ya Nishati ikiongozwa na Dk Medard Kalemani, ilihuisha mkataba wa kuendelea kutunzwa kwa vyura hao waliofikia 6,000.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande vyura hao walipaswa kurejeshwa nchini mwaka 2019, lakini sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko – 19, ilishindika hivyo Serikali ikaongeza mkataba wa miaka miwili kuwahifadhi.

“Mkataba huo uliisha Juni 2022 na Desemba 2022, makubaliano yalifikiwa ya kuanza kuwarudisha. Tangu hapo, Wizara ya Nishati chini ya Waziri January Makamba haijalipia tena utunzaji wa vyura hawa walioko Marekani. Mpango wa Serikali ni kuwarudisha nchini na wataishi kwenye vituo mahususi vilivyotengwa (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-UDSM na Kihansi kuanzia Aprili mwaka huu,” amesema Chande na kuongeza kuwa hadi kufikia Julai 2023 vyura wote watakuwa wamerejeshwa nchini na kuwaweka katika maeneo yao ya asili na yale yaliyotengenezwa.

Mwananchi lilipomtafuta Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa ili kujua iwapo Serikali ina mpango wa kurejeshwa kwa vyura hao ili kuwahifadhi nchini, amesema  ndani ya wiki mbili kuanzia sasa, watalijadili jambo hilo na taarifa itatolewa.

“Ndani ya wiki hizi mbili tunatarajia kukaa tutajadili mambo yote na hoja zote zilizoibuliwa ambazo zinatugusa. Suala la vyura hao ni la kisayansi maana niliambiwa pale kwenye mradi walikuwa wanakufa, lakini baada ya majadiliano tutapata majibu na kutoa taarifa,” amesema Waziri Mchengerwa aliyekabidhiwa wizara hiyo takribani miezi miwili iliyopita.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka amesema suala la utunzaji wa vyura hao ni jambo moja tu kati ya mengi yaliyofanywa katika kuhifadhi asili ya eneo hilo ambalo mradi wa kufua umeme ulitekelezwa.

Amesema katika utekelezaji wa mradi ule, hatua nyingi za utunzaji wa mazingira zilichukuliwa, hilo la kutunza vyura ni moja tu. Taasisi za za Serikali, zisizo za kiserikali kwa pamoja zilichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ikolojia ya eneo hilo haiathiriki ndiyo maana maabara nyingi zilianzishwa. Pia wananchi wa maeneo ya karibu walipewa elimu.

“Viumbe wote wana umuhimu wao katika ikolojia na mambo mengi yapo kama yalivyo sababu ya uwepo wa viumbe hao na wale vyura ni wa kipekee. Hawatagi mayai kama wengine wao hubeba mimba na kuzaa. Hawakuonekana kabla walikuja kuonekana baada ya mradi kuanza ndiyo maana hatua za makusudi zikachukuliwa kuwalinda,” amesema Gwamaka.

Amesema ukiachilia mbali Marekani, hapa nchini kuna maabara za kuzalisha na kutibu vyura hao akitolea mfano maabara iliyopo katika ofisi za Tanesco Kihansi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na baada ya vyura hao kukua hurejeshwa katika maeneo yao ya asili.

“Pale Kihansi kuna vitu vingi vya kipekee, vipepeo na hata kahawa pori ambayo ina caffeine ya asilimia sita ambayo ni tofauti na kahawa nyingine pengine mimea na viumbe wengine wa eneo lile wapo kama walivyo sababu ya uwepo wa hao vyura,” amesema Gwamaka.

Mtaalamu wa uhifadhi, Dk Felician Kilahama amesema uamuzi wowote wa kuhakikisha viumbe hao adimu duniani hawapotei na wanapatikana siku zote kwa faida ya vizazi vyote vilivyopo na vitakavyokuja ni jambo la msingi.

“Faida moja kubwa kwetu ni kutokana na vyura hivyo, kuwepo Jumuiya za kimataifa zinakuwa bega kwa bega nasi kuhakikisha rasilimali hiyo pekee duniani inalindwa kwa faida ya wote,” alisema Kilahama ambaye ni Mkurugenzi mstaafu wa Misitu na Nyuki.

Amesema vyura hao ni wa kipekee, kwani wanaishi kwenye mazingira yanayotoa ‘mvuke usiku na mchana, hawana umbo kubwa lakini wanazaa viumbe hai hawatagi mayai, hivyo ni kivutio cha utalii ikolojia.

“Uwezo wa kuwatunza tunao na kama uwezo huwa haupo unajengwa. Hawa walipelekwa Marekani ambako wametengeneza masingira na asili kama ya Kihansi,” amesema Dk Kilahama.

Kwa nini vyura wa Kihansi

Vyura hawa ambao wanapatikana Tanzania pekee waligunduliwa na kutangazwa mwaka 1996 baada ya kuanza kwa ujenzi wa Bwawa la Kihansi.

Kabla ya hapo vyura hawa hawakuwahi kuonekana duniani, maisha yao yanategemea mvuke unaotokana na maporomoko ya maji. Kutekelezwa kwa mradi wa umeme katika eneo hilo uliwaathiri sana hivyo, Serikali kufikia uamuzi wa kuwatunza nchini Marekani.

Taarifa zilizopo zinaonyesha ujenzi wa Bwawa la Kihansi ukachukua asilimia 90 ya maji yaliyokuwa yanapita ndani ya makazi ya vyura hivyo wakaanza kufa na kutozaliana, idadi yao ikapungua kutoka takriban vyura 20,000 wakati wanagunduliwa.

“Wafadhili wa mradi wetu wa Kihansi, Benki ya Dunia, Serikali ya Sweden na Norway walitoa masharti ya kufadhili mradi huo ni kuhakikisha vyura hao hawapotei na kama sivyo wanajitoa katika mradi huo. Njia pekee ilikuwa ni kukubali kuwatunza na kupata mradi ambao kwa sasa manufaa yake yanaonekana kwenye uzalishaji wa umeme nchini,” amesema Chande.

Mwaka 2000 kabla vyura hawa hawajapotea kabisa mpango wa kuwaokoa ulianzishwa na vyura 500 wakapelekwa Marekani kwenye bustani za wanyama za Bronx na Toledo zenye utaalamu na miundombinu bora ya kuwatunza vyura hao wasipotee kabisa duniani.

Mpaka kufikia mwaka 2010 idadi ya vyura hawa kwenye bustani hizo zilizopo nchini Marekani ilikadiriwa kufika 6,000.

Mwaka huo pia vituo viwili vya kuzalisha vyura hao vilianzishwa Tanzania (UDSM na moja Kihansi), majaribio ya kuwarudisha yaliwahi kufanyika miaka ya nyuma, lakini hayakufanikiwa (vyura walikufa kutoka na mabadiliko ya mazingira).

Bwawa la Kihansi lilianza kuzalisha umeme mwaka 2000 na linachangia megawati 180 kwenye gridi ya Taifa.