Exim yaandaa hafla ya futari Dodoma na Tanga, viongozi wa dini, serikali waguswa

Maofisa wa Benki ya Exim Tanzania akiwemo Mkuu wa  kitengo cha Hazina na Masoko  ya Dunia, Nelson Kishanda (katikati) wakikabidhi msaada wa chakula na mahitaji muhimu kwa mmoja wa wananchi wenye uhitaji jijini Tanga. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa (wa tatu kushoto) na  Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tanga Sheikh Juma Luwuchu (kushoto)


Benki ya Exim Tanzania imehitimisha rasmi zoezi la uandaaji wa futari kwa wateja wake katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma na Tanga kwa msimu huu wa mwezi wa Mtukufu wa Ramadhani huku wadau mbalimbali wa benki hiyo wakiwemo wateja, viongozi wa dini na serikali wakionyesha kuridhishwa na utaratibu wa benki hiyo wa kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum katika mwezi huo.

Katika kuhitimisha zoezi hilo ilishuhudiwa viongozi waandamizi wa serikali na dini katika mikoa ya Tanga na Dodoma wakishirikiana na viongozi waandamizi wa benki hiyo akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Jaffari Matundu pamoja na Mkuu wa Rasilimali watu wa benki hiyo Fredrick Kanga katika kuongoza hafla mbili tofauti zilizoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wenye imani ya Kiislam  katika mikoa hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Sambamba na hafla hizo benki hiyo pia kupitia Mkuu wake wa  kitengo cha Hazina na Masoko  ya Dunia Nelson Kishanda pamoja na baadhi ya wateja wake iliweza kukabidhi msaada wa chakula na mahitaji muhimu kwa  familia zenye uhitaji kupitia  taasisi ya Maawal Islamic ya jijini Tanga, shughuli ambayo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa aliyemuwakilisha Mkuu wa mkoa huo, sambamba na Sheikh Mkuu wa Mkoa  huo Sheikh Juma Luwuchu.

Wakizungumza kwenye matukio yote mawili ya jijini Tanga DC Mgandilwa pamoja nae Sheikh Luwuchu walionyesha kufuruhaishwa na mtazamo wa benki hiyo wa kutokutazama mwezi wa Ramadhani kama ni mwezi wa kujenga mahusiano na wateja wao pekee bali pia kuutumia vyema mwezi huo kwa kuyakumbuka makundi yenye uhitaji bila kujali kama si wateja wa benki hiyo.

“Hiki kinachofanywa na benki ya Exim ni mfano haswa wa kuigwa. Wangeweza tu kukutana na wateja wao na kufuturu pamoja lakini wameona kitendo hicho pekee hakitoshi kuuheshimisha mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani hivyo wameona ni vema wawakumbuke pia wenye uhitaji maalum. Kupitia Taasisi ya Maawal Islamic wameweza kukabidhi futari kwa watu wenye uhitaji… hongereni sana,’’ alipongeza DC Mgandilwa.

Akizungumzia matukio hayo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu alisema ni muendelezo wa utaratibu wa benki hiyo kwa zaidi ya10 miaka sasa ikilenga kujumuika na wateja wake kama hatua ya kuonyesha mshikamano na umoja katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake jijini Tanga

Alisema benki hiyo inaheshimu sana Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutokana na ukweli kwamba, ni kipindi ambacho mwanadamu anajiweka karibu na Muumba wake kupitia mfungo na kufanya maombi.

“Kwetu sisi mwezi huu tunautazama kiimani zaidi ndio sababu tunazama makundi yote wakiwemo wateja wetu pamoja na watu wenye uhitaji maalum. Tumeweza kuandaa matukio kama haya mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Zanzibar na leo tunakamilisha na mikoa ya Tanga na Dodoma.’’

“Zaidi tutaendelea kutoa zawadi za Sikukuu ya Eid al-Fitr katika maeneo mengine pia. Lengo ni wote tufurahie mwezi huu muhimu huku pia tukikumbushana kufanya kilicho chema mbele za Mungu wetu,” alisema Matundu.

Hafla zote mbili zilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wateja, mawakala pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.