Facebook kuanza kulipa vyombo vya habari

Facebook kuanza kulipa vyombo vya habari

Muktasari:

  • Facebook imesema leo kuwa imefikia makubaliano na baadhi ya magazeti ya Ufaransa kuwa itaanza kulipia habari zao zinazowekwa katika tovuti zao na ambazo watumiaji watashirikisha wengine (share), ikiwa ni miezi kadhaa baada ya Google kutangaza kuwa italipia habari zilizo kwenye tovuti kila zitakapotafutwa (search).

Paris, Ufaransa (AFP). Facebook imesema leo kuwa imefikia makubaliano na baadhi ya magazeti ya Ufaransa kuwa itaanza kulipia habari zao zinazowekwa katika tovuti zao na ambazo watumiaji watashirikisha wengine (share), ikiwa ni miezi kadhaa baada ya Google kutangaza kuwa italipia habari zilizo kwenye tovuti kila zitakapotafutwa (search).

Facebook imesema makubaliano ya leseni pamoja na APIG, umoja wa magazeti ya taifa na ya kikanda, "yanamaanisha Facebook itakuwa na uwezo wa kupandisha na kushirikisha (share) habari miongoni mwa jamii, huku pia ikihakikisha kuwa hakimiliki za wachapishaji zinalindwa".

Vyombo vya habari, ambavyo vinakabiliana na kuporomoka kwa mauzo ya magazeti, kwa muda mrefu vimekuwa vikichukizwa na kitendo cha Google kushindwa kutoa sehemu ya mamilioni ya fedha inazopata katika matangazo yanayowekwa katika habari.

Mwezi Januari, Google ilisema imefikia makubaliano na APIG kulipia kwa wachapishaji baadhi ya maudhui yanayoonekana wakati watumiaji wakisaka habari (search).

Mpango huo unaonekana kuwa ni ushindi katika vita ya Ufaransa kulinda haki za uchapishaji kwa vyombo na mashirika ya habari.

Ufaransa ilikuwa nchi ya kwanza katika Umoja wa Ulaya (EU) kupitisha sheria mwaka 2019 kuhusu haki shiriki, lakini awali Google haikukubaliana nayo, ikisema vyombo vya habari tayari vinanufaika na watumiaji wanaotembelea tovuti zao.

Facebook imesema, mbali na kulipia habari, pia itaanzisha huduma ya habari kwa Kifaransa mwezi Januari "kuwapa watu nafasi ya kufikia maudhui kutoka vyanzo vya habari vinavyoaminika".