Fadhila na adabu za kumtembelea mgonjwa
Muktasari:
- Ni vema mtu akachagua muda unaofaa wa kumtembelea mgonjwa, na wala asimtembelee wakati ambao unamletea uzito.
Dar es Salaam. Hakika kumtembelea mgonjwa ni katika adabu zilizo tukufu ambazo Uislamu umehimiza Waislamu kuzizingatia, na umezifanya kuwa miongoni mwa haki muhimu za Muislamu juu ya ndugu yake Muislamu.
Pia ni katika njia za kuleta upendo baina ya waja. Allah Mtukufu amesema: “Na shikamaneni na kamba ya Allah nyote pamoja, wala msifarakane..” (3:103) Kumtembelea mgonjwa humfanya ajisikie roho ya udugu wa Kiislamu wakati wa maradhi yake, na hilo huwa sababu ya kupunguza maumivu na huzuni zake, na kumfidia baadhi ya yale aliyoyakosa ya nguvu na afya.
Katika adabu za wema waliotangulia (Allah awaridhie), kwamba wakikosa kumuona mmoja wa ndugu zao walikuwa wakimuulizia; akiwa safarini walimwombea dua na kuingalia familia yake, akiwa yupo walimtembelea, na akiwa mgonjwa walimzuru.
Ibn Hazm (Allah amrehemu) ameuelezea ugojwa kuwa ni kila kinachomtoa mwanadamu katika nguvu na uwezo wa kufanya mambo.
Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa kumtembelea mgonjwa ni wajibu kifaya, yaani ambao ukifanywa na baadhi ya watu hutosheleza kwa wengine.
Hoja yao ni kauli ya Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake): “Walisheni wenye njaa, watembeleeni wagonjwa, na muwakomboe mateka.” Wanazuoni wamejengea hoja hadithi hii kuwa kumtembelea mgonjwa kunahusika kwa kila mgonjwa; awe mwanaume au mwanamke, mkubwa au mdogo, Muislamu au asiye Muislamu, bila kujali aina ya ugonjwa wake.
Ama Jopo la wanazuoni (Aljumhur) wamesema kumtembelea mgonjwa ni jambo la kupendeza (sunna) iwe ni kwa anayemjua au asiyemjua, awe ni ndugu au asiye ndugu.
Hitimisho lenye nguvu (rajihi) suala la kumtembelea mgonjwa, linaweza kuwa wajibu kwa baadhi ya watu kama jamaa, ndugu na majirani, na kuwa sunna kwa wengine.
Ni vema mtu akachagua muda unaofaa wa kumtembelea mgonjwa, na wala asimtembelee wakati ambao unamletea uzito mgonjwa.
Ni sunna kumfariji mgonjwa na kumkumbusha hekima ya Allah kwamba ugonjwa unafuta madhambi kwa kumwambia: “Laa ba’sa Twahuur Inshaallah” yaani: “Hakuna ubaya, ni utakaso kwa idhini ya Allah.”
Hii ni kwa sababu ugonjwa unafuta dhambi. Mtume wa Allah amesema: “Haumpati Muislamu uchovu, wala ugonjwa, wala huzuni, wala maumivu, wala dhiki, hata mwiba unaomchoma, isipokuwa Allah humfutia kwa hayo baadhi ya madhambi yake.”
Kadhalika, ni sunna kumuuliza mgonjwa hali yake ili kumfariji. Ikiwa mgonjwa hawezi kuzungumza, basi anayemtembelea anaweza kuwauliza watu wake kuhusu hali yake.
Ni wajibu kwa anayemtembelea mgonjwa kumkumbusha matokeo mazuri ya subira na kumhimiza kuridhia, na kumsomea aya na hadithi zinazomtuliza moyo na kuondoa huzuni yake.
Aidha, amjulishe kuwa Allah anawapenda wenye subira. Kadhalika amkumbushe hadithi ya Mtume wa Allah “Ukubwa wa malipo huambatana na ukubwa wa mtihani,...” Na amkumbushe mgonjwa kuwa kulalamika na kulaani ugonjwa hakuondoi ugonjwa, bali humfanya apoteze malipo na huenda akapata dhambi.
Vile vile amkataze mgonjwa kutamani kifo. Kadhalika, aisihi familia yake wawe na subira katika kumhudumia na wamtendee wema mgonjwa; kwa sababu mara nyingine watu wa karibu wa mgonjwa, wanaweza kumchoka au kumuona mzigo, hasa ugonjwa unapochukua muda mrefu au kuwa mkali na kuwachosha katika kumhudumia.
Pia ni sunna kwa anayemtembelea mgonjwa kumwombea dua na kumfanyia ruqya (dua za tiba). Mtume wa Allah alipomtembelea mgonjwa alikuwa akisema: “Ewe Mola wa watu! Ondoa maradhi, mpe shifa, Wewe ndiye Mponyaji, hakuna uponyaji ila uponyaji wako, uponyaji usioacha ugonjwa wowote.”
Ni sunna kumsomea dua: “Kwa jina la Allah nakusomea ruqya, kutokana na kila kinachokuumiza, kutokana na shari ya kila nafsi au jicho la mwenye husuda. Allah akuponye...”
Kadhalika dua: “Najilinda kwa maneno kamili ya Allah dhidi ya kila shetani, kila kiumbe chenye sumu, na kila jicho baya.” Kisomo cha Ruqya kinaruhusiwa alimradi kisiwe na ushirikina ndani yake.
Inaruhusiwa kumtafutia mgonjwa daktari. Na inapowezekana mwanamume atibiwe na daktari mwanaume, mwanamke atibiwe na daktari mwanamke. Lakini kwa dharura, inaruhusiwa kinyume chake.
Ni sunna kutoa sadaka kwa ajili ya kuomba uponyaji: Mtume wa Allah amesema: “Waponyeni wagonjwa wenu kwa sadaka.” Aidha, ni sunna kumtamkisha Shahada anapokaribia kufa. Mtume amesema: “Wafundisheni waliokaribia kufa kusema: Laa ilaaha illa Allah” Hii hufanywa kwa mwenye fahamu na anayeweza kuzungumza. Akishatamka, usirudie mara kwa mara ili asichoke au kukerwa.
Kutozidisha muda wa ziara, baadhi ya watu huwa wazito katika ziara; hukaa muda mrefu kwa mgonjwa, jambo ambalo linapingana na mwongozo wa Uislamu katika kumtembelea mgonjwa, na hata katika ziara kwa ujumla. Miongoni mwa adabu muhimu ni kumtia mgonjwa matumaini ya kupona kwa idhini ya Allah, na kutomuumiza kwa kumkumbusha waliokufa kwa ugonjwa huo.
Mtume wa Allah amesema: “Mnapomtembelea mgonjwa, mtieni matumaini ya kuishi; kwani hilo halizuii chochote (kilichoakadiriwa na Allah), lakini humfariji moyo wa mgonjwa.” 0712 690811