Fahamu mzunguko sahihi kwa mwezi

Fahamu mzunguko sahihi kwa mwezi

Muktasari:

  • Kwa kawaida hedhi si ugonjwa, bali kuna sababu mbalimbali zinazochangia baadhi ya wanawake kupata matatizo yanayotokana na hedhi.

  

Kwa kawaida hedhi si ugonjwa, bali kuna sababu mbalimbali zinazochangia baadhi ya wanawake kupata matatizo yanayotokana na hedhi.

Baadhi ya matatizo hayo ni kutokwa damu nyingi kupita kiasi, kutokwa damu katikati ya mwezi, kukosa hedhi na maumivu makali wakati wa hedhi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Living Colman akizungumza na Jarida la Afya anasema ikiwa mwanamke au msichana anapata hedhi chini ya siku 21 au zaidi ya siku 35 kwa mwezi kimzunguko atakuwa na tatizo.

Pia ikitokea akapata hedhi chini ya siku nne au zaidi ya siku nane za kawaida, nalo ni tatizo.

“Pia iwapo damu itakuwa kidogo au nyingi zaidi ya glasi moja, atahesabika kuwa na tatizo katika uwiano wa homoni, hivyo anashauriwa kuwaona wataalamu wa afya,” anasema.

Dk Colman anasema uwiano wa homoni ambazo zipo kwenye mfumo au mpangilio maalumu kutoka kwenye ubongo mpaka kwenye mayai usipokuwa sawa huleta shida katika mzunguko.

Anasema kuwa katika mpangilio kuna amri hutolewa katika ubongo mpaka kwenye mayai kuhakikisha yanatoa homoni na kutengeneza ukuta wa kizazi, kizazi ni muhimu kuwepo ili mtu aone hedhi.

“Kukiwa na hitilafu yoyote kuamrisha yale mayai au taarifa zikiwa pungufu zitatoa homoni pungufu. Umuhimu wa ile hedhi huyu mwanamke anaandaliwa kila mwezi apate ujauzito na sehemu ya kumhifadhi mtoto, ikitokea mimba haikutungwa lile eneo lililoandaliwa linatolewa, kwa hiyo matokeo yake ndiyo hedhi,” anafafanua.

Dk Colman anasema kama kulikuwa na hitilafu sehemu ya ubongo au mayai hayapokei taarifa kutengeneza homoni au kizazi kimeziba au anavyo viwili, inakuwa ngumu kupata hedhi ya kawaida, itazidi sana, itapungua au inakuwa na maumivu makali.

Anasema mara nyingi wanaopata maumivu huwa hawapati kabisa hedhi au wanapata kidogo kidogo na wengi hupata maumivu makali ambayo yanamfanya ashindwe kufanya mambo mengine.

“Maumivu yana sababu za moja kwa moja na zile ambazo huwezi kuzizungumzia, wengi hupata maumivu kutokana na uzalishwaji wa kemikali ambazo zinakuwa kwenye ukuta wa kizazi, lakini ili hedhi itoke kama kuna vitu mbalimbali kama PID, uvimbe kwenye kizazi, mirija ya kizazi imejipenyeza ndani au zipo nje ya kizazi anaweza kupata mauivu makali,” anasema Dk Colman.

Dk Colman anasema ikiwa mwanamke ataona baadhi ya dalili za kupata damu ya hedhi siku chache baada ya kumaliza hedhi huwa ni matokeo ya mvurugiko wa homoni.

“Hii hutokea iwapo una msongo wa mawazo, wakati mwingine homoni hazijazalishwa katika uwiano unaokubalika, matokeo yake zile homoni kwa kuwa hazijajijenga vizuri zitaendelea kidogo kidogo.

“Ikiwa pia mwanamke anaona siku zake baada ya wiki moja au mbili anaona tena au siku 14 anaona kidogo, huyu ana tatizo lakini katika tiba pia tunaangalia umri wa tatizo, hasa miaka 30 na kuendelea huyu lazima sababu itakuwa ni vivimbe kwenye kizazi,” anasema.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Nathanael Mtinangi anasema kwa kawaida mwanamke anapopevuka huanza kwa kuvunja yai moja kila mwezi.

“Mwanamke anatoa yai moja kwa mwezi, kwa mwaka anatoa mayai 12 na uzao wa mwanamke ni kwa kipindi cha miaka 30.

“Akipevuka na miaka 15 mpaka anafikisha miaka 45, tayari ni miaka 30, ukizidisha mara 12 utaona ana mayai 360, huu ni wastani. Wapo wanawake wengine wana mayai zaidi na wengine wana pungufu,” anasema Dk Mtinangi.

Magonjwa yatokanayo na hedhi

Akizungumzia magonjwa ambayo mwanamke anaweza kuyapata kutokana na hedhi, Dk Mtinangi anasema kama atatokwa na damu nyingi kuna uwezekano akapata tatizo la upungufu wa damu ‘anaemia’ ambalo pia husababisha tatizo la kufeli kwa moyo.

Anasema tatizo hilo lisipodhibitiwa vizuri, huweza kusababisha matatizo katika figo.

Dk Colman anasema kama damu itapungua kwa kiasi kikubwa na mhusika hajapata usaidizi au tiba anaweza kupata matatizo makubwa zaidi.

“Akiona ana tatizo hilo, ni lazima aonane na wataalamu ili wafanye uchunguzi wagundue aina ya tatizo alilonalo na matibabu yaanze, mabinti wadogo walio wengi wanapovunja ungo wakiwa na miaka 12 mpaka 22 hupata tatizo la homoni.

“Hawa mara nyingi unakuta mfuko haujakomaa vizuri au homoni zimepungua au zimezidi, anapata maumivu au damu nyingi. Akiwahi hospitali atachunguzwa na kupatiwa tiba kwa wakati, hivyo anaepukana na magonjwa sugu kama moyo na figo,” anasema.

Epuka pedi muda mrefu

Dk Colman anasema kuna madhara ya kukaa na kitambaa au pedi muda mrefu bila kubadilisha wakati wa hedhi.

“Hedhi inapotoka inakuwa ni kama uchafu, ikikaa muda mrefu inatengeneza chakula cha bakteria na ndiyo maana huona inatoa harufu.

“Hapo bakteria watajitengeneza, mtu anaweza kupata maambukizi katika njia ya mkojo (UTI) au kwenye uke baadaye yakapanda mpaka kwenye kizazi, mirija akapata PID,” anasema.