Faida, hasara kuvunjwa Jiji la Dar es Salaam

Faida, hasara kuvunjwa Jiji la Dar es Salaam

Muktasari:

  • Jana Jumatano Februari 24, 2021 Rais John Magufuli alivunja Jiji la Dar es Salaam akisema halina miradi yoyote ya maendeleo linayotekeleza badala yake madiwani wanachangiwa fedha za kulipana posho.

Dar es Salaam. Jana Jumatano Februari 24, 2021 Rais John Magufuli alivunja Jiji la Dar es Salaam akisema halina miradi yoyote ya maendeleo linayotekeleza badala yake madiwani wanachangiwa fedha za kulipana posho.

Kufuatia uamuzi huo, Rais ameipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia jana.

Meya wa zamani wa manispaa ya Ubungo na mjumbe wa halmashauri hiyo (2016 na 2019), Boniface Jacob amesema faida ya kwanza ni Serikali kupunguza gharama za uendeshaji, ikiwamo magari, mafuta, machapisho, posho za watumishi na madiwani pamoja na nyumba walizokuwa wakiishi wakuu wa idara wa jiji hilo.

“Serikali itaondokana na gharama hizi na itafaidika,” amesema Jacob, ambaye aliwahi kuwa meya wa Manispaa za Kinondoni.

Kwa mujibu wa Jacob, hasara itakayopatikana ni kuondoka kwa historia ya Jiji la Dar es Salaam iliyokuwapo tangu ukoloni na baada ya Uhuru wa Tanganyika.

“Kimuundo na utawala halmashauri moja itafaidika kuliko nyingine itakayoteuliwa kuwa jiji. Kwa sababu itapata mali mbalimbali zinazohamishika, ikiwamo magari, pia kuna baadhi ya halmashauri hazitahesabika kuwa zipo kwenye jiji.”

“Mbali na hilo, jiji la Dar es Salaam litaondoka kwenye orodha ya majiji bora Afrika na duniani,” amesema Jacob.

Historia Jiji la Dar es Salaam

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa inaliongoza Jiji kutoka mwaka 1961 mpaka mwaka 1972 ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilizivunja Halmashauri zote nchini na kuwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu.

Serikali kuu ilizirudisha Serikali za mitaa nchini chini ya sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) namba 8 mwaka 1982 ambapo Halmashauri ya Jiji ilianza kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma kwa wananchi kuanzia mwaka 1983.

Mwaka 1996 Serikali kuu iliivunja Halmashauri ya Jiji na kuunda Tume ya Jiji la Dar es Salaam kwa Tangazo la Serikali namba 110 na 11 ya Juni 28, 1996.

Tume ya Jiji ilifanya kazi kwa kipindi cha miaka minne ambapo mwaka 2000 Serikali iliunda mamlaka nne za Serikali za mitaa (mamlaka ya miji) namba 8 ya mwaka 1982 kama ilivyo rekebishwa kwa sheria namba 6 ya mwaka 1999.

Ulivyokuwa mgawanyo Halmashauri sita

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

Halmashauri ya manispaa ya Temeke

Halmashauri ya manispaa ya Kinondoni

Halmashauri ya manispaa ya Ilala

Halmashauri ya manispaa ya Ubungo

Halmashauri ya manispaa ya Kigamboni