Familia ya muuguzi aliyetoweka KCMC sasa kutumia taratibu za kimila kumsaka
Muktasari:
- Tayari zimepita siku 23 tangu kutoweka kwa Muuguzi wa Hospitali ya KCMC, Lenga Masunga na sasa familia yake imesema itatumia taratibu za kimila kumtafuta na kujua yupo hai au amefariki dunia.
Moshi. Wakati Jeshi la Polisi likisema linafuatilia mawasiliano ya mwisho na watu aliokuwa akiwasiliana nao Muuguzi wa KCMC, Lenga Masunga (38) aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha hivi karibuni, familia yake imesema itatumia taratibu zake za kimila kujua ndugu yao huyo yuko hai au amefariki dunia.
Muuguzi huyo wa idara ya masikio, pua na koo (ENT), anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, mwaka huu nyumbani kwake Mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokuwa akiishi.
Taarifa iliyotolewa na Hospitali ya KCMC, ilisema Masunga alikuwa na mapumziko ya siku mbili, Julai 2 na 3 na alitakiwa kuwepo kazini Julai 4, mwaka huu, lakini hakuonekana hali iliyoibua mashaka na kusababisha uongozi wa hospitali hiyo kumtafuta kupitia simu zake za mkononi ambazo hazijapatikana hewani mpaka sasa.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Jumatano Julai 24, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kutoweka kwa muuguzi huyo na kwamba wanachokifanya sasa, ni kufuatilia mawasiliano yaliyofanyika siku aliyotoweka.
"Tunaendelea kufuatilia mawasiliano yake ya simu kwa ukaribu kujua watu aliowasiliana nao mara ya mwisho wakati anatoweka, maana mpaka sasa simu zake hazijapatikana," amesema Maigwa.
Ameitaka jamii kuendelea kuwa na subira kwa kuwa jambo hilo linahitaji muda wa kulichunguza.
Akizungumzia hilo, kaka wa muuguzi huyo, Paschal Jeremiah amesema familia bado imeshikwa na mtanziko kuhusiana na kupotea kwa ndugu yao huyo.
Amesema wanakusudia sasa kutumia “taratibu zao za kimila” ili kubaini wapi alipo ndugu yao huyo.
"Mpaka sasa hivi bado hatujampata, tumemtafuta kwa kila namna hapatikani, tumeamua kutumia utaratibu wa kimila kumtafuta ili kujua alipo ndugu yetu, kama yupo hai au la!" amesema Jeremiah bila kufafanua njiahizo za kimila.
Amesema wazazi wake hawalali wamejawa na simanzi hali inyoifanya familia nzima kukosa amani.
Masunga ambaye alikuwa amtolee mahari mchumba wake, Neema Mmasy, alitoweka nyumbani na kuacha mlango wazi huku baadhi ya vitu vyake yakiwamo mabegi vikiwa vimepekuliwa.