Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Foleni malori Dar inavyokwamisha utoaji huduma-2



Dar es Salaam. Baada ya uchunguzi wa Mwananchi kuonesha baadhi ya madereva wa malori husimama kwa siku kadhaa katika maeneo ya bandari kavu wakisubiri mizigo, imebainika hali hiyo si chanzo cha foleni pekee, bali pia inaathiri utoaji wa huduma za dharura, shughuli za kiuchumi na maisha ya kila siku ya wananchi.

Kwa mujibu wa wananchi, watoa huduma za usafiri, viongozi wa Serikali za mitaa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, msongamano wa malori katika baadhi ya maeneo ya jiji ni kikwazo kwa huduma muhimu, huku Serikali na wadau wakitafuta suluhisho la kudumu.

Katika sehemu ya kwanza ya uchunguzi huu, Mwananchi ilibaini baadhi ya madereva hulazimika kusimama kwa muda mrefu kandokando ya barabara wakisubiri mizigo kutokana na uhaba wa maegesho, ucheleweshaji wa huduma za kupakia na kushusha mizigo pamoja na utaratibu wa kusubiri ‘michongo.’

Uchunguzi huo pia, ulionesha ongezeko la mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam limeongeza shinikizo kwa bandari kavu na miundombinu inayozihudumia.


Ni maumivu kwa huduma nyingine

Dereva wa bajaji, Mwinjuma Masumbuko anasema msongamano wa malori katika Barabara ya Kilwa umeendelea kuathiri usafiri wa abiria na shughuli za kiuchumi.

Anasema wakati mwingine foleni huanzia Gerezani hadi Sabasaba, hali inayofanya safari za kawaida kuchukua muda mrefu.

“Ukiangalia foleni hii imeanzia Gerezani hadi hapa Sabasaba, mtu anayepanda usafiri kwenda Kariakoo unaweza kujiuliza atafika saa ngapi,” anasema.

Anasema changamoto huwa kubwa zaidi asubuhi na jioni na huathiri watoa huduma za usafiri pamoja na wananchi wanaorejea makwao.

Mkazi wa Mbagala, Erick Gervas anasema foleni hizo ni kero kwa wananchi na wafanyabiashara kutokana na miundombinu kutokidhi mahitaji ya sasa ya usafiri.

“Wakati mwingine wananchi hulazimika kutembea kwa miguu kutokana na magari kusimama kwa muda mrefu,” anasema.


Zimamoto wanena

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Temeke limesema maegesho holela ya malori ni kikwazo kikubwa katika utoaji wa huduma za uokoaji wakati wa matukio ya moto na dharura nyingine.

Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo, Boniface Adhiri anasema mara kadhaa magari ya zimamoto hukwama njiani kutokana na malori kuegeshwa bila kuzingatia njia za kupita kwa magari ya uokoaji.

“Tunapokea taarifa za moto na kuanza safari kuelekea eneo la tukio, lakini tunakutana na barabara zilizozibwa na malori yaliyopaki hovyo. Hali hiyo hutulazimu kutafuta namna ya kuyaondoa kabla ya kuendelea na safari ya uokoaji,” anasema.

Anasema katika matukio ya moto kila dakika ni muhimu na kuchelewa kufika eneo la tukio huongeza uwezekano wa moto kusambaa na kusababisha hasara kubwa.

Adhiri anasema changamoto hiyo ni kubwa zaidi katika maeneo yenye msongamano wa malori yanayosubiri kupakia au kushusha mizigo, huku baadhi ya madereva wakiondoka na kuyaacha magari yao kwa muda mrefu.

“Wakati mwingine askari hulazimika kutafuta mmiliki wa lori ili liondolewe, zoezi linalochukua muda wakati huduma ya dharura inahitajika,” anasema.

Adhiri anawataka madereva na wamiliki wa malori kuzingatia taratibu za maegesho na kuacha nafasi ya kutosha kwa magari ya uokoaji kupita wakati wowote.


Kilio cha Serikali ya mtaa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sandali na Katibu wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Kata ya Sandali, Habibu Ndege anasema changamoto hiyo imekuwa kero kwa wakazi wa kata hiyo na athari zake zinaonekana katika mitaa yote minane.

Anasema kwa miaka kadhaa wananchi wamekuwa wakikumbana na adha ya foleni zinazosababishwa na malori yanayoelekea maeneo ya kuhifadhi na kushughulikia mizigo.

“Kero ya malori ni kubwa. Watu wanapata shida kufika kazini, kwenye vituo vya usafiri na kufanya shughuli zao za kila siku,” anasema.

Ndege anasema licha ya maboresho yaliyofanyika katika baadhi ya maeneo, tatizo bado linaendelea kwenye barabara zinazotumiwa na malori mengi.

“Tulipeleka malalamiko katika vikao mbalimbali na kuahidiwa ufumbuzi, lakini wananchi bado wanaendelea kupata usumbufu,” anasema.

Anataja pia athari kwa huduma za dharura, akieleza wakati mmoja gari lililokuwa likimpeleka mjamzito hospitalini lilikwama kutokana na msongamano wa malori.

Mbali na hilo, anasema uwepo wa shule na zahanati katika kata hiyo unaongeza hatari kwa wanafunzi wanaotumia barabara hizo kila siku.

“Watoto wanapata wakati mgumu kuvuka barabara na wengine huchelewa kufika shuleni kutokana na msongamano wa malori,” anasema.


Taasisi ya madereva

Naibu Katibu wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania (Chamamata), Muhidini Sangoti anasema sehemu ya tatizo inatokana na baadhi ya madereva kufika maeneo ya kupakia mizigo kabla ya taratibu za upakiaji kukamilika.

Anasema kampuni za usafirishaji zinapaswa kuyaweka magari katika yadi zao na kuyaita pale vibali na mizigo vinapokuwa tayari.

“Dereva anatoka na gari mapema, anakwenda kuliegesha nje ya ICD au ghala akisubiri vibali. Hapo ndipo msongamano unaanza kujitokeza,” anasema.

Sangoti anasema suluhisho linahitaji ushirikiano wa Serikali, mamlaka za jiji, kampuni za usafirishaji, waendeshaji wa ICD na madereva wenyewe.

Anasema uboreshaji wa miundombinu pamoja na nidhamu katika shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo ni muhimu ili kupunguza foleni na kuongeza ufanisi wa shughuli za uchumi.


Wamiliki wa malori wajibu

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani anasema kumekuwa na vikao kati ya Serikali na wadau wa usafirishaji kutafuta suluhisho la muda mrefu la msongamano wa malori.

Anasema baada ya majadiliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi aliongoza ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ili kubaini maeneo yanayoweza kutumika kama maegesho ya malori.

Anasema baadhi ya maeneo tayari yameainishwa na hatua za awali za upimaji zimekamilika huku mchakato wa kutafuta wawekezaji ukiendelea.

“Hii si kwa ajili ya malori ya transit pekee, bali malori yote yanayoingia au kutoka Dar es Salaam ili kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa shughuli za uchumi,” anasema.

Hata hivyo, anasema changamoto hiyo haiwezi kutatuliwa kwa kutenga maegesho pekee bila kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yanayohifadhi makontena.

“Lazima upangaji wa maeneo ya ICD uende sambamba na uwekezaji wa miundombinu. Vinginevyo malori yataendelea kuingia katika maeneo ya makazi na kuzua malalamiko,” anasema.

Pia anakosoa baadhi ya madereva wanaoegesha malori karibu na maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo vituo vya zimamoto.


Tanroads wachukua hatua

Msimamizi wa Idara ya Mipango Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Clever Akilimali anasema kuondoa malori katika hifadhi za barabara ni shughuli endelevu inayofanyika katika maeneo mbalimbali.

“Tumekuwa tukiwatoa madereva wanaoegesha malori katika maeneo yanayosababisha msongamano wa barabara na zoezi hili litaendelea,” anasema.

Simu moja baada ya Mwananchi kuandika habari ya maegesho ya malori barabarani, Meneja wa Tanroads Dar es Salaam, Mhandisi Lazeck Kyamba anasema wanaendesha operesheni maalumu ya kuzuia na kuondoa malori yaliyoegeshwa kinyume na taratibu eneo la Mbagala Zakhiem.

Anasema kumekuwa na ongezeko la malori yanayotumia barabara na kusimama eneo hilo huku shughuli mbalimbali za usafirishaji zikiendelea.

Kyamba anasema hali hiyo imekuwa ikichangia msongamano wa magari na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

 Anasema baadhi ya madereva wamekuwa wakiegesha malori katika maeneo yasiyoruhusiwa, ikiwamo kwenye barabara saidizi, jambo linaloathiri matumizi sahihi ya miundombinu ya barabara na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.

 Pia, anawahimiza madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kuepuka kuegesha magari maeneo yasiyoruhusiwa ili kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote.

 Meneja anasisitiza kuwa, operesheni hizo zitaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuhakikisha sheria za matumizi ya barabara zinazingatiwa na kuondoa changamoto zinazotokana na maegesho holela ya malori.

 “Lengo letu ni kuhakikisha barabara zinatumika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Tunawaomba madereva wote kushirikiana nasi kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.”


Mipango ya Tasac

Mei 8, 2026, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) lilisema limeanza kujadili changamoto za uanzishwaji na uendeshaji wa bandari kavu ili kutafuta suluhu ya foleni ya malori jijini Dar es Salaam.

Tasac ilitaja changamoto zinazojitokeza kuwa ni ongezeko la msongamano wa magari, ucheleweshaji wa upatikanaji wa mizigo kwa wateja, kuongezeka kwa gharama na uwezo mdogo wa baadhi ya bandari kavu kuhudumia mizigo mingi.

Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum anasema wingi wa makontena yanayoingia nchini unachangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo.

“Ili kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza kero, ni muhimu wadau wote kushirikiana kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuzingatia sheria na kanuni,” anasema.

Kwa mujibu wa Tasac, Temeke ndiyo yenye bandari kavu nyingi zaidi ikiwa na 74 sawa na asilimia 64.3 ya zote zilizopo Dar es Salaam.

Takwimu hizo zinaonesha pia kuwa uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam unaendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 16 kila mwaka na unatarajiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka 2030.

Itaendelea kesho