Fredrick Lowassa aweka rehani ubunge wake

Mbunge wa Monduli, Frederick Lowassa akisalimiana na Wananchi kata ya Esilalei baada ya kuwasili kukagua mradi wa shule ya Laiboni. Picha na Bertha Ismail

Muktasari:

  • Asema aliachiwa wosia na baba yake, hayati Edward Lowassa kwenye moja ya kampeni, ahakikishe wananchi wanapata haki zao.

Monduli. Mbunge wa Monduli (CCM), Fredrick Lowassa ameahidi kuachia ubunge wake endapo utatuzi wa mgogoro wa Ranchi ya Manyara aliyoianzisha baba yake, hayati Edward Lowassa hautafika mwisho mwaka huu, 2024 na wananchi kunufaika nayo.

Fredrick amesema mgogoro huo uliodumu kwa miaka 26 sasa, kati ya vijiji vya Ortukai na Esilalei vilivyopo Kata ya Esilalei wilayani Monduli mkoani Arusha na Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT), ulikuwa ukifuatiliwa na hayati Lowassa, aliyekuwa mbunge wa Monduli.

Fredrick amesema hayo leo Aprili 21, 2024 katika shule ya Laiboni iliyoko kitongoji cha Esmit alichokitembelea akiwa ziarani kufuatilia miradi na kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM.

Pia amezungumza na wananchi kujua matatizo yanayowakabili ili ayafikishe bungeni.

“Baba yangu amepigania haki zenu kuhakikisha shamba hili linarudi kwenye umiliki wa vijiji vyenu, na mnanufaika nazo, hadi amekufa amefanikisha hati imerudi serikalini kupitia halmashauri yetu,” amesema.

“Ameniachia wosia kwenye moja ya kampeni zangu kuwa nihakikishe mnapata haki zenu. Na mimi ninaahidi kuhakikisha kabla ya mwaka huu kwisha, mnapata haki zenu na mnanufaika na shamba hili,” amesema Fredrick.

Amesema kibarua alichoachiwa anataka kukitendea haki, kuhakikisha wananchi wananufaika na ardhi ya Ranchi ya Manyara hasa kimapato.

“Hii ni kama laana ameacha baba yangu mzazi, na nataka niwaambie, yamesemwa mengi lakini puuzeni, nataka niwahakikishie mtanufaika na ardhi ile na nisipofanikiwa mwaka huu ni bora niachie ubunge wangu,” amesema Fredrick.

Awali, eneo la Ranchi ya Manyara lenye ukubwa wa ekari 44,930 lilikuwa linamilikiwa na TLCT bila wananchi wa vijiji husika kunufaika wala kuendelezwa, hali iliyozua mgogoro.

Mwaka 2016, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimaliza mgogoro huo wa ardhi baada ya kukabidhi hati ya eneo hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli baada ya kubadilishwa umiliki wake kutoka TLCT kwenda kwa wananchi wa vijiji hivyo.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imeamua kurudisha umiliki wa eneo hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili kupitia Halmashauri ya Monduli, ambayo ingepanga matumizi bora ya ardhi.

Licha ya maelekezo hayo, wananchi mara kadhaa wamelalamika viongozi wa halmashauri kuhodhi eneo hilo kwa miaka minane bila kukabidhi kwa uongozi wa vijiji, huku mapato yanayopatikana yakiwa hayawanufaishi, hivyo wamekuwa wakiitaka Serikali kupitia Waziri wa Ardhi kushughulikia suala hilo.

Awali, akisoma risala ya Shule ya Msingi Laiboni iliyotembelewa na mbunge huyo Mkuu wa shule hiyo, Mimutie Lengiteng' amesema ina wanafunzi 405 na inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji na hati miliki ya eneo la shule.

“Tunaomba utusaidie fedha za kumalizia nyumba ya walimu, iliyoanza kwa nguvu ya wananchi,” amesema.

Amesema walimu wamekuwa wakipata shida kuwahi shuleni kutokana na kuishi mbali na shule.

Fredrick ameahidi kuchangia Sh10 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo ya walimu kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.